ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, March 17, 2018

SHUWASA YATOA ELIMU YA MAJI KWA WANAFUNZI SHULE YA SEKONDARI MWASELE SHINYANGA


Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Shinyanga (SHUWASA) imetoa elimu ya huduma za maji kwa wanafunzi 727 wa shule ya sekondari Mwasele iliyopo katika kata ya Mwasele Manispaa ya Shinyanga.


Elimu hiyo imetolewa leo Ijumaa Machi 16,2018 ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya wiki ya Maji inayoendelea nchini.
Akizungumza shuleni hapo,Afisa rasilimali watu na utawala kutoka SHUWASA,Kambira Mtebe alisema mamlaka hiyo inaendelea kutoa elimu ya huduma za maji kwa jamii ili kuhakikisha wateja wanapata huduma bora.
“Tumefika hapa kuwapeni elimu ya huduma za maji tunazotoa kwani nyinyi ni miongoni mwa wadau wetu wakubwa na tunatambua kuwa mtakuwa mabalozi wazuri katika familia mnazoishi”,alieleza Mtebe.
“Wajibu wa SHUWASA ni kutoa huduma bora ya maji na kuhakikisha tunamtua ndoo kichwani mwanamke,hivyo ni lazima tushirikiane na wadau wetu katika kufanikisha malengo haya”,alisema.
Mtebe aliwahamasisha wateja kuokoa muda kwa kutumia huduma njia ya mtandao wa simu na benki kulipia ankara za maji badala ya kupanga foleni kwenye dirisha la SHUWASA.
“Tumeboresha huduma zetu kwa kiwango cha juu,sasa unaweza kulipia ankara ‘Bill ya maji’ kwa njia ya Tigo- Pesa,M-pesa,benki ya CRDB,NMB au kwa mawakala wa NMB au Fahari Huduma”,alisema Mtebe.
Aidha aliwataka wateja kulipia ankara za maji kwa wakati ili kuepuka usumbufu wa kukatiwa huduma na inapotokea mteja amekatiwa huduma ya maji basi asichanganye faini kwenye malipo ya ankara za maji.
“Tunawashauri wateja wetu kulipa ankara za maji kwa wakati ili kuepuka usumbufu unaojitokeza, na ikitokea umekatiwa huduma ya maji,usilipe faini kwa mfumo wa ankara kwani itaingia kwenye ankara,unachotakiwa kufanya ni kufika ofisini na kulipa faini yako kwani mifumo haiingiliani”,alieleza Mtebe. 
Kwa upande wake,Kaimu Afisa Mawasiliano SHUWASA, Hadija Mabula ambaye pia ni Afisa huduma kwa wateja SHUWASA, aliwataka wateja kulinda na kutunza miundombinu ya maji na kama kuna uharibifu wawasiliane na SHUWASA.
Mabula alitoa rai kwa wananchi kuwafichua watu wanaohujumu miundombinu ya maji na wezi wa maji na kuweka utaratibu wa kusoma dira za maji mara kwa mara.
“Niwakumbushe tu kuwa marekebisho ya mita/dira za maji kufanywa na mafundi kutoka SHUWASA,usiruhusu mtu kutoka mtaani afanye marekebisho kwenye dira ya maji”,alieleza.
Nao wanafunzi wa shule hiyo,waliishukuru SHUWASA kwa kuwapa elimu kuhusu maji kwani wao ni sehemu ya jamii na wateja wakubwa wa mamlaka hiyo.
“Sisi tunatumia maji kila siku,elimu hii itatusaidia kwa kiasi kikubwa katika maisha yetu katika kupata huduma bora ya maji na kuepuka mambo ambayo yamekuwa yakifanya ankara za maji zinakuwa kubwa”,walieleza wanafunzi hao.
Wanafunzi hao wamejengewa uwezo kuhusu SHUWASA,mambo yanayosababisha ankara za maji kuwa kubwa,ubora wa maji yanayosambazwa na SHUWASA,namna ya kufanya malipo ya ankara za maji kwa njia ya simu na benki,namna ya kudhibiti uvujaji wa maji na jinsi ya kuwasiliana na SHUWASA.
Kambira Mtebe akiwaelezea wanafunzi wa shule ya sekondari Mwasele kuhusu huduma zinazotolewa na  Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Shinyanga (SHUWASA).
Kaimu Afisa Mawasiliano SHUWASA, Hadija Mabula ambaye pia ni Afisa huduma kwa wateja SHUWASA akielezea kuhusu mambo yanayosababisha ankara ya maji kuwa kubwa. Alitaja baadhi ya mambo hayo kuwa ni kufua nguo na kuosha vyombo kwenye bomba maji yakiendelea kutiririka,kusukutua meno na kuoga huku maji yakiendelea kutoka.
Kulia katikati ni Mwanafunzi wa shule ya sekondari akijibu swali kuhusu huduma za maji zinazotolewa na SHUWASA.
Wanafunzi wa shule ya sekondari Mwasele wakinyoosha mikono kujibu maswali yaliyoulizwa na maafisa kutoka SHUWASA.
Mwanafunzi akipokea zawadi ya madaftari na kalamu kutoka Kaimu Afisa Mawasiliano SHUWASA, Hadija Mabula ambaye pia ni Afisa huduma kwa wateja SHUWASA baada ya kujibu vizuri maswali aliyoulizwa kuhusu huduma za maji.
Kaimu Afisa Mawasiliano SHUWASA, Hadija Mabula ambaye pia ni Afisa huduma kwa wateja SHUWASA akitoa zawadi ya daftari na kalamu kwa mwanafunzi aliyejibu kwa usahihi swali kuhusu huduma za maji.
Wanafunzi wakinyoosha mikono baada ya kuulizwa "Nani anahitaji kupewa Mkataba wa huduma kwa mteja (SHUWASA)".
Kaimu Afisa Mawasiliano SHUWASA, Hadija Mabula ambaye pia ni Afisa huduma kwa wateja SHUWASA akigawa mikataba ya huduma kwa wateja.
Zoezi la kugawa mikataba ya huduma kwa wateja likiendelea.
Kambira Mtebe  akiendelea kugawa mikataba ya huduma kwa wateja.
Maafisa kutoka SHUWASA,Hadija Mabula na Kimbira Mtebe wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa serikali ya wanafunzi shule ya sekondari Mwasele.


Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog

No comments: