KWAKO msanii wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ habari za siku? Mambo yanasemaje mzee baba? Binafsi mimi ni mzima wa afya, hofu kwako wewe ambaye kila wakati najua unakuwa nje ya nchi kutuwakilisha kimuziki.
Kwanza nikupongeze kwa kutuwakilisha vizuri, sisi kama vijana wa Kitanzania tunajivunia wewe kufanya shoo nyingi nje ya nchi, kuwashirikisha wasanii wakubwa wa kimataifa wakiwemo Wamarekani. Hakika wewe ni kioo halisi cha Tanzania katika upande wa Bongo Fleva.
Leo nimekukumbuka kwa barua maana unastahili kuandikiwa barua nzito, hapa huwa tunakosoa na pia huwa tunapongeza pale inapobidi. Leo nataka nikupongeze, kupitia ulichokifanya kwa msanii Hawa, ni tendo jema ambalo hakika unastahili pongezi.
Kitendo cha kumsafirisha binti yule hadi India na kufanyiwa matibabu ya moyo, kimedhihirisha wazi kwamba wewe una moyo wa kujitoa. Unaguswa na matatizo ya wengine maana kwa kawaida wanadamu wengi huwa tunaguswa zaidi na matatizo yetu, ya wenzetu huwa tunaona kama hayatuhusu.
Wewe ulimuona Hawa anateseka, fedha zilizokuwa zinahitajika kwa ajili ya safari na matibabu ni nyingi na nina hakika familia yake pekee isingeweza kumsafirisha lakini mara baada ya kupata taarifa ukasema hapana, lazima umsaidie.
Kupitia watu wako wa karibu, mliratibu safari hiyo na hatimaye Hawa na mama yake mzazi Ndagina Hassan wakasafiri hadi India na Mungu akawasimamia matibabu yakaenda vizuri na muda wowote kutoka sasa Hawa anaweza kurejea nchini akiwa na ahueni kubwa baada ya kupata matibabu.
Najua si kwamba wewe una fedha nyingi sana lakini uliguswa, ukaona umsaidie hivyo hilo ni somo kubwa kwetu. Ni somo kubwa kwa mastaa wengine kwani hata vitabu mbalimbali vya dini vinatufundisha kwamba unapotoa unapata baraka zaidi.
Ndugu zangu tujifunze kutoa, tutoe vikubwa ili Mungu atupe baraka kubwakubwa. Sadaka njema ni ile inayokugusa na si kutoa ile unayoona ni ziada. Leo Diamond ameonesha njia, wasanii wengine muige mfano huu.
Siyo lazima utoe kikubwa sana, toa kile ambacho Mungu amekujaalia.
Bahati nzuri sana Mungu anatujua sisi mpaka kwenye roho zetu hivyo tutoe kwa ukarimu. Usitoe kwa kunung’unika.
Toa kwa upendo huku ukijua kwamba vyote tulivyonavyo ni mali yake hivyo usiwe mchoyo, usimuibie Mungu maana anakuona muda wote. Anawaona jinsi mnavyoteketeza fedha nyingi kwenye anasa za kidunia, kula bata na kumsahau Muumba wetu.
Ndugu zangu tujifunze kupitia Diamond, tuwe na moyo wa kutoa, kusaidia jamii mbalimbali zenye uhitaji. Watu wenye matatizo kama haya ya Hawa wapo wengi, kuna watoto yatima, kuna makundi mengi tu yanayohitaji msaada.
Kuna wagonjwa kama hivyo, sisi ambao leo ni wazima wa afya na Mungu ametupa pumzi basi yatupasa kumshukuru na kusema asante, yatupasa kutoa shukrani kwa kuwasaidia wengine na Mungu atatubariki.
Tupunguze starehe, haya mambo yapo tu, tufanye ibada kwani maisha yetu hapa duniani ni mafupi.
Nirudie kukupongeza Diamond kwa ulichofanya na uendelee hivyo kwani nilifurahi pia kuona kwamba unataka kumwezesha mtaji wa biashara Hawa pindi atakaporejea, ni upendo wa kipekee kwa kweli Mungu akubariki sana. Jamani shime tufuate nyayo zake.
Mungu ibariki Tanzania, bariki muziki wa Bongo Fleva na mbariki Diamond, Amen.
Mimi ni ndugu yenu;
Anko Nangale. GPL
No comments:
Post a Comment