Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dk. Adelardus Kilangi akitoa maelezo ya muundo mpya ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na majukumu ya Ofisi hiyo kwa Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa wakati wa uzinduzi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wakili Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka. Uzinduzi wa Ofisi hizo tatu ulifanywa na Waziri Mkuu siku ya Jumatano jijini Dodoma ( picha na habari na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali)
SERIKALI KUIFANYIA MAREJEO MIKATABA MUHIMU YENYE MASLAHI NA TAIFA-AG
Na Mwandishi Maalum, Dodoma
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk. Adelardus Kilangi, amezikumbusha Wizara na Taasisi za Serikali ambazo bado hazijawasilisha mikataba ambayo imeombwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kwaajili ya marejejo kufanya hivyo mapema iwezekanavyo.
Ametoa wito huo siku ya jumatano wiki hii wakati wa hafla ya uzinduzi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka . Uzinduzi huo ulifanywa na Mhe. Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa Jijini Dodoma.
Akielezea Muundo mpya wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa Mhe. Waziri Mkuu na majukumu ambayo Ofisi hii imepanga kuyatekeleza. Mwanasheria Mkuu ameyataja baadhi hayo ni pamoja na marejeo ( review) ya mikataba muhimu kwa lengo la kuhakikisha mikataba hiyo ina masharti yanayolinda maslahi ya taifa.
“Tumepanga kufanya marejeo ya mikataba muhimu kwa lengo la kuhakikisha kuwa mikataba hiyo ina masharti yanayolinda maslahi ya taifa. Zoezi hili litahusisha mikataba yote ya kimataifa, mikataba ya uendelezaji madini ( MDAs) na mikataba ya uzalishaji na mauzo ya gesi asilia”, ameeleza Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Mikataba mingine itakayofanyiwa marejeo ni mikataba inayohusu uwekezaji baina ya Tanzania na nchi nyingine pamoja na mikataba mingine ambayo Serikali ina maslahi.
“Mhe. Waziri Mkuu, ninaomba kutumia fursa hii kuzishukuru Wizara na Taasisi za Serikali kwa kuendelea kutupatia mikataba tunayoihitaji kufanyia marejeo. Kwa Wizara na Taasisi ambazo hazijawasilisha mikataba iliyoombwa, zinakumbushwa kufanya hivyo mapema ili shughuli hiyo ianze”.
Pamoja na kufanya marejeo ya mikataba muhimu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema, Ofisi yake inapanga kuweka mfumo utakaokuwa na regista ya mikataba yote ya kimataifa ili iwe rahisi kuifanyia rejea au kupatikana pindi inapohitajika kwa matumizi mbalimbali ya kiserikali na kisheria.
Vilevile Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Kilangi ameeleza kwamba, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu pia imejipanga kuwa na mkakati wa kutumia maendeleo ya teknolijia ya mawasiliano katika utekelezaji wa majukumu yake ya utoaji wa huduma za kisheria kwa Serikali na Taasisi za Serikali na Wananchi.
Kwa mujibu wa Mwanasheria Mkuu, mkakati huo utahusisha kuweka kanzi data ya Mawakili wa Serikali walioajiriwa katika utumishi wa umma ili kuwezesha kuwasimamia na kuratibu shughuli zao ipasavyo.
Aidha mkakati huo wa matumizi ya teknolojia za kisasa za mawasiliano pia utahusu uanzishwaji wa kanzi data ya mikataba ya kitaifa na kimataifa ambayo imeingiwa na Serikali za mitaa na Taasisi za Serikali, kanzi data ya sheria zilizofanyiwa marejeo na kutafsriwa, kanzi data ya huduma za maktaba na masjala ya sheria na kanzi data ya kesi ambazo Serikali ni mdaawa.
Mwezi February mwaka huu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , kwa mamlaka aliyonayo chini ya Ibara ya 36 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977, alitoa “Amri ya Maboresho ya Muundo wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu” kupitia Tangazo la Serikali Na 48 la mwaka 2018 kwa lengo la kuboresha huduma za kisheria katika sekta ya Umma.
Amri hiyo ya Maboresho ilitambua kuwepo kwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali yenye wajibu wa kutoa ushauri wa kisheria kwa Serikali Kuu, Mamlala za Serikali za Mitaa, Idara za Serikali na Mashirika ya Umma, kuandaa Miswaada ya Sheria; kuandaa nyaraka mbalimbali za kisheria na rasimu za maazimio ya Bunge pamoja na majukumu mengine.
Amri hiyo ya Maboresho pia ilitambua kuanzishwa kwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka yote ya jinai mahakamani; na kutambua kuanzishwa kwa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali inayosimamia na kuendesha mashauri yote ya madai.
Imetolewa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Dodoma
No comments:
Post a Comment