Dar es Salaam. Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC), Mizengo Pinda amewataka wananchi wa jimbo la Ukonga kumchagua Mwita Waitara ili aunganishe nguvu za kuleta maendeleo zilizojazana ndani ya Serikali.
Pinda ambaye ni waziri mkuu mstaafu wa awamu ya nne, amesema hayo wakati wa uzinduzi wa kampeni za CCM katika jimbo la Ukonga leo Jumamosi Septemba Mosi, 2018.
Amesema Waitara alipokuwa upinzani haikuwa rahisi kwake kuonana viongozi wa Serikali, lakini kwa kuwa yuko CCM amepata marafiki wengi watakaomsaidia kutatua kero za wananchi wa Ukonga.
Pinda ambaye aliteuliwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais John Magufuli kuwa mjumbe wa NEC aliwaeleza wananchi wa Ukonga kuwa mkandarasi wa ujenzi wa daraja la Kitunda suala lake limeanza kufanyiwa kazi na yeye (Pinda) atakuwa ‘mpambe’ wa kuhakikisha suala hilo linafanikiwa.
Amewaeleza wananchi kuwa Waitara ni muhimu kwao kwa kuwa sasa anaungwa mkono na viongozi wa wilaya, mkoa na Taifa, hivyo matatizo ya wananchi yatashughulikiwa kwa haraka.
"Upo bungeni unasimama kumnanga waziri mkuu kisha unamfuata pembeni unamuomba mradi wa maji atakuambia analifanyia kazi, kumbe kakuacha na yeye ni binadamu anataka heshima,” amesema Pinda.
Amewataka wananchi wawaeleze wapinzani kuwa tabia yao ya matusi na kelele za unafiki itawafanya wasubiri sana na watapata tabu sana.
Pinda amewataka mabalozi wa nyumba 10 waheshimiwe kwa sababu wao ndiyo wameshika mizizi ya chama.
"Mabalozi tembeeni nyumba kwa nyumba kuhakikisha mnamtafutia kura Waitara," amesisitiza Pinda.
Mjumbe mwingine wa NEC, Makongoro Nyerere akimnadi mgombea wa CCM, amesema yeye na Pinda walikuwa ‘benchi’ lakini Rais Magufuli akawateua kuwa wajumbe wa NEC.
Amesema yeye pia alikuwa upinzani ambako alisota kwa miaka saba bila kuteuliwa hata ukatibu kata. Makongoro alikuwa mwanachama wa NCCR-Mageuzi.
Amesema aliamua kurudi CCM na aliweza kupata nafasi za uongozi ikiwamo mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara.
“Waitara amerudi hivi karibuni ana mapovu anataka kuyatoa mimi naona huruma nilikuwa nao wale,” amesema.
Amesema mambo yaliyokuwa yakimkera alipokuwa upinzani ni hoja zisizo kwisha za ufisadi, rushwa na upendeleo.
Makongoro ambaye ni mtoto wa Mwalimu Julius Nyerere amesema mafisadi na wala rushwa walikuwapo CCM lakini walishughulikiwa na vyombo husika.
No comments:
Post a Comment