ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, August 16, 2018

SONGWE KAMILISHENI UJENZI KWA WAKATI, NAIBU WAZIRI KWANDIKWA


 Mafundi wakiendelea na ujenzi wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Songwe inayojengwa na Wakala wa Majengo Nchini TBA mkoa wa Songwe.
 Naibu Waziri wa Ujenzi Mhe. Elias John Kwandikwa akisisitiza jambo kwa Kaimu Meneja wa Wakala wa Majengo nchini TBA mkoani Songwe msanifu majengo Christine Shayo, wakati wa ukaguzi wa shughuli za TBA mkoani Songwe .
 Naibu Waziri wa Ujenzi Mhe. Elias John Kwandikwa akisisitiza jambo kwa wataalam wa mkandarasi China Geo-Engineering Corporation anayejenga barabara ya Mpemba-Isongole kwa kiwango cha lami alipokagua barabara hiyo.
Mafundi wakiendelea na ujenzi wa daraja kubwa katika barabara ya Mpemba- Isongole KM 50.3 wilayani ileje, barabara hiyo inaunganisha nchi za Tanzania na Malawi.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhe. Elias John Kwandikwa amemtaka mkandarasi China Geo- Engineering Corporation aneayejenga barabara ya Mpemba-Isongole KM 50.3 kwa kiwango cha lami kuongeza kasi ya ujenzi ili barabara hiyo ikamilike  kwa muda uliopangwa.
Amemtaka mkandarasi huyo kuongeza vifaa, wafanyakazi ili ujenzi wake ugawanywe sehemu mbili na hivyo kuwezesha ujenzi huo kukamilika ifikapo  mwezi Agosti mwakani.
“Kutokana na umuhimu wa barabara hii kwa uchumi wa mkoa wa Songwe hakikisheni inakamilika ili kufungua uchumi wa Wilaya ya Ileje na mkoa wa Songwe kwa ujumla”, amesema Mhe, Kwandikwa.
Barabara hiyo ambayo inaunganisha Tanzania na Malawi kupitia mto Songwe itachochea huduma za uchukuzi na kurahisisha usafiri kwa wakazi wa wilaya ya Ileje mkoani Songwe.
Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), Mkoa wa Songwe mhandisi Yohana Kasaini amesema barabara hiyo inahusisha ujenzi wa madaraja makubwa manne, ya kati 14 na madogo 172, imesanifiwa kubeba magari ya aina zote na itagharimu zaidi ya shilingi bilioni 107 itakapokamilika.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri Kwandikwa amekagua ujenzi wa ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Songwe na hospitali ya Tunduma zinazojengwa na Wakala wa Majengo Nchini (TBA),mkoani Songwe na kumtaka kaimu meneja wa TBA mkoani humo msanifu majengo Christine Shayo kuhakikisha ujenzi huo licha ya kutoa fursa za ajira kwa wakazi wa maeneo hayo pia ukamilike kwa wakati na ubora uliokusudiwa.
Zaidi ya kilomita 3,856 za barabara nchini zitasanifiwa ili kujengwa kwa lami katika mwaka wa fedha 2018/2019.


No comments: