ANGALIA LIVE NEWS

Friday, February 22, 2019

RAIS DKT. MAGUFULI AOMBOLEZA VIFO VYA WATU 19 WILAYA MBOZI SONGWE, NA ATOA MKONO WA POLE KWA FAMILIA YA DKT. KIGWANGWALLA


 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akisaini kitabu cha Maombolezo, Victoria Jijini Dar es salaam nyumbani kwa Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamis Kigwangala, kufuatia kifo cha Mtoto wake aitwaye Zul Hamis Kigwangala Kilichotokea Februari 21,2019 katika Hospitali ya Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (Muhimbili)  Jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akipeana mkono wa pole na Dkt. Bayoum Kigwangala ( Mke wa Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Kigwangala),  pamoja na Bi Hawa Mushi na Bi. Bagaile Bakari nyumbani kwa Waziri huyo Victoria Jijini Dar es salaam, kufuatia kifo cha Mtoto wake aitwaye Zul Hamis Kigwangala Kilichotokea Februari 21,2019 katika Hospitali ya Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (Muhimbili)  Jijini Dar es Salaam.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Watoto Hk Junior ,Sheila na Hawa ambao ni watoto wa Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamis Kigwangala alipoambata na mkewe Mama Janeth Magufuli kutoa pole kwa Familia ya Waziri huyo nyumbani kwake Victoria Jijini Dar es salaam, kufuatia kifo cha Mtoto wake aitwaye Zul Hamis Kigwangala Kilichotokea Februari 21,2019 katika Hospitali ya Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (Muhimbili)  Jijini Dar es Salaam.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika Dua maalum na mkewe Mama Janeth Magufuli ,Dkt. Bayoum Kigwangala (Mke wa Dkt. Kigwangala), Hk Junior , Sheila, Hawa (Watoto wa Waziri Kigwangwala) pamoja na Bi Hawa Mushi na Bi. Bagaile Bakari nyumbani kwa Waziri huyo Victoria Jijini Dar es salaam, kufuatia kifo cha Mtoto wake aitwaye Zul Hamis Kigwangala Kilichotokea Februari 21,2019 katika Hospitali ya Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (Muhimbili)  Jijini Dar es Salaam

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametuma salamu za rambirambi kwa familia zilizopoteza jamaa zao katika ajali            ya barabarani iliyotokea katika Wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe na kusababisha vifo vya watu 19.

Ajali hiyo imetokea jana tarehe 21 Februari, 2019 majira ya saa 3:15 usiku katika mteremko wa mlima Senjele ambapo lori (Semi-trailer) lililokuwa likisafiri kutoka Tunduma kwenda Mbeya Mjini lililigonga basi la abiria kwa nyuma, kisha basi hilo likaminywa katikati baada ya kuligonga lori jingine (Semi-trailer) lililokuwa mbele yake  na kusababisha vifo vya watu wote 18 waliokuwemo ndani ya basi pamoja na dereva    wa lori lililogonga basi la abiria.

Mhe. Rais Magufuli amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Mstaafu Nicodemas Elias Mwangela kufikisha salamu zake za pole kwa ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na vifo vya watu hao na amewaombea kwa Mwenyezi Mungu aziweke roho za Marehemu wote mahali pema peponi, Amina.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amezitaka mamlaka zinazohusika na usalama wa barabarani Mkoani Songwe kufanya uchunguzi wa ajali hiyo na kuchukua hatua zinazostahili pamoja na kujipanga vizuri kukabiliana na matukio ya ajali za barabarani.

Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli ametoa mkono wa pole kwa familia 
              ya Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla ambaye amefiwa na mwanae aitwaye Zul Hamis Kigwangalla jana tarehe 21 Februari, 2019 Jijini Dar es Salaam.

Mhe. Rais Magufuli akiwa na Mkewe Mhe. Mama Janeth Magufuli wamefika nyumbani kwa familia hiyo Mikocheni Jijini Dar es Salaam na kukutana na baadhi ya wanafamilia wakiongozwa na Mama wa Marehemu Dkt. Bayoum Kigwangalla wakiwa katika maandalizi ya kusafirisha mwili wa marehemu kwenda Nzega Mkoani Tabora.          

Dkt. Hamis Kigwangalla ameshatangulia Nzega ambako mazishi yatafanyika baadaye leo.
                      
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam

22 Februari, 2019

No comments: