ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, March 16, 2019

WAKUU WA IDARA ZA ARDHI WATAKAOKALIA HATI ZA ARDHI OFISINI SASA KUKIONA


 Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na wananchi wa Mji wa Mtukula wilayani Misenyi mkoa wa Kagera wakati akiwa katika ziara yake ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya Serikali kupitia sekta ya ardhi.
 Sehemu ya wananchi wa Mji wa Mtukula wilaya ya Misenyi mkoa wa Kagera wakimsikiliza Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (hayupo pichani) wakati akiwa katika ziara ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia sekta ya ardhi.
 Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na watendaji wa sekta ya ardhi katika halmashauri ya wilaya ya Misenyi mkoa wa Kagera wakati akiwa katika ziara yake ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya Serikali kupitia sekta ya ardhi.
  Sehemu ya wananchi wa Mji wa Kyaka wilaya ya Misenyi mkoa wa Kagera wakimsikiliza Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (hayupo pichani) wakati akiwa katika ziara ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia sekta ya ardhi.
 Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiangalia moja ya majalada ya ardhi aliyoyakuta katika ofisi ya halmashauri ya Misenyi mkoa wa Kagera wakati akiwa katika ziara yake ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya Serikali kupitia sekta ya ardhi. Kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Misenyi Kanali Denis Mwila na wa pili kushoto ni Kaimu Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Ziwa Elia Kamyanda na kulia ni Kaimu Mkuu wa Idara ya Ardhi Misenyi Emanuel Samson.

Na Munir Shemweta, MISENYI
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amesema kuanzia sasa Mkuu wa Idara ya Ardhi atakayekutwa amekaa na hati ya ardhi kwa muda mrefu   bila kuipeleka ofisi ya Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda kwa ajili ya kukamilisha taratibu za utolewaji hati hiyo basi Mkuu huyo ataondolewa katika nafasi yake.

Dkt Mabula alisema hayo jana tarehe 15 Machi 2019 alipozungumza na watendaji wa sekta ya ardhi katika halmashauri ya wilaya ya Misenyi mkoani Kagera akiwa katika ziara yake ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia sekta ya ardhi.

Kauli hiyo ya Dkt Mabula inafuatia kukuta baadhi ya hati katika halmashauri ya wilaya ya Misenyi zikiwa kwenye masijala ya ardhi tangu mwaka 2017 bila kupelekwa ofisi ya Kamishna wa Ardhi Kanda ya Ziwa kwa ajili ya kukamilishwa ili wahusika wapatiwe hati.

Alisema, baadhi ya halmashauri alizozitembelea wakati wa ziara yake ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia sekta ya ardhi amebaini wakuu wengi wa idara ya ardhi wakiwa na hati kwenye ofisi zao kwa muda mrefu bila kufanya jitihada zozote za kuhakikisha hati hizo zinaenda ofisi ya Kamishna kwa ajili ya kukamilishwa ili wahusika wapatiwe hati.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Ardhi, ucheleweshaji utoaji hati miliki za viwanja na mashamba siyo tu unawakera wananchi bali unaikosesha serikali mapato ya kodi ya ardhi kwa kuwa wananchi wanakuwa hawajamilikishwa ardhi kwa mujibu wa sheria.

Dkt. Mabula ametoa onyo kali kwa Mkuu wa idara ya ardhi halmashauri ya wilaya ya Misenyi mkoani Kagera kwa kukaa na hati kwa zaidi ya miaka miwili kwenye ofisi yake bila kuwasilisha  hati hizo ofisi ya Kamishna Msaidizi Kanda ya Ziwa kwa ajili ya kukamilishwa na hatimaye kukabidhiwa kwa wahusika  kwa haraka na wakati.

Katika hatua nyingine Dkt Mabula amewataka wananchi wa miji ya Kyaka na Mtukula katika wilaya ya Misenyi mkoa wa Kagera kuchangamkia zoezi la urasimishaji makazi holela ambalo limeonekana kusuasua katika miji hiyo.

Akizungumza na wakazi wa Kyaka na Mtukula kwa nyakati tofauti Dkt Mabula alisema kuwa, haridhishwi kabisa na namna kasi ya urasimishaji inavyoendelea katika miji hiyo ambapo takwimu zinaonesha wananchi waliojitokeza kwenye zoezi hilo ni ndogo ukilinganisha na wakazi wa miji hiyo.

Dkt Mabula ametolea mfano wa Mji wa Mtukula katika kitongoji cha Katede kuwa, pamoja na eneo hilo kuwa na Kaya 842 zenye wakazi zaidi ya 3000 lakini ni watu 13 tu waliolipia fedha za kurasimishiwa maeneo yao na watu hao wamechangia jumla ya shilingi milioni moja na laki nane.

Aidha, Naibu Waziri Mabula amewataka wananchi wa miji ya Kyaka na Mtukula kutofanya maendelezo katika eneo lolote ambalo hawajajua mipango yake ili kuepuka kubomolewa na kupoteza haki zao kwa kujenga katika maeneo yasiyo ruhusiwa ambapo ameitaka halmashauri ya wilaya ya Misenyi kupanga mpango wa matumizi bora ya ardhi kwa lengo la kuwa na miji iliyopangika.

No comments: