Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Lawrence Museru akizungumza na Balozi wa Cuba nchini Tanzania, Mhe. Lucas Domingo Hernandez Polledo pamoja na Naibu Waziri wa Kilimo wa Cuba, Mhe. Miquel Rodriquez de Armas wakati walipoitembelea hospitali hiyo kuona huduma mbalimbali za matibabu zinazotolewa na wataalam wa nchi hiyo kwa kushirikiana na wataalam wa Muhimbili. Kulia ni Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa Muhimbili, Makwaia Makani, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji, Dkt. Sufiani Baruani, Afisa wa Wizara ya Mambo ya Nje, Mohamed Kamal Mohamed, Kaimu Mkurungezi wa Huduma za Uuguzi Muhimbili, Sista Zuhura Mawona na Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Tiba, Dkt. John Rwegasha.
Kutoka kulia ni Naibu Waziri wa Kilimo wa Cuba, Mh. Miquel Rodriquez de Armas, Afisa katika Ubalozi wa Cuba nchini Tanzania, Sultan Hamud Said, Balozi wa Cuba nchini Tanzania, Mhe. Lucas Domingo Hernandez Polledo na wengine ni ujumbe wa Naibu Waziri huyo kwa pamoja wakimsikiliza Prof. Museru.
Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi Muhimbili, Sista Zuhura Mawona, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji, Dkt. Sufiani Baruani na Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Tiba, Dkt. John Rwegasha wakiongoza ujumbe huo kutembelea maeneo mbalimbali katika hospitali hiyo.
Balozi wa Cuba nchini Tanzania, Mhe. Lucas Domingo Hernandez Polledo akizungumza na baadhi ya wataalam wa Cuba, huku akiwataka kuongeza bidii zaidi ili kutoa huduma bora za kibingwa katika hospitali hiyo. Wengine ni wataalam wa afya wa MNH.
Daktari Bingwa wa Mapafu na Wagonjwa Mahututi, Dkt. Paulina Chale wa Muhimbili akizungumza na Balozi Lucas Domingo Hernandez Polledo (wa nne kulia) wakati alipotembelea wodi ya wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum. Wengine ni baadhi ya wataalam wa Muhimbili na Cuba.
Naibu Waziri wa Kilimo wa Cuba, Mhe. Miquel Rodriquez de Armas akisisitiza jambo wakati akizungumza na wataalam kutoka Cuba ambao wanashirikiana na wataalam wa Muhimbili kutoa huduma za matibabu katika hospitali hiyo. Kushoto ni Balozi wa Cuba nchini Tanzania, Mhe. Lucas Domingo Hernandez Polledo na kulia ni Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa Muhimbili, Makwaia Makani.
Wataalam kutoka Cuba wanaofanya kazi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) wakimsikiliza Naibu Waziri huyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Lawrence Museru akiwa katika picha ya pamoja, Naibu Waziri wa Kilimo wa Cuba, Mhe. Miquel Rodriquez de Armas (kushoto) na Balozi wa Cuba nchini Tanzania, Mhe. Lucas Domingo Hernandez Polledo (kulia). Wengine ni baadhi ya wataalam wa Muhimbili na maofisa walioambatana na ujumbe huo. Picha na John Stephen, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)
Serikali ya Cuba imeeleza azma yake ya kuendelea kushirikiana na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) katika kutoa huduma bora za kibingwa sambamba na kuwajengea uwezo watalaam wa Muhimbili. Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Balozi wa Cuba nchini Lucas Domingo Hernandez Polledo ambaye ameambatana na ujumbe kutoka Serikali ya Cuba ukiongozwa na Naibu Waziri wa kilimo wa nchi hiyo, Jose Miguel Rodriguez de Armas.
Ujumbe huo umetembelea Muhimbili leo kwa lengo la kuangalia utendaji kazi wa hospitali pamoja na utendaji kazi wa watalaam wa afya 17 wa nchini Cuba ambao wapo Muhimbili kwa ajili ya kusaidia kutoa huduma. Awali, wakiwa katika mazungumzo na uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Balozi Polledo ameupongeza uongozi wa Muhimbili kwa utoaji bora wa huduma za matibabu na kueleza kuwa amekua akipata mrejesho mzuri kutoka kwa wataalam wao na kusisitiza kwamba ushirikiano huo haunabudi kudumishwa.
“Tunapenda ushirikiano huu uendelee kwa faida ya nchi zote mbili na endapo mkihitaji tuwaongezee wataalam wengine zaidi tupo tayari kuwapatia,” amesema Balozi Polledo. Balozi Polledo pia ametumia fursa hiyo kuwataka wataalam hao wa Cuba kuzidisha juhudi katika utendaji kazi kwa kuwa uwepo wao Muhimbili unawakilisha Serikali ya Cuba hivyo wanapaswa kuwa mabalozi wazuri.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Lawrence Museru amesema MNH inaridhishwa na huduma wanazotoa wataalam hao kwani uwepo wao umesaidia kuwajengea uwezo wataalam wa ndani katika maeneo mbalimbali wanayohudumia na kuiwezesha hospitali kufikia malengo yake ya kutoa huduma bora za kibingwa kwa wagonjwa mbalimbali.
Katika timu hiyo ya wataalam wapo Madaktari Bingwa wa usingizi wawili, madaktari bingwa wa magonjwa mahututi wawili, daktari bingwa wa upasuaji wa macho mmoja, mtaalam wa radiolojia mmoja pamoja na wauguzi kumi wa vyumba vya wagonjwa wanaohitaji uangallizi maalum (ICU).
Wataalam hao kutoka Cuba walianza kutoa huduma za afya katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Oktoba 2017 kufuatia makubaliano kati ya Serikali ya Cuba na Muhimbili ambapo watafanya kazi kwa muda wa miaka miwili.
No comments:
Post a Comment