ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, January 3, 2019

UCSAF YALETA CHANGAMOTO CHANYA KWA KAMPUNI ZA SIMU ZA MKONONI

Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (wa tatu kulia) akisikiliza kwa makini taarifa kutoka kwa Afisa Mtendaji Kata ya Katwe, Wilaya ya Sengerema, Mwanza, Deus Ngodagula Masasi (aliyenyoosha kidole) kuhusu ukosefu wa mawasiliano kwenye kisiwa cha Maisome wakati wa ziara yake ya kukagua hali ya mawasiliano wilayani humo. Naibu Katibu Mkuu – Sekta ya Mawasiliano Dkt. Jim Yonazi (aliyeshika ramani) akiwa na Mkurugenzi wa Uendeshaji, UCSAF, Mhandisi Albert Richard (wa kwanza kushoto).
Naibu Katibu Mkuu – Wizara Ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Sekta ya Mawasiliano Dkt. Jim Yonazi (aliyeinua mkono) akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (wa kwanza kulia) wakati wa ziara yake ya kukagua changamoto ya mawasiliano kisiwani Maisome, Mwanza. Anayesikiliza wa kwanza kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya TCRA, Dkt. Jones Kilimbe.
Diwani wa Kata ya Bangwe, wilayani Sengerema, Mwanza, Yonas Magikulu akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (wa kwanza kulia) wakati wa ziara yake ya kukagua hali ya mawasiliano Wilayani humo. Wa kwanza kushoto ni Naibu Katibu Mkuu, Wizara Ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Sekta ya Mawasiliano Dkt. Jim Yonazi.

Mkurugenzi Uendeshaji wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Mhandisi Albert Richard amemweleza Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye kuwa UCSAF imeleta changamoto chanya kwa kampuni za simu za mkononi zinazotoa huduma za mawasiliano nchini
Richard ameyasema hayo wakati wa ziara ya Nditiye ya kukagua changamoto za mawasiliano kwenye maeneo mbali mbali wilayani Sengerema mkoani Mwanza.  Richard amefafanua kuwa awali kampuni za simu za mkononi nchini zilisita kuwekeza kwenye vijiji mbali mbali ambavyo havina mawasiliano nchini kwa kuwa havina mvuto wa kibiashara ambapo kampuni hizo zilikuwa zinakwenda maeneo ya mijini yenye mvuto wa kibiashara
“Ila sasa Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano tunashirikiana na kampuni za simu za mkononi kufikisha huduma za mawasiliano vijijini na kampuni zimepata mwako,” amesema Richard. Ameongeza kuwa Serikali imekuwa inatoa ruzuku kwa kampuni hizo ili waweze kujenga minara kwa lengo la kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma za mawasiliano
Nditiye amesema kuwa amefanya ziara ya siku tatu ya kukagua mawasiliano kwenye maeneo mbali mbali wilayani Sengerema ili kuona changamoto za mawasiliano ambapo amekiri uwepo wa changamoto za mawasiliano kwenye Wilaya hiyo kwenye baadhi ya kata ambapo ina jumla ya kata 21 na kubaini uwepo wa ukosefu wa mawasiliano kabisa kwenye baadhi ya maeneo, mawasiliano ya kusuasua na mahitaji ya kuongeza nguvu ya usikivu wa mawasiliano kwenye baadhi ya maeneo
Pia, amekiri kuwa wameshindwa kufika moja kwa moja kwenye kata ya kisiwa cha Maisome ambapo kuna wananchi wengi wanaoishi huko na hawana mawasiliano kwa kuwa kisiwa hicho kinasomeka kwenye ramani kuwa ni hifadhi ya misitu ambapo kampuni ya Halotel wamepata ruzuku kutoka UCSAF ya kujenga minara ya kufikisha mawasiliano kwenye kisiwa hicho
“Nimemwelekeza Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Sekta ya Mawasiliano, Dkt. Jim Yonazi aonane na Wizara husika ya Maliasili na Utalii na taasisi ya misitu ya TFS ili waweze kupata kibali cha kuiwezesha Halotel kujenga minara,” amesema Nditiye
Nditiye ameilekeza UCSAF na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) wafanye tathmini ya hali halisi ya mawasiliano wilayani Sengerema. Pia, washirikiane kwa pamoja na kampuni za simu za mkononi kuongeza nguvu za mawasiliano kwenye maeneo mbali mbali ambayo hayana mawasiliano, kujenga minara kwenye maeneo ambayo hayana mawasiliano kabisa au kuweka minara mingine ya ziada kwa kuwa mawasiliano ni ulinzi na usalama, mawasiliano ni uchumi
Naye Dkt. Yonazi amesema kuwa amezingatia maelekezo na wataboresha mawimbi ili wananchi waendelee kupata mawasiliano katika eneo la Buchosa na tutaendelea kuboresha usikivu  wa mawasiliano na kufikisha mawasiliano kwenye maeneo ambayo hakuna mawasiliano kabisa. Ameongeza kuwa tutaendelea kutoa elimu kwa wananchi na tutashirikiana na TCRA ili kuhakikisha ubora wa mawasiliano kwa wananchi unaboreshwa
Mwenyekiti wa Bodi ya TCRA, Dkt. Jones Kilimbe amesema kuwa tumefika Buchosa na tumeshuhudia wenyewe hali ya mawasiliano Buchosa na tumeona kuna baadhi ya sehemu hakuna mawasiliano kabisa na kwingine nguvu ya mawasiliano ni ndogo na ziara hii itatuwezesha kufanyia kazi changamoto hizi sehemu mbali mbali nchi nzima
“Ni jukumu letu kuhakikisha wananchi wanapata huduma za mawasiliano hususani kuwahudumia wananchi wanaoishi vijijini,” amesema Kilimbe. Ameongeza kuwa mawasiliano ni maendeleo na ni uchumi, watu wanatumia huduma za mawasiliano ikiwa ni pamoja na kutuma na kupokea pesa
Richard ameongeza kuwa hadi sasa asilimia 94 ya watanzania wanapata huduma za mawasiliano na asilimia 6 iliyobaki ni ya watu wachache ambapo Serikali inaendelea kupata ufumbuzi wa teknolojia rahisi ya kufikisha mawasiliano na kwa maeneo ya Buchosa ambayo yana changamoto za mawasiliano zitajumuishwa kwenye zabuni za mwaka 2019 ili maeneo hayo yapate mawasiliano

No comments: