ANGALIA LIVE NEWS

Monday, December 17, 2018

WAZIRI LUKUVI ALINIKABA NA KUNIPORA MKOBA WANGU ULIOKUWA NA FEDHA-KILUWA

Na Karama Kenyunko, globu ya Jamii.

MSHITAKIWA Mohamed Kiluwa (50) anayekabiliwa na shtaka la kutoa rushwa ya Sh. Milioni 90 kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Willium Lukuvi, ameieleza mahakama ya Wilaya ya Ilala kuwa Waziri Lukuvi alimkaba na kumpora mkoba uliokuwa na fedha zake. 

Kiluwa ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Kiluwa Steal Group. Co.ltd na Kiluwa Free Processing Zone amedai hayo leo Desemba 17.2018 wakati akitoa utetezi wake mbele ya Hakimu Mkazi Samweli Obas.

Akiongozwa na Wakili wake Imani Madega kutoa utetezi wake, Kiluwa amedai Julai 14 mwaka huu  alipata taarifa kutoka kwa  Shabani Selemani aliyemtaarifu kuwa anatakiwa kupeleka hati zake za viwanja ofisini kwa Waziri Lukuvi, ndipo Julai 16, 2018 alifanikiwa kufika ofisini hapo kwa Waziri na kumkuta akiwa peke yake.

Amedai baada ya kumuelekeza Mahali pa kukaa alimuuliza hati zake ziko wapi na yeye akamjibu kuwa anazo mbia mwenzake ambaye kwa wakati ule alikuwa amesafiri.

Aliendelea kudai kuwa, Waziri Lukuvi  alimuuliza tena kuwa hati ziko wapi na kumjibu kuwa mwenzake akirudi ataziwasilisha kwake baada ya majibu hayo Waziri Lukuvi alikaa kimya kama dakika tatu kisha akanyanyuka na kumuuliza kwenye mkoba wake amebeba nini.

Nilimwambia kuna fedha za shoping za ofisini kwangu, baada ya jibu hilo Waziri aliinuka na kuniambia nimpatie mkoba huo, mimi nikawa namwangalia, ikafika wakati alinishika, akaniinua na kuninyanganya begi kisha akalifungua  akatoa fedha na kuziweka juu ya meza.


"Baada ya kitendo kile cha kuninyanganya begi nikawa napiga kelele nikisema nisaidieni.... Muda mfupi kidogo mlango ulifunguliwa na akaingia mtu mmoja na kuniambia nipo chini ya ulinzi lakini Kabla hajamaliza akaingia mwingine naye akasema nipo chini ya ulizi nirudi nyuma hatua mbili, "alidai Kiluwa.

Baada ya watu hao kuingia Waziri Lukuvi alitoka nje ya ofisi na kumuacha yeye pamoja na watu hao wawili waliongia na kumuweka chini ya ulinzi,  ambapo walianza kujiuliza maswali juu ya nani wamfanye shahidi katika tukio hilo.

"Tumfanye nani shahidi,  waliulizana mmoja akajibu muulize mheshimiwa ndipo akatoka nje,  aliporudi akasema Waziri amesema wamwite Sekretari wake ili awe shahidi, Sekretari alikuja na wakamwambia kuwa asome namba za kila fedha iliyopo mezani na ndivyo alivyofanya, "alidai Kiluwa.

Akizidi kujitetea,  Kiluwa ameiomba mahakama imuachie huru kwa kuwa si Waziri Lukuvi wala mashahidi wa upande wa mashitaka waliofika mahakamani hapo kutoa ushahidi waliothibitisha kuwa alitoa rushwa.

"Mimi sina hatia naiomba Mahakama iniachie huru mimi na pia inirejeshee mali zangu walizozishikilia, naiomba pia inipatie hati zangu na kuzirudisha katika daftari la msajili, "alidai.

Aidha Kiluwa alidai kuwa Waziri Lukuvi anatumika na baadhi ya wafanyabiashara nchini kumuharibia jina lake na biashara zake, jambo ambalo litakwamisha azma ya Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli ya kufikia uchumi wa viwanda.

Kilua Aliendelea kudai Kuwa,  anaviwanja 73 lakini mpka sasa ameshapata hati za viwanja 57 na kwamba  katika hatua zote za kupata hati hizo hajawahi kuombwa wala kutoa rushwa.

Naye shahidi wa pili upande wa Utetezi, ambaye ni miongoni mwa wamiliki na mwanahisa katika Kampuni ya Kiluwa, Jurijs Martinovs alidai mahakamani hapo kuwa Julai 3 mwaka huu alisafiri kupeleka watoto likizo kwa bibi yao nchini Latvia na kurejea Tanzania Agosti 16 mwaka huu.

Martinovs aliwasilisha nakala ya pasipoti ya kusafiria kuonyesha kwamba alisafiri na mahakama iliipokea kama kielelezo cha utetezi katika kesi hiyo.

Baada ya kusikilizwa utetezi huo Hakimu Obas aliharisha kesi hiyo hadi Desemba 24 kwa ajili ya kutoa hukumu.

Kiluwa  anadaiwa kutoa rushwa ya USD 40,000 ambazo ni sawa na Sh milioni 90 kwa Waziri Lukuvi.
Fedha ambazo inadaiwa lengo lake ilikuwa asiwasilishe hati ya umiliki wa kiwanja namba 57 Block B Kikongo na D Disunyura kilichopo eneo la viwanda lililopo Kibaha mkoani Pwani. Kiluwa yupo nje kwa dhamana.

No comments: