ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, March 9, 2019

MOI Yaendelea Kuimarisha Huduma za Kibingwa

Image result for moi muhimbili hospital
Na; Frank Mvungi- MAELEZO

Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) imetajwa kuendelea kuwa Kituo Bora cha huduma za Kibingwa ikiwemo upasuaji wa kuondoa vivimbe vya mishipa ya damu kwenye ubongo.

Akizungumza katika kipindi cha ’TUNATEKELEZA’ mkurugenzi mtendaji wa MOI Dkt. Respicius Boniface amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imejenga uwezo kwa Taasisi hiyo kuweza kutoa huduma za kibingwa zenye ubora wa viwango vya kimataifa.

" Serikali imenunua darubini ya kisasa ya kufanyia upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu na kuongeza vyumba vya kufanyia upasuaji kutoka 6 hadi 9 na kununua vitanda 9 vya kufanyia upasuaji " Alisisitiza Dkt. Boniface

Akifafanua amesema kuwa Serikali imewezesha Taasisi hiyo kupata mashine mpya za uchunguzi za MRI, CT Scan, Ultrasound, X-Ray za kidijitali na X- Ray zinazohamishika na X- Ray za kawaida.

Aliongeza kuwa katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Tano vitanda katika Taasisi hiyo vimeongezeka kutoka 150 hadi 340 ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali kuimarisha huduma za afya kuanzia ngazi ya chini hadi zile za kibingwa.

Akizungumazia huduma mpya zinazotokana na uboreshaji uliofanywa na Serikali Dkt. Boniface amesema kuwa ni pamoja na ; kuanzisha huduma ya upasuaji wa magoti kwa njia ya matundu, upasuaji wa kunyoosha kibiongo, upasuaji wa mgongo kwa kufungua eneo dogo,kuanzishwa kwa wodi ya kulazwa na kufanyiwa upasuaji siku hiyo hiyo.

" Vitanda vya wagonjwa walio katika uangalizi maalum vimeongezeka kutoka 8 hadi 32 na pia tumeanzisha kitengo cha wagonjwa wa dharura" Alisisitiza Dkt. Boniface

Kipindi cha 'TUNATEKELEZA ' kinaratibiwa na Idara ya Habari (MAELEZO) na kinawashirikisha viongozi mbalimbali wa Serikali wakiwemo watendaji wakuu wa Taasisi za Serikali, Mawaziri, Wakuu wa Mikoa na Idara zinazojitegemea.

No comments: