ANGALIA LIVE NEWS

Friday, February 16, 2018

KWANDIKWA : WATENDAJI WA TAASISI ZA WIZARA TIMIZENI WAJIBU WENU KUFANIKISHA TANZANIA YA VIWANDA.

 Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwa akisalimiana na Watendaji wa Taasisi zilizopo chini ya Wizara hiyo ikiwemo TBA, TANROADS na TEMESA wakati wa mkutano wa majumuisho ya ziara yake ya kukagua miradi mbalimbali ya sekta za ujenzi inayosimamiwa na Wizara hiyo jana Alhamisi Februari 15, 2018. Kulia kwake ni Meneja wa TANROAD Mkoa wa Tanga, Mhandisi Alfred Ndumbaro.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwa akizungumza na Watendaji wa Taasisi zilizopo chini ya Wizara hiyo ikiwemo TBA, TANROADS na TEMESA wakati wa mkutano wa majumuisho ya ziara yake ya kukagua miradi mbalimbali ya sekta za ujenzi inayosimamiwa na Wizara hiyo.


Na Ismail Ngayonga
NAIBU Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwa amewataka Watendaji wa Taasisi zilizopo chini ya Wizara hiyo kutumia weledi, maarifa na ujuzi walionao ili kufanikisha adhma ya Tanzania kuwa nchi ya kipato cha kati kupitia uchumi wa viwanda.

Akizungumza katika kikao cha majumuisho ya Zaira yake ya kukagua miradi ya sekta ya ujenzi Mkoani Tanga na Watendaji wa Wizara hiyo, jana Alhamisi Februari 15, 2018, Naibu Waziri Kwandikwa amewataka Watendaji hao kubuni mipango na mikakati mbalimbali itayoweza kulisaidia Taifa.
Alisema  Watendaji wa Taasisi zilizopo chini ya Wizara hiyo ikiwemo Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) na Wakala wa Ufundi na Umeme Serikalini (TEMESA) wana wajibu mkubwa wa kutimiza matarajio hayo yaliyowekwa na Serikali katika kufikia nchi ya kipato cha kati.
Kwa mujibu wa Kwandikwa alisema, Wizara hiyo imekuwa na watalaamu wa kutosha na wenye weledi ambao wamekuwa tegemeo kubwa katika Taifa, hivyo ni wajibu wa Watendaji hao kufanya kazi kwa bidii kwa kutumia vipaji vyao badala ya kuacha ujuzi na maarifa waliyonayo yakipotea bila ya kuinufaisha.
“Wizara hii, imekuwa tegemeo katika sekta zote za kiuchumi, hususani wahandisi tulionao katika Taasisi zetu, hivyo ni vyema tuhakikishe kuwa utaalamu huu unaweza kuleta matokeo chanya katika Taifa letu ikizingatia kuwa Tanzania ya Uchumi wa Viwanda itagemea sana Wataalamu wengi kutoka Wizara yetu” alisema Kwandikwa.
Aidha Kwandikwa alisema Wizara yake inatambua Changamoto mbalimbali zinazowakabili watendaji waliopo katika Taasisi zake ambapo hata hivyo Serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbaili katika kuhakikisha kuwa Watumishi hao wanafanya kazi katika mazingira mazuri yanayozingatia maslahi na mahitaji yao.
Akifafanua zaidi Kwandikwa alisema ili matarajio hayo yawezwe kufikiwa ni wajibu wa Watendaji wote wa Wizara hiyo kufanya kazi kwa ushirikiano wa pamoja katika maeneo yao hatua inayowezesha kubaini changamoto zinazowakabili na hivyo kuzipatia ufumbuzi za kudumu.
Kwandikwa pia aliwataka Watendaji wa Wizara hiyo kuwa na utaratibu wa kujitafakari katika maeneo yao ya kazi na kutathimini mchango wao katika kulisaidia Taifa, kwa kuwa mkakati huo mikakati hiyo utaisadia Serikali kutekeleza vyema mipango yake hususani katika kuinua uchumi wa wananchi.
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa TBA Mkoa wa Tanga, Edward Ngowi alisema wamepokea kwa mikono miwili ushauri na maelekezo ya Naibu Waziri kwa kuwa ziara yake pia imekuwa somo na chachu ya mabadiliko ya utendaji kazi kwa Watumishi wa Taasisi za Wizara hiyo katika kutekeleza majukumu yao.
Ngowi alisema watendaji wa Taasisi hizo watahakikisha kuwa wanafanya kazi kwa bidii pamoja na kuzingatia sheria, taratibu na kanuni zilizopo ili kuhakikisha kuwa wataleta tija na matokeo chanya katika maendeleo ya sekta ya ujenzi nchini.

No comments: