ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, July 12, 2018

Machangudoa Watiwa Mbaroni Kwa Kuwauzia Ngono Wanafunzi

Jeshi  la Polisi mkoani Katavi limewakamata wanawake 14 wanaodaiwa kufanya biashara ya kuuza miili yao maarufu ‘madadapoa’ au  'Machangudoa', ambao inadaiwa wateja wao wakubwa wakiwa wanafunzi wa kiume wa sekondari.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Damas Nyanda, alisema watuhumiwa hao walikamatwa juzi usiku kufuatia msako uliofanyika katika Mtaa wa Majengo maarufu ‘Mtaa wa Fisi’ katika Mji wa Mpanda Manispaa ya Mpanda, huku akisisitiza msako huo ni endelevu.

Alibainisha kuwa msako huo ulifanyika katika madanguro matano na nyumba ya kulala wageni jirani na kituo cha mafuta cha Allyen katika Mji wa Mpanda.

Kamanda Nyanda alieleza kuwa madada hao kabla ya kupelekwa mahakamani, watachukuliwa alama za vidole vyao na kupigwa picha.

Alisema msako huo umefanywa kufuatia malalamiko ya wazazi kuwa wanafunzi wa kiume wa sekondari ni miongoni mwa wateja wa uhakika wa ‘madadapoa’ hao, huku wakionyesha wasiwasi wao wa uwezekano wa kupata maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU).

Taarifa za uhakika zinaeleza wengi wa ‘madadapoa’ hao wanatoka mikoa ya Tabora, Kigoma, Mbeya, Rukwa, Singida, Manyara, Arusha, Dodoma na mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Inadaiwa kuwa ‘dadapoa’ hao awali walikuwa wakifanya biashara hiyo ya kuuza miili yao katika machimbo ya madini ya dhahabu ya Isumamilolo mkoani Katavi, lakini baada ya dhahabu kupungua na biashara yao kudorora, waliamua kuvamia Mtaa wa Fisi na kuendelea na biashara ya kuuza miili yao.

Baadhi yao ambao wamenusurika kukamatwa wakati wa msako huo, walikiri kuwa wamepanga nyumba yote ambapo wanamlipa mmiliki nyumba Shilingi 6,000 kila siku kwa kila chumba, hivyo kwa mwezi kila chumba kinalipiwa Shilingi 180,000.

“Biashara ni nzuri inalipa sana kwani katika siku nzuri napata na kuwahudumia kingono wateja kati ya kumi hadi kumi na watano … wateja wetu wa kubwa ni wanafunzi wa sekondari na vijana wa kiume ambao wanachangamsha sana biashara,” alibainisha mmoja wao.

No comments: