ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, February 27, 2019

Kifo cha Ruge gumzo kila kona

Mwananchi
Ruge Mutahaba, mtu aliyejitoa maisha yake kuendeleza burudani hasa sanaa ya muziki, kufundisha vijana ujasiriamali na kuongoza kampuni maarufu ya Clouds Media, amefariki dunia baada ya kuugua kwa muda.

Ruge alikuwa mdau mkubwa wa burudani, akishiriki kuanzisha matamasha makubwa ya muziki kama Fiesta, Summer Jam, kuunganisha wasanii katika kampeni mbalimbali za kijamii kama Kipepeo, Fursa na Nyumba ni Choo. Alishirikiana na Joseph Kusaga, ambaye ni mkurugenzi mtendaji wa Clouds Media, kuanzisha studio ya Mawingu na baadaye Clouds Media.

Pia alianzisha kampuni ya kuratibu shughuli za muziki ya Primetime Promotions na kituo cha Tanzania House of Talents (THT), ambacho kimezalisha wasanii wengi maarufu kama Barnaba, Mwasiti, Lina, Nandy, Maua Sama, Amini na Ruby.

Katika siku zake za mwisho, Ruge, ambaye habari zinasema alikuwa na tatizo la figo lililosababisha aende kutibiwa nje ya nchi, alikuwa akitibiwa Afrika Kusini.

“Tumepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha kijana wangu Ruge Mutahaba. Daima nitamkumbuka kwa mchango wake mkubwa katika tasnia ya habari, burudani na juhudi za kujenga fikra za maendeleo kwa vijana. Poleni wanafamilia, ndugu, jamaa na marafiki,” ameandika Rais John Magufuli katika akaunti yake ya Twitter.

Kituo cha redio cha Clouds FM kilitangaza kifo hicho majira ya saa 1:40 wakati wa kipindi cha “Amplifier” ambacho kilikatisha matangazo yake.

“Tumepata taarifa ambazo zimetustua. Mmoja wa waasisi wa Clouds Media, Ruge Mutahaba amefariki leo akiwa hospitalini Afrika Kusini,” alisema mtangazaji wa kipindi hicho, Millardo Ayo na kuachia muziki wa “Kamanda” wa Daz Nundaz ambao kibwagizo chake kinasema “Kalale pema peponi kamanda”.

Muda mfupi baadaye, Clouds Media waliandika katika akaunti ya Twitter kuhusu kifo hicho.

“Tunasikitika kutangaza kifo cha mkurugenzi wetu wa vipindi na uzalishaji Clouds Media,

Ndugu Ruge Mutahaba. Ruge ametutoka leo huko Afrika Kusini akipatiwa matibabu. Mioyo yetu imejeruhiwa. Tutaendelea kuwapa taarifa zote kuhusiana na msiba huu mzito,” Clouds imeandika katika akaunti hiyo.

Pamoja na Clouds FM kutoa taarifa wakati huo, habari za kifo cha Ruge zilishazagaa mapema mitandaoni.

Habari hizo zilianza kuzagaa majira ya saa 1:00 jioni wakati watumiaji wa mitandao ya kijamii walipozitoa kwa njia tofauti, wengi wakimuomba Mwenyezi Mungu ailaze pema

peponi roho yake na wengine kwa kusifia kazi kubwa aliyoifanya katika nyanja ya burudani.

“Rest in peace our brother Ruge (pumzika kwa amani kaka yetu),” ameandika Maria Sarungi katika akaunti yake ya Twitter akiweka mikono miwili ya kuonyesha kutoa pole.

“Mchango wako katika sekta ya habari umeacha alama isiyofutika. Pumzika kwa amani.”

Barnaba Elias, msanii aliyekuzwa katika kituo cha Tanzania House of Talents kilichoanzishwa na Ruge, alikuwa na maneno ya majonzi zaidi.

“Baba, baba, baba. Wewe Ruge, nani ataniambia Barnaba imba tena. Wewe baba, amka Ruge baba. Wewe moyo wangu, jamani naumia. Mimi, wewe uliniambia niimbe. Wewe Ruge wewe, Mungu nisaidie,” ameandika Barnaba katika akaunti yake ya Twitter.

Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba naye ameandika “umeondoka

Ruge Mutahaba, umeondoka shujaa, umeondoka mpambanaji. Pole kwa familia, ndugu na jamaa. Pole zaidi kwa Watanzania kwa msiba huu mzito. Najua ya kuwa wewe waweza

kufanya mambo yote na ya kuwa makusudi yako hayawezi kuzuilika-Ayubu 42:2”.

Soma zaidi: VIDEO: Kusaga kutoa ratiba ya mazishi ya Ruge

No comments: