ANGALIA LIVE NEWS

Friday, September 14, 2018

DKT. KIJAJI: UWEKEZAJI WA MSHAHARA NI JUKUMU LA MFANYAKAZI



Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb)

Na. WFM
Serikali imeeleza kuwa uwekezaji wa mishahara kwa wafanyakazi nchini ni jukumu la mfanyakazi mwenyewe kwa kuwa mshahara ni mali ya mfanyakazi hivyo anaweza kuutumia kwa kuwekeza au kuto kuwekeza.

Hayo yameelezwa Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, alipokuwa akijibu maswali ya Mbunge wa Viti maalum Mhe. Mwantum Dau Haji, aliyetaka kujua Serikali inasema nini kuhusu uwekezaji wa mishahara kwa watumishi wa umma na kuwepo kwa ucheleweshaji wa mishahara kwa Watumishi wa Umma..

Dkt. Kijaji alieleza kuwa Serikali kwa upande wake inawalipa mishahara wafanyakazi wake kwa wakati kwa kuzingatia waraka wa Hazina namba 12 wa mwaka 2004 ambao unaitaka Serikali kulipa mishahara kabla ya tarehe 25 ya kila mwezi.

“Kumbukumbu za malipo ya mishahara kwa watumishi wa umma zinaonesha kuwa, kuanzia Julai 2017 hadi Agosti 2018, watumishi walilipwa mishahara yao kati ya tarehe 20 na 24 ya kila mwezi hivyo napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu na umma kwa ujumla kuwa hakuna ucheleweshaji wa malipo ya mishahara kwa watumishi wa umma” alieleza Dkt. Kijaji.

Aidha Serikali imekuwa ikiwatendea haki wafanyakazi wake katika upandishaji wa madaraja na kila mwaka wafanyakazi hupandishwa madaraja.

No comments: