ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, May 31, 2018

Serikali Kuendelea Kuchukua Hatua za Kisera Kuhakikisha Riba za Mikopo Zinapungua

Waziri wa Madini Mhe. Angellah   Kairuki akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Fedha ya Wizara hiyo kwa mwaka 2018/2019 leo Bungeni  Jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge Uratibu  Kazi Vijana Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akitoa maelezo  Bungeni kuhusu hatua zitakazochukuliwa na Serikali katika kuwalinda watoto wa kike ambapo ameahidi kuwa Serikali itatoa taarifa rasmi kuhusu kuwepo kwa baadhi ya watu wanaowadhalilisha kijinsia watoto wa kike  na hatua zilizochukuliwa na Serikali.
Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akisisitiza kuhusu mikakati ya Serikali kupambana na Janga la Ukimwi hapa nchini ikiwemo kuhamasisha upimaji wa Virusi vya UKIMWI  hasa kwa wanaume kote nchini ili wajue hali zao na kuchukua hatua stahiki.
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Jenerali Venance Mabeyo (wakwanza kushoto) akifuatilia hotuba ya Waziri wa Madini Mhe Angellah Kairuki Bungeni Jijini Dodoma leo.
Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof. Idrissa Kikula aliyesimama (kushoto) na Mmoja wa Makamishna wa Tume hiyo Prof. Abdulkarim Mruma wakitambulishwa Bungeni leo mara baada ya kipindi cha maswali na majibu.
Sehemu ya Viongozi wa Tume ya Madini na wageni  mbalimbali wakiwemo wakuu wa Mikoa yenye madini wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Madini Bungeni Jijini Dodoma leo.
Sehemu ya Wanafunzi waliofika Bungeni kwa ziara ya mafunzo wakiwa ndani ya ukumbi wa Bunge wakati wa kipindi cha maswali na majibu. ( Picha zote na Frank Mvungi-  MAELEZO)
Na Lilian Lundo - MAELEZO, Dodoma.
Serikali imesema kuwa pamoja na huduma za bidhaa ya fedha kuamuliwa na nguvu ya soko kwa upande wake imekuwa ikichua hatua za kisera ili kuhakikisha kuwa riba za mikopo zinapungua katika soko hapa nchini.
Hayo yameelezwa leo Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Ashatu Kijaji alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Konde, Mhe. Khatibu Haji juu ya Serikali inachukua hatua gani ili benki ziweze kupunguza viwango hivyo vya riba?
"Baadhi ya hatua zilizochukuliwa na Serikali kupitia Benki Kuu ni pamoja na kuzitaka benki za biashara kutumia mfumo wa kuhifadhi na kutoa taarifa za wakopaji (Credit Reference Bureau System). Aidha, Benki hiyo imekuwa ikitoa mikopo ya muda mfupi kwa benki za biashara kwa kiwango cha asilimia 6.89," amesema Dkt. Kijaji.
Dkt. Kijaji amezitaja hatua nyingine zilizochukuliwa kuwa ni Benki Kuu kushusha riba (Discount Rate) kutoka asilimia 16.0 hadi asilimia 9.0 pamoja na kupunguza kiwango cha chini cha amana kinachotakiwa kuwekwa Benki Kuu na benki za biashara (Statutory Minimum Reserve Requirememnt (SMR)) kutoka asilimia 10.0 hadi asilimia 8.0.
Vile vile Serikali imeendelea kulipa malimbikizo ya madai yaliyohakikiwa kwa lengo la kupunguza kiwango cha mikopo chechefu na kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi.
Aidha, amesema baada ya hatua hizo za kisera kuchukuliwa na Serikali, baadhi ya benki za biashara hapa nchini zimeanza kupunguza riba za mikopo.
Ameongeza kuwa, Serikali itaendelea kuchukua hatua za kisera ili kuhakikisha kuwa riba za mikopo katika soko zinaendelea kupungua.

No comments: