ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, September 18, 2018

WAZIRI KAMWELWE: SINA IMANI NA MHANDISI MSHAURI

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, akitoa maelekezo kwa Mhandisi Mshauri kutoka Kampuni ya LEA International Bw. Sanjeev Gupta (kushoto) anayesimamia ujenzi wa barabara ya Usesula-Komanga yenye urefu wa KM 108 kwa kiwango cha lami, wakati akikagua hatua za ujenzi wa barabara hiyo na kutoridhishwa na madaraja na makalvati yaliyotengenezwa katika mradi huo, mkoani Tabora.
Fundi Mchundo Bw. Fadhili Amiri, akitoa ufafanuzi kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, (wa pili kushoto) kuhusu kazi anazozifanya  wakati alipokuwa akikagua hatua za ujenzi wa barabara ya Usesula-Komanga yenye urefu wa KM 108 kwa kiwango cha lami, mkoani Tabora.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, akikagua mchanga unaotumika kutengenezea madaraja na makalvati katika ujenzi wa barabara ya Usesula-Komanga yenye urefu wa KM 108 kwa kiwango cha lami, na kutoridhishwa na ubora wake, mkoani Tabora.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, akizungumza na Mhandisi Mshauri kutoka Kampuni ya LEA International Bw. Sanjeev Gupta anayesimamia ujenzi wa barabara ya Usesula-Komanga yenye urefu wa KM 108 kwa kiwango cha lami, wakati akikagua kokoto zitakazotumika katika mradi huo na kutoridhishwa nazo, mkoani Tabora.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, (wa kwanza) akisisitiza jambo kwa Mkandarasi wa Kampuni ya SAMOTA Bw. Abdallah Salim, kuhusu kukamilisha mradi huo kwa wakati, mara baada ya kukagua hatua za maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Urambo-Kaliua yenye urefu wa KM 28, Mkoani Tabora.
Muonekano wa sehemu ya  barabara ya Usesula-Komanga yenye urefu KM 108 inayojengwa kwa kiwango cha lami, mkoani Tabora. Mradi wa ujenzi huo utakamilika mwezi Machi mwaka 2021.
Muonekano wa sehemu ya barabara ya Tabora-Sikonge yenye urefu wa KM 30, inayojengwa kwa kiwango cha lami. Ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 90 mpaka sasa.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe ameuagiza Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Tabora kujiridhisha kwa kuyapima tena madaraja na makalvati yaliyoanza kutengenezwa kwenye ujenzi wa barabara ya Usesula-Komanga yenye urefu wa KM 108 kama yanakidhi ubora na viwango kwa kuwa mchanga uliotumika haufai.

Waziri Mhandisi Kamwelwe amesema kuwa hata eneo ambalo mkandarasi anasaga mawe kuna vumbi jingi kulinganisha na kokoto zinazozalishwa hii kitaalamu ina maanisha kwamba mwamba huo wa mawe ni dhaifu.

Ameyasema hayo katika kijiji  cha Ipole wilayani Sikonge wakati akikagua ujenzi wa barabara hiyo na kusema kuwa hana imani na mhandisi mshauri kutoka kampuni ya LEA International Ltd katika usimamizi wa mradi huu.

"Sijaridhishwa na madaraja na makalvati haya Mhandisi wa Mkoa kushirikiana na Mhandisi Mshauri na Mkandarasi mkayapime tena ubora kwenye Maabara ya Taifa na kama hayafai muyaondoe maramoja na kutengeneza mengine",amesema Waziri Mhandisi Kamwelwe

Amesisitiza kuwa fedha za kujengea barabara hiyo zimefedhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika  (AfDB) na tutalazimika kuzilipa hivyo ni lazima thamani ya fedha inaonekana katika mradi huu.

Ameongeza kuwa ujenzi wa barabara hiyo utaongeza tija ya maendeleo kwa wananchi katika mikoa hiyo kwani tokea tupate uhuru hawajawahi kuona lami na utafungua mkoa huu na ule wa Katavi.

Naye Afisa Mwajiri na Mahusiano kutoka kampuni ya Mkandarasi M/S Jiangxi Geo-Engineering Corporation Bw. Fidelis Masanja wametoa nafasi 20 kwa vijana kutoka kila kijiji unakopita mradi huo na hivyo kutoa rai kwa vijana kuchangamkia fursa hizo. 

Bw. Masanja amefafanua kuwa wameamua kutumia viongozi wa serikali za vitongoji na vijiji wakiamini kuwa watapata vijana waadilifu na waaminifu katika mradi huo.

Kabla ya kukagua barabara hiyo Waziri huyo alikagua ujenzi wa barabara ya Urambo-Kaliua yenye urefu wa KM 28 inayojengwa na mkandarasi mzawa wa kampuni ya SAMOTA na kumtaka kukamilisha barabara kwa muda uliopangwa.

Waziri Kamwelwe amesema hayupo tayari kutumbuliwa kwa kushindwa kumsimamia mkandarasi huyo na badala yake ataondoka yeye.

Kwa upande wake Meneja wa TANROADS Mhandisi Damian Ndabalinze, amemuahidi  Waziri huyo kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa na Waziri na kuwafatilia kwa karibu makandarasi hao katika miradi yote.

No comments: