ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, September 6, 2018

Serikali Kutoa Dawa ya Kinga Kwa Ambao Bado Hawajaambukizwa Virusi Vya UKIMWI

Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, imesema ipo katika mpango wa kuwapa dawa za ugonjwa wa UKIMWI watu wasioathirika kwa lengo la kuwazuia na ugonjwa huo pindi watakapokuwa wamekutana kimwili na wahanga wa tatizo hilo.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa wizara hiyo Dkt. Faustine Ndugulile, leo Septemba 06, 2018 Bungeni Jijini Dodoma kwenye kikao cha 03 mkutano wa 12 wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge, Hawa Mchafu, aliyetaka kufahamu hali ya Tanzania juu ya kutumia dawa za UKIMWI kwa lengo la kuzuia maambukizi ya ugonjwa huo endapo atajamiana na mtu mwenye maambukizi.

"Sayansi katika matibabu ya ugonjwa wa UKIMWI yameonyesha kwamba mtu asiyekuwa na maambukuzi ya UKIMWI anaweza akapatiwa dawa ambazo zinaweza kumsaidia kumkinga dhidi ya ugonjwa wa ukimwi. Lakini naomba kuweka msisitizo kuwa hadi hivi sasa hatuna tiba ya ugonjwa wa UKIMWI bali tunachokifanya hichi ni dawa kinga na sisi kama Tanzania tunalijua hilo na tumeshaanza ngazi ya majaribio", amesema Dkt. Faustine na kuongeza;

"Baada ya majaribio haya tutaitawanya nchi nzima na tunalenga makundi mahsusi ambayo ni pamoja na wanaofanya biashara ya ukahaba, wanaojidunga dawa za kulevya , lakini kinga hii inaendana sambamba na kutumia njia nyingine za kujikinga kwa kuwa hiyo  sio suluhu ya kutopata maambukizi ya UKIMWI".

Kwa upande mwingine, Dkt. Faustine Ndugulile amesema serikali imeanza kutumia mifumo mipya ya kuwafuatilia waathirika wa ugonjwa wa UKIMWI unaoitwa 'Biometric', kwa lengo la kuwasaidia kupata matibabu popote watakapo kuwepo kwa lengo la kuwatoa katika njia ya kukatisha utumiaji wa dawa za ugonjwa huo.

No comments: