ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, January 10, 2019

WADAU WAKUTANA TABORA KUANDAA JUMBE ZA KUTOKEMEZA UKATILI WA WANAWAKE NA WATOTO

 Kaimu Katibu  Tawala Mkoa wa Tabora Raphael Nyanda (katikati) akifungua mafunzo ya kuandaa ujumbe wa kupinga ukatili dhidi ya wananwake na watoto na mimba za utotoni. Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi kutoka Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii ya Wizara ya Afya , Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Grace Mwangwa na kushoto niAfisa aneyeshughulikia Maendeleo ya Jamii kutoka Ofisi ya Rais , Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mwajina Ally.
 Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya  kuandaa ujumbe wa kupinga ukatili dhidi ya wananwake na watoto na mimba za utotoni  wakiwa katika mafunzo hayo mjini Tabora.
Kaimu Katibu  Tawala Mkoa wa Tabora Raphael Nyanda(katikati) akiwa katika picha ya pamoja na washiri wa  mafunzo ya kuandaa ujumbe wa kupinga ukatili dhidi ya wananwake na watoto na mimba za utotoni. Picha na Tiganya Vincent

WANANCHI wametakiwa kuunganisha nguvu pamoja kuhakikisha wanatokemeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto na mimba za utotoni hapa nchini kama ilivyoekelezwa katika Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokemeza Ukatili wa wanawake na watoto(MTAKUWWA). Tatizo hilo linasababisha athari nyingi ikiwemo vifo, ulemavu , kuwa na kundi kubwa la watoto kukimbilia mitaani na umaskini kwa watoto wanaokatishwa masomo na ndoto zao la baadae na hivyo kudhofisha juhudi za ujenzi wa uchumi wa kati na viwanda hapa nchini.

Kauli hiyo imetolewa  na Katibu Tawala Mkoa wa Tabora Msalika Makungu katika hotuba yake iliyosomwa na Katibu Tawala Msaidizi Raphael Nyanda kwenye ufunguzi wa mafunzo ya kuandaa ujumbe wa kupinga ukatili dhidi ya wananwake na watoto na mimba za utotoni. Alisema suala hilo ni kubwa katika baadhi ya jamii na hivyo linahitaji kila mwanajamii kuwa mstari wa mbele kukemea na kutoa taarifa ambazo zitasaidia kukomesha ukatili kwa watoto , wanawake na kuondoa ndoa na mimba za utotoni hapa nchini na wahusika kufikishwa katika vyombo vya sheria.

 Nyanda alisema kuwa wakati mwingine vitendo vya ukatili vimekuwa vikifanyika katika jamii huku  wanajamii wanakaa kimya wakiwemo baadhi ya viongozi wa maeneo husika wakiwa wamefumba macho. Alisema ni lazima jamii itambue kuwa ukatili unafanyika kwa mtoto wa jirani kesho unaweza kufanyikwa kwa watoto wao na hivyo wanapaswa kuchukua hatua wanapoona vitendo vya namna hiyo vikifanyika.

 Awali Mkurugenzi Msaidizi kutoka Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii ya Wizara ya Afya , Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Grace Mwangwa alisema mikoa ambayo ina vitendo vya juu vya ukatili wa wanawake na watoto ndio hiyo hiyo ipo juu katika tatizo la mimba na ndoa za utotoni. Aliitaja mikoa inayoongoza kwa mimba za utotoni kuwa ni Katavi kwa  asilimia 45, Tabora asilimia 43, Morogoro 39 na  Mara asilimia 39 na kwa upande wanajifungua kwa umri mdogo  ni Shinyanga kwa asilimia 59, Tabora 58, Mara 55, Dodoma 51 na Lindi 48.

 Mwangwa aliwaomba viongozi wa Dini hapa nchini kutumia ushwawishi wao wa kiroho kukemea ukatili wa wanawake na watoto kama vile upigaji wa wanawake na watoto, ukeketaji unaoendelea kwa siri katika baadhi ya maeneo, ndoa za utotoni na mimba za utotoni ambazo nyingine zinatokana na kubakwa.

 Aidha aliwataka wazazi au walezi wa watoto kuwa makini na kuwalaza watoto wao chumba kimoja na wageni kwa kuwa wakati unyanyasaji ikiwemo ubakaji na ulawiti unafanywa na watu hao ambao wamekaribishwa kama ndugu au marafiki. Alisema hatua hiyo inatokana na utafiti ambao umeonyesha asilimia 60 ya ukatili kwa watoto ufanyika nyumbani na 40 ndio unaofanywa katika maeneo ya Shule.


 Mkurugenzi Msaidizi huyo alisema ukatili kwa watoto ni pamoja na matusi, vipigo, kuchomwa moto wakifanya kosa, kunyimwa chakula, kubakwa, kulawitiwa na kuolewa katika umri mdogo. Aliitaka jamii kurudi katika mitazamo ya awali ambapo kila mtu mzima alimchukulia kila mtoto anayemuona mbele yake ni mwanae.

No comments: