Wafugaji wa jamii ya Wabarbaig katika Kijiji cha Endesh Kata ya Baray wilaya ya Karatu mkoa wa Arusha wakiimba nyimbo za asili wakati wa hafla ya kukabidhiwa hati ya kimila yenye mpango wa matumizi bora ya ardhi na nyanda za malisho iliyoandaliwa na Ujamaa Community Resouce Team(UCRT).
Mkuu wa wilaya ya Karatu mkoa wa Arusha,Theresia Mahongo(kulia) akiwa ameungana na Wanawake wa jamii ya kifugaji ya Wabarbaig katika Kijiji cha Endesh Kata ya Baray wakiimba nyimbo za asili.
Mkuu wa wilaya ya Karatu mkoa wa Arusha,Theresia Mahongo(kulia) akimkabidhi Hati ya Kimila Mwenyekiti wa Kijiji cha Endesh Kata ya Baray ,Geway Nanagi kutoka jamii ya kifugaji ya Wabarbaig wakati wa hafla ya kukabidhiwa hati ya mpango wa matumizi bora ya ardhi na nyanda za malisho iliyoandaliwa na Ujamaa Community Resouce Team(UCRT).
Mzee wa jamii ya kifugaji ya Wabarbaig katika Kijiji cha Endesh Kata ya Baray wilaya ya Karatu,mkoa wa Arusha,Gidaulanda Marakwa akifurahia Hati ya Kimila iliyoandaliwa na taasisi ya Ujamaa Community Resources Team.Picha na Filbert Rweyemamu
Mkuu wa wilaya ya Karatu,Theresia Mahongo amewaonya wananchi wanaowashawishi wenzao kukataa ardhi ya vijiji vyao isipimwe na kupangiwa matumizi bora ya ardhi kuwa serikali haitasita kuwachukulia hatua kali za kisheria .
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi Hati ya Kimila ya maeneo ya malisho kwa uongozi wa Kijiji cha Endesh Kata ya Baray jana amesema utaratibu wa kupima na kupanga matumizi bora ya ardhi una baraka za serikali na unalenga kupunguza migogoro ya ardhi kati ya wafugaji,wakulima na wawekezaji.
‘Serikali haitawaonea huruma wanaokwamisha juhudi za serikali kuhakikisha tunakua na vijiji vyenye ramani zinazotambulika kisheria na ambazo wananchi wamekubaliana namna ya matumizi ya ardhi katika shughuli za maendeleo,”amesema Mahongo
Amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa wataalam wa ardhi wanaofika katika maeneo yao kwaajili ya kupima na kupanga matumizi bora ya ardhi kwamba ni jambo zuri ambalo lina faida kubwa katika kujipangia mipango ya maendeleo.
Mratibu wa UCRT kanda ya Mang’ola ,Dismas Meitaya amesema eneo la Kijiji cha Endesh lina eneo la Hekta 40,000 na nusu ya eneo hilo limetengwa kwaajili ya malisho ya mifugo katika kipindi cha mwaka mzima hatua ambayo itapunguza migogoro na vijiji jirani.
Amesema wamewazesha wananchi kuweka mipango ya matumizi bora ya ardhi kwa kuzingatia matumizi endelevu ya ardhi na maliasili katika ngazi ya vijiji na wilaya pia kujenga uwezo wa jamii ya wawindaji,wafugaji na wakusanya matunda kumiliki na kusimamia ardhi yao.
Meitaya ameongeza katika wilaya hiyo wamekeleza majukumu yao katika vijiji nane ambavyo ni Qang’ded,Dumbechand,Mbunga-nyekundu,Endesh,Matala,Jobaj,Mikocheni na Endamaghan ikiwa na kuwapa mafunzo ya kuanzisha mabaraza ya ardhi ya vijiji na Kata.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Endesh,Gibway Nanagi amesema maisha ya wafugaji yanategemea ardhi hivyo baada ya kupata hati ya kimila ya kijiji chao inayoonesha matumizi bora ya ardhi imekua ni faraja kubwa na kuishukuru serikali kufanikisha mpango huo.
No comments:
Post a Comment