Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi imewahukumu kifungo cha miaka mitatu jela washtakiwa wawili na mmoja kutumikia adhabu ya kifungo cha miaka miwili jela baada ya kukutwa na hatia ya kutorosha makontena bandarini.
Kesi hiyo ya uhujumu uchumi inahusiana uondoaji wa makontena 329 katika bandari kavu ya Azam (AICD) bila kulipiwa kodi.
Washtakiwa hao wamehukumiwa adhabu hiyo leo na Jaji Winfrida Korosso aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo baada ya kuwatia hatiani katika mashtaka 107 kati ya 110 yaliyokuwa yakiwakabili.
Waliohukumiwa adhabu hiyo ni Raymond Adolf Louis aliyekuwa meneja wa oparesheni za usalama na ulinzi Azam ICD, Khalid Yusuph Hassan na Benson Vitalis Malembo.
Louis na Hassan wamehukumiwa kifungo cha miaka mitatu kila mmoja kwa kila shtaka katika mashtaka 104 ya kughushi na kifungo cha miaka miwili kila mmoja katika shtaka moja la kuisababishia Mamlaka ya Mapato (TRA) hasara ya Sh12.5 bilioni.
Mbali na adhabu hiyo ya kifungo, pia Jaji Korosso ameamuru washtakiwa baada ya kumaliza kifungo chao kuilipa TRA fidia ya nusu ya hasara waliyoisababishia, yaani zaidi ya Sh6 bilioni wote kwa pamoja.
Malembo amehukumiwa kutumia adhabu ya miaka miwili jela baada ya kupatikana na hatia katika shtaka moja la kuisababishia TRA hasara hiyo ya Sh12.5 bilioni.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment