ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, March 20, 2018

DC SHINYANGA AFUNGA MAFUNZO KWA VIKUNDI VYA WAJASIRIAMALI WANAWAKE NA VIJANA

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro amefunga mafunzo kwa vikundi vya wajasiriamali vya wanawake na vijana manispaa ya Shinyanga yaliyolenga kuwajengea uwezo wa namna ya kutumia vizuri fedha za mikopo walizopewa na manispaa hiyo.

Mafunzo hayo ya siku tatu yamefanyika katika ukumbi wa Lewis Kalinjuna uliopo katika ofisi za manispaa ya Shinyanga na kuhudhuriwa na wanawake na vijana 60 kutoka vikundi 20 vya wajasiriamali ambao wamepata mikopo ya shilingi milioni 125.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo leo Jumatatu Machi 19,2018 Matiro aliwataka vijana na wanawake hao kutumia fedha walizopewa kwa malengo waliyokusudia na kuhakikisha wanaanzisha viwanda vidogo vitakavyoinua uchumi wao.
“Tumieni mikopo hii kwa ajili ya kuanzisha viwanda vidogo ili kumuunga mkono rais wetu mpendwa Dkt. John Pombe Magufuli anayetaka Tanzania iwe nchi ya viwanda,pale mnapokwama tafadhali wasilianeni na viongozi wa serikali,tutawasaidia na pia tutatembelea miradi yenu ili tujue mnachofanya”,alisema Matiro.
Aidha aliwataka vijana na wanawake kujitokeza kwa wingi kuomba mikopo kwenye halmashauri za wilaya ,mikopo ambayo haina masharti magumu wala riba kubwa ukilinganisha na taasisi za kifedha (benki).
“Msikubali kukata tama kwamba maisha ni magumu,hata siku moja serikali haiwezi kugawa pesa kwa mtu mmoja mmoja,anzisheni vikundi vya ujasiriamali,kisha ombeni mikopo kwenye halmashauri,pesa zipo”,aliongeza Matiro.
Kaimu Afisa Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Shinyanga Octavina Kiwone alisema vikundi hivyo vimepata mkopo wa shilingi milioni 125 kutoka mfuko wa wanawake na vijana ikiwa ni asilimia 10 ya mapato ya ndani ya manispaa hiyo.
“Katika mwaka wa fedha 2017/18 manispaa imelenga kutoa shilingi milioni 208 kwa ajili ya vijana na wanawake,katika awamu hii ya kwanza tumetoa shilingi milioni 125 kwa vikundi 11 vya wanawake na 9 vya vijana”,alieleza Kiwone.
“Baada ya kutoa mikopo hiyo,tumeona ni vyema tuwape elimu ya kuhusu namna ya kunufaika na mikopo,mafunzo yamedumu kwa muda wa siku tatu,na kipaumbele cha manispaa ya wajasiriamali kuanzisha viwanda vidogo vidogo”,aliongeza Kiwone.
Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya vijana Manispaa ya Shinyanga,Charles Luchagula alisema manispaa hiyo inaendelea kupokea maombi ya mikopo kwa vijana na wanawake ili kujiinua kiuchumi na kujikimu kimaisha.
Nao washiriki wa mafunzo hayo walisema kupitia mafunzo hayo ya siku tatu wamepata elimu kuhusu namna ya kuanzisha biashara na kutafuta masoko,kutengeneza mnyororo wa thamani kutunza kumbukumbu na vifungashio na umuhimu wa uwekaji lebo.
Walisema pia wamejifunza taratibu za utoaji wa mikopo na urejeshaji wa mikopo,wajibu wa kiongozi wa kikundi,ukweli kuhusu Ukimwi,ukatili dhidi ya wanawake na watoto pamoja na elimu kuhusu mfuko wa bima ya afya (CHF iliyoboreshwa.
Washiriki wa mafunzo kwa vikundi vya wajasiriamali vya wanawake na vijana  wa manispaa ya Shinyanga wakiwa wamesimama baada ya mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro kuingia ukumbini kwa ajili ya kufunga mafunzo hayo.Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akiwasisitiza wanawake na vijana kutumia kwa malengo yaliyokusudiwa pesa za mikopo walizopata
Washiriki wa mafunzo hayo wakiwa ukumbini.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akiimba wimbo kuhusu wanawake ...."Wanawake wote hongeraa...."
Kaimu Mkurugenzi wa manispaa ya Shinyanga Rajabu Masanja akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo.
Kaimu Afisa Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Shinyanga Octavina Kiwone akielezea lengo la mafunzo hayo ya siku tatu. Alisema lengo  ni kuwajengea uwezo  wanufaika wa mkopo huo kutumia vizuri fedha walizopata.
Afisa Maendeleo ya vijana Manispaa ya Shinyanga,Charles Luchagula akiwasisitiza wanawake na vijana kutumia fedha walizopata kuanzisha viwanda vidogo.
Washiriki katika mafunzo hayo wakiwa ukumbini.
Washiriki wa mafunzo hayo wakijaza mkataba wa mkopo waliopata katika kikundi chao
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog

No comments: