Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilipokea Rufaa moja (1) kutoka kwa mgombea Udiwani wa Kata ya Kibutuka katika Halmashauri ya Wilaya Liwale, Tume imefanya hivyo kwa kuzingatia Kifungu cha 44(5) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa kikisomwa pamoja na Kanuni ya 28(1) ya Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (Uchaguzi wa Madiwani) za mwaka 2015.
Rufaa hiyo iliwasilishwa na mgombea Udiwani kutoka Chama cha Wananchi CUF, Ndugu Mdohoma Bashiru Ismaili akitaka arejeshwe kuwa mgombea udiwani katika Kata ya Kibutuka kupitia chama hicho.
Kuenguliwa kwake kulitokana na kuwekewa pingamizi na mgombea mwenzake kwa madai kuwa majina yake katika fomu ya uteuzi yalitofautiana na Msimamizi wa uchaguzi kukubaliana na pingamizi hilo na hivyo kumuengua.
Tume katika kikao chake cha tarehe 30 Septemba 2018, imekubaliana na maelezo ya mrufani na kuelekeza arejeshwe kuendelea kuwa mgombea Udiwani katika Kata ya Kibutuka, Halmashauri ya wilaya ya Liwale kwa kuwa imejiridhisha kwamba mrufani wakati wa kujaza fomu yake ya uteuzi Na. 8C alianza na jina la mwisho likifuatiwa na majina mengine kwa kuwa ndilo alilotaka lianze kuandikwa kwenye karatasi ya kupigia kura.
Kwa mujibu wa Maelekezo ya Tume kuhusu ujazaji wa fomu Na. 8 C ya Uteuzi katika kipengele namba (2) yanatoa uhuru kwa mgombea kuanza na jina ambalo angetaka liandikwe kwa herufi kubwa kwenye karatasi ya kupigia kura.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi inavikumbusha Vyama vya Siasa na Wagombea wanaoshiriki uchaguzi mdogo wa Ubunge katika jimbo la Liwale na Udiwani katika Kata mbalimbali za Tanzania Bara, utakaofanyika tarehe 13 Oktoba 2018 kuzingatia Sheria na Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya Mwaka 2015, wakati wote wa kampeni na hata Siku ya Uchaguzi.
Imetolewa leo tarehe 30 Septemba ,2018
Hamis Mkunga
KAIMU MKURUGENZI WA UCHAGUZI
No comments:
Post a Comment