Dodoma/Dar. Unaweza kusema hapatoshi kati ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad na Spika Job Ndugai.
Hiyo ni baada ya jana Spika Ndugai kuitisha mkutano na waandishi wa habari ofisini kwake Dodoma na kumtaka Profesa Assad kufika mbele ya Kamati ya Maadili, Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge Januari 21 kwa hiari yake kwa ajili ya kuhojiwa kuhusu madai ya kulidhalilisha Bunge, vinginevyo atapelekwa akiwa amefungwa pingu.
Mbali na CAG, mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee naye ameitwa katika kamati hiyo Januari 22 kwa madai ya kutoa kauli iliyounga mkono kilichosemwa na Profesa Assad.
Hatua hiyo ya Spika Ndugai imeibua mjadala mzito kwenye mitandao ya kijamii huku watu wa kada mbalimbali wakiwamo wanasheria na wabunge wakitoa maoni kupinga.
Akihojiwa hivi karibuni na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa na mtangazaji Anord Kayanda kuhusu ukaguzi unaofanywa na ofisi yake kuonekana na wananchi kuwa haufanyiwi kazi CAG alisema, “Kama tunatoa ripoti zinazoonyesha kuna ubadhirifu halafu hatua hazichukuliwi, huo kwangu ni udhaifu wa Bunge. Bunge linatakiwa kusimamia na kuhakikisha pale panapoonekana kuna matatizo basi hatua zinachukuliwa.”
“Sisi kazi yetu ni kutoa ripoti. Na huu udhaifu nafikiri ni jambo lenye kusikitisha. Lakini ni jambo ambalo muda si mrefu huenda litarekebishika. Ni tatizo kubwa ambalo tunahisi Bunge linashindwa kufanya kazi yake kama inavyotakiwa.”
Kwa kauli hizo, Ndugai pia alimtaka pia Profesa Assad ajitathmini kama anatosha katika nafasi yake.
“Kama ni upotoshaji basi CAG na ofisi yake ndiyo wapotoshaji, huwezi kusema nchi yako vibaya unapokuwa nje ya nchi, na kwa hili hatuwezi kufanya kazi kwa kuaminiana,” alisema Ndugai.
“Mle ndani (bungeni) kuna mawaziri, Waziri Mkuu, spika na naibu wake. Kitendo hiki kimenikasirisha sikutegemea msomi kama huyo angeweza kutoa maneno ya kudhalilisha Bunge lililojaa wasomi zaidi ya mabunge yote tangu Uhuru.”
Ndugai alisema si kweli kwamba Bunge ni dhaifu na kwamba wameipokea kauli hiyo kwa masikitiko kwa kuwa taarifa za CAG zinafanyiwa kazi.
“Sikatai Bunge kukosolewa, lakini nachukizwa na dharau na kwa kweli kama ni upotoshaji basi ofisi ya CAG ni wapotoshaji namba moja. Huwezi kusema una uhuru wa kuongea katika nafasi yako halafu unakwenda kutoa maneno ya tuhuma ya kudhalilisha nchi yako nje ya nchi,” alisema Ndugai.
Alisema kuna watu lazima watajitokeza na kuhoji kuhusu uhuru wa ofisi ya CAG na kusisitiza kwamba hakuna uhuru usiokuwa na mipaka kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania.
Alisema kilichozungumzwa na Profesa Assad ni sawa na mkimbizi ambaye anaweza kusema chochote, kwamba mtu mwenye misingi ya utaifa hawezi kusema vibaya Serikali yake akiwa nje ya nchi.
Alimtaka CAG kupeleka maelezo ya hoja moja baada ya nyingine ambazo hazikujibiwa au kufanyiwa kazi ili Bunge chini ya kamati zake mbili ambazo zinaongozwa na wabunge wa upinzani wakazifanyie kazi.
Kamati za Bunge zinazoongozwa na wapinzani ni ile ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na ya Hesabu za Serikali (PAC).
Kuhusu Mdee, Ndugai alisema aliunga mkono kilichozungumzwa na Profesa Assad, hivyo naye anapaswa kufika mbele ya kamati hiyo kwa ajili ya kuhojiwa.
Baada ya kauli ya Spika
Baada ya kauli hiyo, waandishi wetu walizungumza na baadhi ya wanasheria kupata maoni yao kuhusu hatua hiyo ya Spika. Akitoa maoni yake, wakili wa kujitegemea, Faraja Mangula alisema kwa mujibu wa Katiba wa nchi, Bunge linaweza kumuita mtu yeyote linapomhitaji bila kujali yeye ni nani, lakini alikosoa utaratibu ulioutumiwa na Spika.
“Katiba imelitaja Bunge kama chombo huru na CAG naye ametajwa kama taasisi huru ambayo haipaswi kuingiliwa na wote Katiba imewalinda. Kwa mfano, mchakato wa kumuondoa CAG madarakani ni mrefu na ilifanyika hivyo ili kumlinda,” alisema Mangula.
Alisema licha ya kuwa Bunge limepewa mamlaka ya kumuita mtu yeyote, lakini CAG ambaye Katiba inamlinda hajatendewa haki kwa namna alivyoitwa.
“Kwa maoni yangu naona Spika alipaswa kutumia njia za ndani kumuita kiongozi huyo badala ya kutumia kauli za kusherehesha kama vile kuna jambo baya sana amefanya.”
Wakili Albert Msando alisema Spika anapaswa kujitathmini kwani jambo alilolifanya linasababisha mgongano usio wa lazima baina ya Serikali, Bunge na ofisi ya CAG.
“CAG hawezi kuitwa kwa mkutano wa waandishi wa habari na Spika tayari ameitisha kamati ya maadili imshauri, lakini amekimbilia kufanya kazi ya kamati hiyo na anatoa lugha ya vitisho vya pingu na kumuita CAG,” alisema.
Alisema hoja ya Ndugai kuwa mtu hapaswi kusema vibaya mambo yanayohusu nchi akiwa ughaibuni haina mashiko kwani CAG alitoa kauli hiyo kulingana na mazingira, lakini vilevile ni haki yake kutoa maoni kuhusu jambo lolote.
Wakili Fulgence Masawe alisema Ndugai hakushauriwa vizuri kabla ya kutoa kauli hiyo na kwamba CAG amewekewa kinga katika Katiba ambayo ndio sheria mama na hakuna kanuni inayoweza kuwa juu ya msingi wa Katiba.
“Spika anamuita kwa mujibu wa kanuni ambazo ziko chini ya Katiba, haziwezi kuwa na mamlaka hayo, CAG anatakiwa kuwa huru kwa mujibu wa sheria hiyo, kwa hiyo unapoanza kumwajibisha na kumwita mbele ya suala hili ni kuathiri utendaji na ukiukwaji wa sheria inayompatia uhuru wa kutekeleza majukumu yake,” alisema Masawe.
Nyongeza na Kelvin Matandiko
No comments:
Post a Comment