Morogoro. Marita Malambi (25), mwanamke aliyenusurika kuliwa na mamba amepokea msaada wa Sh349,400 fedha zilizochangwa na wasomaji wa gazeti la Mwananchi ili kumwezesha kimaisha.
Marita alinusurika kuuawa na mamba wakati akiteka maji kwenye Mto Mgeta uliopo Dakawa mkoani Morogoro, Februari 17.
Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu kuhusu maisha yake ya sasa, Marita alishukuru kupata msaada huo wa fedha na kuahidi kuzizalisha kwa kufanya biashara ili imsadie kiuchumi na familia yake.
“Nashukuru sana gazeti la Mwananchi na wasomaji kwa ujumla, Mungu awabariki kutokana na matatizo ambayo nilikuwa nimeyapata nisingeweza kufanya kitu chochote, lakini nashukuru Mungu leo nimepata fedha hizi nitaweza kufanya mradi ili uniwezeshe kuinua maisha yangu,” alisema Marita.
Soma Zaidi: Simulizi ya mwanamke aliyepambana na mamba-1
Alisema kwa hali aliyonayo sasa ni ngumu kuliko ilivyokuwa mwanzo, kwa kuwa hawezi tena kufanya vibarua kama ilivyokuwa awali na hata shughuli za mtoni ikiwemo kilimo cha mbogamboga amesimama kuzifanya kwa kuhofia maisha yake.
“Kutokana na hali yangu ya mguu siwezi kufanya chochote, Mungu awabariki mmeweza kunisaidia na kunikomboa katika maisha yangu, kwa sasa nipo na wazazi wangu sina pa kwenda, wao ndiyo wanaonitafutia chochote kitu, endeleeni kuwa na moyo huohuo,” alisema.
Emma Lolensi ambaye ni mama wa Marita alisema hawakutegemea kupata msaada huo kwani yeye na mumewe wamekuwa wakifanya vibarua ili kupata chakula na hawana mashamba yanayozalisha.
Marita alishambuliwa na mamba, tukio lililosababisha kupoteza mtoto wake wa kiume, Godfrey David (mwaka mmoja na miezi miwili), ambaye alikufa na baadaye mwili wake kusombwa na maji.
Katika tukio hilo, baada ya kupambana na mamba kwa muda, Marita alifanikiwa kuokolewa na vijana waliokuwa karibu na mto huo na kupelekwa Kituo cha Afya Dutumi kabla ya kupelekwa Hospitali ya Rufaa Morogoro ambako alihudumiwa kwa siku tano kisha kupewa rufaa kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Alitibiwa katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) akianza na matibabu kabla ya kufanyiwa upasuaji mkubwa wa mfupa mrefu wa paja kwa kuwekewa chuma maalumu ndani ya mfupa.
Kabla ya upasuaji huo, madaktari walifanya jitihada ya kusafisha vidonda pamoja na kumpatia dawa za kuzuia maambukizi ili kuondoa bakteria na kumwepusha na madhara mengine.
Athari za vidonda
Vidonda vinavyosababishwa na mamba visipotibiwa kwa umakini huleta maambukizi ambayo husababisha mishipa ya damu, mfupa, misuli na mishipa ya fahamu kuharibika na hivyo kulazimu kiungo husika kuondolewa mwilini.
Soma: Simulizi ya mwanamke aliyepambana na mamba – 3
No comments:
Post a Comment