Balozi Ombeni Sefue akimkabidhi Mkuu wa Taasisi ya Stadi za Masuala ya Afrika, Profesa Ajay Dubey zawadi ya Kinyago.
Chuo cha Diplomasia Tanzania (Center for Foreign Relation -CFR) wamefanya ziara ya kikazi nchini India kuanzia tarehe 13-15 Agosti 2018. Ziara hiyo imekuja kufuatia mwaliko wa Taasisi ya Mafunzo ya Kidiplomasia ya India (Foreign Service Institute-FSI), na ililenga kujua shughuli za FSI na taasisi zinazoshirikiana nazo, pamoja na kujadiliana juu ya uwezekano wa kuingia katika makubaliano ya ushirikiano.
Wajumbe wa CFR waliongozwa na Balozi Ombeni Sefue, Katibu Mkuu Kiongozi (Mst.), ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya CFR. Wajumbe wengine walikuwa ni pamoja na Kaimu Mkuu wa cha Diplomasia (CFR), Dr Bernard Achiula, Dr Lucy Shule wa CFR, Dr Richard Mbunda kutoka UDSM, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia (DAA), Bibi Justa Nyange. Kutoka ubalozi wa Tanzania nchini India, alikuwepo Balozi Baraka Luvanda na Bibi Natihaika Msuya, Afisa Mambo ya Nje.
Aidha, wajumbe hao walipata fursa ya kutoa mihadhara katika Kituo cha Stadi za Masuala ya Afrika katika Chuo Kikuu cha Nehru, Taasisi ya Stadi za Masuala ya Ulinzi na Usalama (IDSA) pamoja na Taasisi ya Tafiti Mahususi kuhusu ushirikiano baina ya Nchi za Kusini (South Cooperation Research Information System-RIS).
Kwa ujumla, ziara hiyo imekuwa ya mafanikio makubwa ambapo taasisi wenyeji zimeonesha dhamira ya dhati ya kushirikiana na CFR katika kujenga uwezo wa wanadiplomasia wa Tanzania.
No comments:
Post a Comment