VIONGOZI mbalimbali wa vyama vya siasa vya upinzani nchini, wakiwemo Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamadi, Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, Edward Lowassa na Kiongozi wa ACT – Wazalendo, Zitto Kabwe wamejichimbia visiwani Zanzibar wakijipatia mafunzo mbalimbali juu ya mwenendo wa siasa na demokrasia.
Mbali na hao, viongozi wengine walionekana na Rais wa Chama Cha Mawakili Tanzania, (TLS) Fatma Karume na viongozi wengine mashuhuri nchini ambapo imeelezwa walijadili juu ya mwenendo wa hali ya kisiasa nchini tangu jana Jumatatu, Desemba 17, 2018.
Kaimu Msemaji wa CUF, Mbarara Maharagande amesema kikao hicho kimeandaliwa na taasisi ya marekani IRI kupitia kwa Katibu wa CUF, Maalim Seif.
“Ni kweli kuna semina inafanyika ya viongozi wa vyama inafanyika Zanzibar ambayo inafanyika kwa siku tatu, na aliyewaalika ni Katibu Mkuu wetu Maalim Seif na imeandaliwa na taasisi ya IRSA, watu wa democratic ya America,” amesema Maharagande.
Kupitia ukurasa wake wa Twitter Maalim Seif aliandika; “Ni heshima kubwa kwangu na kwa CUF kuandaa na kuwa mwenyeji wa kikao cha kutathmini demokrasia yetu na kujitathmini sisi wenyewe kama vyama vya upinzani na mwelekeo wetu.”
No comments:
Post a Comment