Akilisimulia Ijumaa Wikienda mkasa mzima akiwa nyumbani kwake hapo, Elias alisema kidonda hicho kikubwa kilichopo mguuni kwake kilianza kama kipele au lengelenge kwenye mguu wake wa kulia huku kikitoa maji yenye harufu kali kiasi ambacho hawezi kukaa na mtu karibu.
Akiendelea kusimulia, mgonjwa huyo alisema baada ya kuona hivyo alienda moja kwa moja hadi Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambapo alianzia kupata matibabu, lakini kila alipokuwa akitumia dawa, kidonda cha mguu huo ndiyo kilikuwa kikiendelea kukua na kuwa kikubwa.
“Unajua kuna wakati mwingine nilikuwa naungalia mguu wangu nikawa sielewi kabisa maana kidonda kilizidi kukua, nikaanza kushindwa hata kutembea au kusogeza mguu hata hatua moja, ndipo nilipolazwa tena Muhimbili,” alisema mgonjwa huyo.
Akiendelea kusimulia alisema baadhi ya madaktari baada ya kuuona mguu huo ulivyo wakamuandikia kwamba ukatwe na wakawaambia manesi kuwa asisafishwe kidonda kwani kesho yake atapelekwa kukatwa mguu huo maana hawezi kupona.
“Yaani wakati wanajiandaa wanipeleke chumba cha operesheni kwa ajili ya kukatwa mguu wangu, alipita profesa mmoja, akauchunguza, akaamua kunisafisha mwenyewe na akagundua kuwa kidonda bado kilikuwa kibichi kabisa na pia vidole vyangu vinaweza kujikunja na kukunjuka hivyo akaamuru usikatwe,” alisema.
Aliongeza kuwa, baada ya hapo aliendelea kufanyishwa mazoezi na kusafishwa akatoka, lakini baada ya muda akiwa nyumbani mguu ukaanza kutoa funza na harufu kali. “Mbaya zaidi usiku panya alikuwa akija na kukitafuna kidonda, nikishtuka anakimbia na kuacha kidonda kikivuja damu nyingi. Sielewi huyu panya kila siku saa tisa usiku alikuwa anatokea wapi,” alisema mzee huyo huku akitokwa machozi.
Aliongeza kuwa, kinachomuuma ni kwamba japo anaumwa, lakini anakumbana na hali ngumu kimaisha maana kuna wakati anaomba mpaka shilingi 100 huku watoto wake wengine wakiwa nyumbani wakikosa ada ya kwenda shuleni kwa kuwa na maisha duni kwani hata kula kwao ni tabu. “Maisha yetu ni magumu mno kuna wakati nawaza mpaka presha inakuwa juu sana nakimbizwa hospitalini,” alisema mzee huyo ambaye enzi hizo alikuwa na jina mjini.
Kwa yeyote aliyeguswa na habari hii anaweza kuwasiliana na mgonjwa huyu kwa kumtumia chochote kupitia namba yake ya simu 0715 880 195 au 0755 880 195- Mhariri.
STORI: Imelda Mtema, DAR GPL
No comments:
Post a Comment