ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, November 22, 2018

Kinachowatokea Yanga Shinyanga ni mpango

By Doris Maliyaga, Mwanaspoti

Dar es Salaam. Baada ya mapumziko ya Ligi Kuu Bara kupisha mechi za mashindano ya timu za Taifa, ligi hiyo itandelea kwa Alhamisi kwa michezo miwili itakayopigwa Uwanja wa Kambarage Shinyanga na Azam Complex.

Katika michezo hiyo miwili, Yanga watacheza ugenini na Mwadui FC wakati Azam FC itawakaribisha Wazee wa Kupapasa Ruvu Shooting.

Huko Shinyanga ndiyo kuna kazi kubwa unaambiwa na macho pamoja na masikio ya wadau wa soka yatakuwa huko kuanzia saa 10:00, jioni mechi hiyo itakapokuwa inachezwa.

Yanga wao walisafiri na ndege kwa mafungu kwenda huko na huo utakuwa mchezo wao wa kwanza kukipiga nje ya Dar es Salaam baada ya kucheza 10, nyumbani kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Lakini, katika safari hiyo wamewakosa wachezaji wao wawili tegemeo kipa Beno Kakolanya na beki, Kelvin Yondani 'Vidic' ambao wamebaki Dar es Salaam kwa kile kinachodaiwa kuwa ni matatizo ya kifamilia.

Kutokana na hali hiyo, iko wazi kuwa kipa Mkongo Klause Kindoki ambaye hakuanza vizuri Yanga kutokana na kuruhusu mabao mengi ya kufungwa katika mechi alizocheza na beki Abdallah Shaibu 'Ninja' akamsaidia Andrew Vincent 'Dante' kwenye beki ya kati.

Kocha Mwinyi Zahera amesema, hana wasiwasi na kikosi chake licha ya kuwakosa Kakolanya na Yondani kwa sababu ana wachezaji wengi.

Mchezo mwingine mkali utakaopigwa Azam Complex kuanzia saa 1:00, jioni wenyeji Azam FC watakuwa na kazi ya kulinda heshima yao na kuendelea kung'ara kileleni mwa ligi kwa maafande hao wa Ruvu Shooting.

Katika kujiweka sawa na mchezo huo, Azam ilikuwa inafanya mazoezi asubuhi na usiku ili kwenda sawa na hali halisi ya mchezo huo.

No comments: