ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, March 23, 2019

Wafungwa Gereza Songwe Walima Ekari 750 za Mahindi

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (kulia), akielekea kukagua mahindi yanayolimwa na wafungwa katika Gereza la Kilimo Songwe kwa ajili ya chakula cha wafungwa nchini. Kushoto ni Mkuu wa Gereza hilo, Mrakibu Mwandamizi, Peter Anatory. Ziara hiyo imefanyika leo jijini Mbeya.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni , akizungumza na Mkuu wa Gereza la Kilimo Songwe, Mrakibu Mwandamizi, Peter Anatory (kushoto) wakati wa ziara ya kukagua shamba katika gereza hilo kwa ajili ya chakula cha wafungwa nchini. Ziara hiyo imefanyika leo jijini Mbeya.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi



Jumla ya ekari 750 za mahindi zimelimwa katika Gereza la Kilimo Songwe ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Dkt. John Magufuli la kutaka magereza yatumike kwa shughuli za uzalishaji ikiwemo kilimo kwa kutumia nguvu kazi ya wafungwa waliopo magerezani.

Akisoma taarifa mbele ya Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, Mkuu wa Gereza hilo ,Mrakibu Mwandamizi, Peter Anatory alisema kwa kutumia nguvu kazi ya wafungwa jumla ya ekari 750 za mahindi zimelimwa ikiwa ni kwa matumizi ya chakula kwa wafungwa ambapo wanatarajia kulisha na magereza mengine.

“Tunaendelea vizuri na kilimo na kama maelekezo ya Mheshimiwa Rais yalivyotufikia ni kweli tunatumia wafungwa ambao tumewapangia zamu katika shughuli hizi za kilimo,tunategemea kulisha magereza saba baada ya mavuno huku jumla ya ekari 750 zimelimwa mahindi hapa” alisema SSP Anatory

Pia aliitaka serikali kuwasaidia kutatua changamoto ya zana za kilimo ikiwepo matrekta ili kukamilisha ekari 250 zilizobaki ili kuweza kukamilisha ekari 1000 zilizopo katika gereza hilo.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, alisema Gereza la Songwe ni moja kati ya magereza kumi nchini yaliyoteuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano kuendeleza kilimo cha mkakati lengo ni kuwezesha magereza yote nchini kuzalisha vyakula kwa ajili ya kulisha wafungwa na mazao yanayoweza kuwaletea kipato badala ya kutegemea ruzuku kutoka serikalini.

“Agizo la Rais Dkt.Magufuli ni kuona magereza yanajitosheleza kwa chakula kupitia wafungwa, nawapongeza kwa ekari mlizolima mahindi na kama wizara tunaahidi kulishughulikia suala la zana za kilimo ikiwemo matrekta, na gereza lenu ni moja kati ya magereza kumi ya kimkakati na mnaendelea vizuri” alisema Masauni

Mbali ya kilimo Gereza la Songwe pia linajishughulisha na ufugaji wa ng’ombe, mbuzi, kondoo, kuku, sungura na simbilisi.

No comments: