ANGALIA LIVE NEWS

Friday, September 7, 2018

Serikali Kuongeza Fedha Katika Mradi Wa Tasaf Ili Ziwafikie Walengwa Wote

SERIKALI imesema ina mpango wa kuongeza fedha katika Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini (TASAF) ili kuongeza idadi ya wananchi watakazonufaika na mradi huo.

Hayo yamesemwa leo tarehe 7 Septemba, 2018 jijini Dodoma katika kipindi cha maswali na majibu, na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Nkuchika.

Waziri Nkuchika ameeleza kuwa, malengo ya TASAF ni kufikia walengwa wote na kwamba hadi sasa asilimia 70 ya walengwa wamefikiwa na mradi huo, hivyo serikali imedhamiria kuongeza fedha.

“Malengo ya TASAF ni kufikia walengwa wote wanaokubali kusaidiwa, mpaka sasa tumefikia walengwa asilimia 70. TASAF kwenye awamu ya tatu B, malengo ya serikali ni kufikia walengwa wote na ili tuwafikie walengwa wote lazima serikali iongeze fedha,” amesema.

Aidha, Waziri Nkuchika ameahidi kufanyia kazi changamoto zinazoikabili mradi huo ikiwemo malalamiko ya upendeleo katika utolewaji wa fedha hizo.

“…Nakubali rai yake yale maeneo yenye malalamiko nitayafanyia kazi, naomba mbunge yoyote mwenye ushahidi kwamba mahali fulani hizi fedha zina upendeleo nitalifanyia kazi. Kwa kuwa TASAF inafanya kazi nzuri hapa nchini, na kufanya kazi maeneo mengi, upande wa afya elimu, sasa hivi inasimamia elimu bure kwa watoto wa masikini, lakini mwenyekiti nasema hivi TASAF haibagui chama, TASAF iko tayari kuwaongezea fedha ili ihudumie watu wengi.” Amesema Waziri Nkuchika.

Mradi wa TASAF ulianza rasmi mwaka 2013 na unatarajiwa kumalizika mwaka 2023 ambapo unatekelezwa katika kipindi cha miaka kumi mfululizo ambapo vimegawanyika kwa awamu mbili. Fedha za utekelezaji wa mradi huo ni za mkopo kutoka Benki ya Dunia (WB)

No comments: