Monday, March 11, 2019

ZAHERA, MANJI ARUDI YANGA KAMA NANI ?

Image result for mwinyi zahera
Kocha Mkuu wa klabu ya Yanga Mwinyi Zahera ameripotiwa na gazeti moja la michezo akieleza kuwa aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo Yusuph Mehbub Manji ana uwezekano mkubwa wa kurejea klabuni hapo.

Habari hii ilipokelewa vema na wanayanga wengi hasa kutokana na kuwa kipindi hiki Yanga inaonekana kuyumba kiuchumi huku ikitegemea zaidi nguvu ya michango ya wanachama, wapenzi na washabiki wake ili kumudu gharama mbalimbali za uendeshaji wa klabu hiyo.

Wakati huu Yanga ikielekea kufanya uchaguzi wake tarehe 23/03/2019 kuna swali la kujiuliza katika hili la Manji kurudi Yanga.

"Manji anarudi kama nani?"

Hili ndiyo swali la msingi ambalo wanayanga wengi wanapaswa kujiuliza.

Ili kuweza kujibu swali hili ni vema kwanza tumfahamu Yusuph Manji mwenyewe ni nani?

Yusuph Manji ni mfanyabiashara. Mfanyabiashara yeyote hulitazama jambo lolote lile kibiashara.

Hivyo hata hii Yanga Manji anaitazama kibiashara.

Binafsi nilifikiria sana kuhusu kusuasua kwa Manji kurejea Yanga hata pale ilipoelezwa kuwa angerejea ofisini mwezi January mwaka huu.

Kwa nini nilijawa na fikira?

Ni kwa sababu Manji ni mfanyabiashara.

Manji anafahamu kabisa kuwa muda si mrefu Yanga itaelekea kwenye mabadiliko kama walivyofanya klabu ya Simba ingawa mfumo wao unaweza kuwa tofauti na ule wa Simba.

Kutokana na hili Manji alihofu kitu kuhusu kuwa Mwenyekiti wa klabu ya Yanga.

Kitu gani hicho?

Hebu tujikumbushe.

Tangazo la tarehe 12 mwezi April mwaka 2016 lililochapwa na gazeti la "The Citizen" lilimnukuu Yusuph Manji akitangaza kung'atuka nafasi zote za utendaji ndani ya Quality Group.

Kwa ufupi alijitoa katika nafasi zote za kiutendaji ndani ya Quality Group ili kubaki kama mshauri na mmoja wa wamiliki wa kampuni hizo za Quality.

Je ni kwa nini Manji alijiuzuru nafasi hizo zote muhimu Quality Group?

Jibu ni hili: Manji aliogopa kuingia kwenye Ethical Dilemma

Tukumbuke kuwa Manji alishinda kiti cha udiwani Kata ya Mbagala Kuu mwaka 2015 hivyo kutokana na nafasi yake aliona ni busara kujiweka kando na masuala ya Quality Group ili asilete mgongano wa maslahi ama Conflict of Interest kwa Kingereza.

Internal Revenue Service (IRS) ya Marekani ilitoa tafsiri ya Conflict of interest ambayo ilinukuliwa na Agard katika kitabu chake Leadership in nonprofit Organizations kwa kueleza:

'Conflict of interest is a situation where "a person in a position of authority over an organization such as director,officer, or manager, may benefit personally from a decision he or she make.'

(IRS, 2006:9) (Agard, 2011:370).

Kwa tafsiri ya kwangu ya Kiswahili ni kuwa:

"Mgongano wa maslahi ni hali ambayo hutokea wakati mtu aliye kwenye nafasi ya mamlaka juu ya taasisi kama vile mkurugenzi, afisa au meneja anaweza kunufaika binafsi kutokana na maamuzi anayofanya."

Ledlow na Coppola katika kitabu chao Leadership for Health Professionals. Theory, Skills and Application walikazia tafsiri ya IRS kwa kueleza:

"Conflict of interest occurs when a person has conflicting duties or responsibilities and meeting one of them makes it impossible to meet the other. The classic example occurs when a decision maker for one organization is also a decision maker or influencer for another organization with which business is transacted."
(Ledlow & Coppola, 2010:246).

Kwa tafsiri yangu ya Kiswahili:

"Mgongano wa maslahi hutokea wakati ambapo mtu ana majukumu ama wajibu unaogongana na kulifikia mojawapo hufanya hali kuwa ngumu kulifikia lingine. Mfano mzuri hali hii hutokea wakati mtu mwenye maamuzi kwa taasisi moja pia ni mwenye maamuzi ama mwenye ushawishi kwa taasisi nyingine ambayo inafanya biashara na kampuni ya kwanza ambayo pia ana maamuzi."

Kama ukitazama kwa kina utagundua kuwa Yusuph Manji alikataa majukumu ya Udiwani yasingiliane na ya utendaji wake katika Quality Group katika masuala ya tenda mbalimbali za Kata n.k hivyo aliona ni busara ajiweke kando Quality.

Ninaamini kabisa ni busara hii ndiyo iliyomuongoza Manji kukataa kurejea Yanga kama Mwenyekiti kwani kuna kitu anakitaka ndani ya Yanga.

Ni kitu gani Manji anakitaka ndani ya Yanga?

Kama nilivyokwisha kueleza awali kuwa Manji ni mfanyabiashara.

Mfanyabiashara yeyote hutafuta fursa, Yanga ni fursa kubwa kibiashara. Hivyo licha ya mapenzi yake kwa klabu hii lakini piano bado nae anahitaji kunufaika kibiashara kama ilivyo mwa mwenzake MO Dewji wa Simba.

Tukumbuke kuwa MO aliwahi kuwekeza Singida United akafeli.

Akawezeka African Lyon ambayo nadhani alijaribu kuunganisha majina mawili ya vilabu vyetu vikubwa Yanga na Simba kwa kuchukua Africans kupata African na kubadili Simba kuita Lyon likiwa na maana ya Simba kwa Kingereza cha zamani ili kupata mchanyato wa majina mawili na kuleta ushawishi miongoni mwa washabiki wengi wa soka Tanzania, lakini nako akafeli akaamua kuiuza.

Tujiulize klabu kama Azam licha ya kuwa inamilikiwa na tajiri mkubwa nchini lakini bado haijamnufaisha mmiliki wa klabu hiyo kama ambavyo alitarajia labda,je tatizo ni nini?

Hapa tunakuja kugundua kuwa Azam inakosa watu kwa maana ya wapenzi na washabiki kama zilivyo Simba na Yanga.

Hawa wapenzi na washabiki ndiyo consumers au walaji wa bidhaa ambazo wamiliki wa klabu kama Azam wanawahitaji kwa bahati mbaya hawana.

Sasa Manji anaitazama Yanga kwa jicho hili, jicho la kuona fursa kubwa kutokana na kuwa na fan base kubwa huenda kuliko klabu yoyote nchini Tanzania.

Kama Manji anaitazama hivi Yanga, wewe mwanayanga unaetaka Manji awe Mwenyeiti unadhani Manji anaweza kukuelewa wakati yeye anajua kabisa akiwa Mwenyekiti atakutana na *Ethical Dilemma kwenye mambo fulani yahusuyo Yanga ambayo nae kama mshauri wa Quality Group ana wajibu wa kushauri?

Manji alikwepa mtego huu mapema,kwa bahati mbaya wanayanga wengi hawakujua lengo lake.

MANJI ANATAKA NINI YANGA?

Yusuph Manji anachotaka Yanga ni kuwekeza. Hiki ndicho anachotaka, si uenyekiti. Yeye anataka kuwa mwekezaji, uenyekiti si kipaumbele kwake.

Lakini je anawekezaje Yanga katika mazingira haya?

Ni wazi kuwa ni ngumu sana kwa Manji kuwekeza Yanga katika mazingira haya ambayo kuna mianya mingi sana ya ufujaji pesa na watu kujinufaisha wao.

Tazama biashara ya jezi Yanga. Yanga kwa sasa ndiyo klabu yenye jezi nyingi mno, lakini tujiulize inanufaika vipi kutokana na mauzo ya jezi hizo? Jibu ni hainufaiki hata kidogo!

Yanga inadaiwa kujawa na vijana wa mjini wengi wakati huu ambao wanaonekana kunufaika na kutokuwa na uongozi kamili katika klabu hii na wanatamani hali hii iendelee ili wanufaike zaidi.

Aliyewahi kuwa Katibu Mkuu Charles Boniface Mkwasa aliwahi kuja na mfumo wa uchangiaji ambao sasa umeshika kasi lakini ukafeli, je nini kilifelisha? Je waliofelisha mfumo ule hawapo? Kama bado wapo tunadhani Manji atarudi?

NINI KIFANYIKE ILI MANJI ARUDI?

Ni lazima ufanyike uchaguzi, uchaguzi huu wa tarehe 23/03/2019 ndiyo utakaomrejesha Manji Yanga na atakuwa anaufuatilia kwa makini sana.

Kuna vitu anatamani vitokee ili arudi Yanga kama muwekezaji.

Ili kujua vitu gani Manji anatamani vitokee hebu tujifunze kutoka China.

Ni nani kati yetu anamfahamu Deng Xiaoping?

Basi tufahamu kuwa Manji anamuhitaji Deng Xiaoping Yanga ili aje kuwekeza.

Deng Xiaoping ni nani?

Deng Xiaoping alikuwa mwanamapinduzi wa kiuchumi wa China aliyeingia madarakani kuanzia mwaka 1978 mpaka mwaka 1989 miaka miwili baada ya kufariki kwa muasisi wa taifa la China Mao Zedong tarehe 19 February, 1976.

China unayoiona leo ni matokeo ya Mapinduzi ya Kiuchumi aliyofanya Deng Xiaoping ndani ya kipindi cha utawala wake mpaka kufariki kwake mwaka 1997.

Garnaut na wenzake katika kitabu chao "China's 40 Years of Reform and Development 1978-2018" walieleza vema namna gani Deng Xiaoping aliibadili China kwa kueleza:

"China initiated the change from central planning to market exchange simultaneously with opening up to international trade and investment. Domestic economic development and participation in economic globalization have marched forward hand in hand." (Garnaut et al, 2018:5)

Waliendelea kusema:

"Deng Xiaoping was a source of , sponsor within the party for and for two decades the protector of China's reform and opening up policy." (Garnaut et al, 2028:6)

Kwa tafsiri ya jumla hapa tunaona kuwa Deng Xiaoping ndiye alikuwa msingi wa China hii tunayoiona sasa ikiisumbua Marekani na kutowapa usingizi viongozi wake kama anavyoteseka Trump hivi sasa.

Deng Xiaoping ndiye alikuwa chanzo, mfadhili na mlinzi wa mabadiliko makubwa ya kiuchumi ndani ya China. Yanga inamuhitaji Deng Xiaoping.

Maelezo ya Garnaut na wenzake yaliwahi kusemwa pia na Raphael Shen katika kitabu chake China's Economic Reform: An Experiment in Pragmatic Socialism:

"Deng Xiaoping succeeded Mao as China's paramount leader in 1976, and from 1978 to 1998 Deng helped engineer the dismantling of Mao's bureaucratic legacies via policies of economic decentralization and liberalization. Deng also promoted China's image as a participant in world affairs."

Hapa tunaona kuwa hata Yanga inahitaji mtu aina ya Deng Xiaoping. Mtu atakayeweza kuvunja ile mianya ya watu kutumia mgongo wa klabu kujinufaisha, mtu atakayefanya Yanga iwe na uwekezaji na wawekezajai mbalimbali kuanzia usafiri, vyakula, malazi, vifaa vya mazoezi, vinywaji na hata jezi na mavazi ya kawaida na vitu vidogo vidogo.

Yanga inahitaji mtu atakayekuwa na ujasiri wa kukemea utovu wa nidhamu kwa wachezaji ambaye ataendana na mwenendo na tabia za kocha Mwinyi Zahera, na awe mtu mwenye vision ya kuifanya Yanga kuwa klabu inayojiendeshwa kibiashara huku ikitambua mchango wa wapenzi, wanachama na washabiki kwani ndiyo walaji wa bidhaa za klabu.

Kiufupi Yanga inamuhitaji Deng Xiaoping wake kama ambavyo China ilimpata Deng Xiaoping mwanauchumi wa mrengo wa Marx (Marxism) ambaye alikwenda Ufaransa akiwa na umri wa miaka 16 tu kwa lengo la kusoma Industrial Skills na hatimaye kupata ujuzi wa viwanda vya chuma, magari Renault, kuchoma vyuma na uhudumu wa jikoni mtu ambaye anautazama mpira kama biashara kama ambavyo Daniel Barthold alipata kueleza kuhusu soka la Ulaya katika kitabu chake The Business of European Football aliposema:

"The reason for the change of European football is diverse but the core of the change needs to be found in the business of soccer." (Barthold, 2009:3)
Kwa msingi huo Yanga inamuhitaji mtu mwenye weledi wa biashara ya soka na usimamizi wake na hiki ndicho anachohitaji Yusuph Manji ili arudi Yanga kuwekeza.

Asanteni:

Abbas Mwalimu

Mchambuzi: Masuala ya Siasa, Kimataifa na Diplomasia.

+255 719 258 484

No comments: