Advertisements

Friday, January 11, 2019

Balozi Seif aongoza matembezii ya miaka 55mya Mapinduzi ya Zanzibar

Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Balozi Seif  akiwa pamoja na Viongozi wa UVCCM Wakijiandaa kuyapokea Maandamano ya Umoja wa Vijana wa CCM kuadhimisha kumbukumbu za Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Mwaka 1964 hapo Uwanja wa Gombani ya Kale Chake Chake Pemba.
Kanyaga kanyaga ni nyimbo wanaoimba Vijana hao wa UVCCM wakati wakiingia kwenye Uwanja wa Gombani ya Kale baada ya kumaliza Matembezi yao katika sehemu mbali mbali za Kisiwa cha Pemba.

Vijana wa UVCCM  wakionekana kuhamasika na umalizaji salama wa Matembezi yao ulioambatana na kazi za kujitolea  katika Miradi ya Kijamii na Kisiasa.
 Balozi Seif  akimpongeza Kiongozi wa Matembezi ya UVCCM Abdullah Ali Chum { Koti } baada ya kukabidhiwa  salama Picha ya Mwenyekiti wa CCM Taifa Dr. John Pombe Magufuli iliyotumika kwenye Matembezi hayo.
Vijana wa matembezi ya kumbukumbu ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964 wa UVCCM wakifurahia na kushukuru huduma nzuri za Afya na lishe walizozipata wakati wa Matembezi yao ya Siku Tano Pemba.
Baadhi ya Vijana wa UVCCM wakifuatilia matukio mbali mbali yaliyokuwa yakifanyika katika Uwanja wa Michezo wa Gombani ya Kale wakati wa kuhitimisha Matembezi yao yaliyoanzia katika Kijiji cha Chokocho Mkoa wa Kusini Pemba.
Balozi eif akikabidhi Vyeti Maalum kwa Vijana wa UVCCM walioshiriki matembezi ya kumbukuimbu ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964 yaliyomng’oa Mkoloni katika Ardhi ya Visiwa vya Zanzibar.
 Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa (UVCCM ) Mkoa wa Kibaha  Azilongwa Bohari akipokea Cheti Maalum kwa niaba ya Washiriki wenzake  cha Kuchiriki Matembezi hayo. Picha na – OMPR – ZNZ.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi alisema Vijana walioshiriki matembezi ya Miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar wanapaswa kujenga ufahamu wa kujuwa Mapinduzi ndio yaliyoleta Ukombozi na kupatiana Mamlaka kamili ya Mwafrika yanayoharakisha Maendeleo ya Jamii hivi sasa.

Alisema jukumu la Vijana hao kwa wakati huu waelewe kwamba Uhuru wa Taifa hili wakati wowote utalindwa na wao wenyewe kwa vile hakuna Mtu au Kikundi kitakachokuja Zanzibar na Tanzania Nzima  kuwalindia Uhuru walioachiliwa kama urithi wao.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati akiyapokea na kuyafunga Matembezi ya Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi {UVCCM} ya kuunga mkono Mapindui ya Zanzibar ya Mwaka 1964 yaliyohitimishwa hapo katika Uwanja wa Gombani ya Kale Chake Chake Kisiwani Pemba.

Alisema Vijana hao ndio warithi halali wa Mapinduzi hayo kwa sababu Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964 yalifanywa na Vijana chini ya Viongozi wa ASP Youth Leagae kwa wakati huo wakitekeleza Muongozo wa Afro Shirazy Party uliolenga kuondoa matendo mabaya, madhila na manyanyaso kwa Waafrika wa Zanzibar.

Balozi Seif aliwataka Vijana hao kuziepuka fitina za kudharauliana wenyewe kwa wenyewe na badala yake waimarishe Umoja na Mshikamano waliokuwa nao miongoni mwao na kamwe wasikubali kutenganishwa kwa vile makundi ni sumu ya Umoja wao.

Alieleza kwamba Waafrika wa Zanzibar baada ya kuchoshwa na Utawala wa Kikoloni waliendelea kushikamana , kuungana kuwa wamoja  kulikowasaidia kuikomboa Nchi yao toka mikononi mwa wageni kwa nia ya kujitawala na kujiamulia mambo yao wenyewe katika Ardhi yao.

Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM Taifa alifahamisha kwamba wakati wananchi na Viongozi wanaposema Mapinduzi Daima inamaanishwa kwamba Serikalki itaendelea kuondoa matendo mabaya, udhalilishaji wa Wanawake na Watoto pamoja na mambo yote yanayorejesha nyuma  au kukwamisha juhudi za kujiletea Maendeleo.

Balozi Seif alielezea faraja yake kutokana na ushiriki wa Vijana kwenye Matembezi  hayo ukiwa  mkubwa jambo ambalo linadhihirisha wazi jinsi gani walivyokomaa Kisiasa pamoja na utayari wao wa kutetea, kulinda na kuyaenzi Mapinduzi ya Zanzibar  kwa vitendo.

Alisema Nchi imetoka mbali kutokana na majaribu mengi iliyopata zilizotokana na changamoto nyingi zinazoonekana kusababishwa na wale wasioitakia mema ambao ni vibaraka wa hao waliopinduliwa Mwaka 1964.

Aliwapongeza Vijana wa kuendelea kulinda Amani ya Taifa huku wakitambua kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ile ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania zimepiga hatua kubwa ya Maendeleo kutokana na  Amani hiyo.

Balozi Seif Ali Iddi akiwa pia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliendelea kuwakumbusha Wananchi kushiriki sherehe za Mapinduzi katika misingi ya Amani na utulivu kama ilivyozoeleka.

Alisema ni vyema kwa Mtu au Kikundi chochote kilichotia niya ya kushiriki sherehe hizo katika mazingira ya kutaka kufanya ushawishi wa vurugu Vyombo vya Dola havitakuwa na mzaha wa kuwadhibiti watu hao hao.

Akitoa Taarifa ya Matembezi  hayo ya Umoja wa Vijana wa CCM Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar Nd. Mussa Haji Mussa alisema matembezi hayo yaliyozinduliwa Tarehe 5 Januri na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dr. Abdullah Juma Saadala katika Kijiji cha Chokocho Mkoa Kusini Pemba.

Nd. Mussa alisema zaidi ya Vijana 400 walishiriki matembezi hayo kwa kuamua kubadilika katika kushiriki zaidi kwenye kazi za Jamii ikiwemo ujenzi wa Taifa wa  Majengo ya Skuli na Matawi ya Chama cha Mapinduzi kwa kuweka alama mote walimopita.

Alisema Umoja wa Vijana utaendelea kuyalinda Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar kwa gharama yoyote ile na kamwe hakutakuwa na Mapinduzi mengine tena kwa vile kila Mwana jamii ameshuhudia kuwa huru kufanya analotaka kwa mujibu wa sheria.

Nd. Mussa alieleza kwamba Mapinduzi hayo ya Zanzibar yameleta utu na usawa wa Wananchi wote wa Zanzibar licha ya baadhi ya Wanasasa uchwara wakijaribu kudhihaki Mapinduzi hayo.

Akimkaribisha Mgeni rasmi kuyafunga matembezi hayo Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM Taifa Nd. Kheri Denis James alisema Vijana wa CCM wana jukumu la kutangaza kazi kubwa inayoendelea kutekelezwa na Marais wote wawili wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Nd. Kheri alisema tafsiri sahihi ya Mapinduzi Daima inayoendelea kutekelezwa hivi sasa imelenga katika kuimareisha Uchumi na Maendeleo ya Taifa ambayo Vijana wanalazimika kupigana kiume katika kuyalinda Maendeleo pamoja na Uchumi huo.

Mwenyekiti huyo wa Umoja wa Vijana wa CCM Taifa aliwaeleza Washiriki wa Matembezi hayo kwamba Wazee Waasisi wa Bara na Zanzibar waliacha Vyama vyenye nguvu kubwa  Vya TANU na ASP na baadae CCM zinazopaswa kudumishwa kwa ustawi wa Kizazi kijacho.

Ujumbe wa Mwaka huu wa Matembezi hayo ya Vijana wa Chama cha Mapinduzi {UVCCM} ya kumbukumbu ya Mapinduzi ya Zanzibar YA Mwaka 1964 unaeleza kwamba “ CCM na Vijana Mapinduzi yanaendelea kufana”.

No comments: