Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof. Idris Kikula wa pili kushoto akiwa katika eneo la wachimbaji wadogo Ipanko wilayani Ulanga akipata maelezo kutoka kwa Kaimu Afisa Madini Mkazi Morogoro Mhandisi Emmanuel Shija alipotembelea kujionea namna shuguli za uchimbaji zinavyofanyika. Wa kwanza kushoto ni Kamishna wa Tume hiyo Dkt. Athanas Macheyeki.
Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof. Idris Kikula akijibu maswali mbalimbali ya waandishi wa habari kwenye eneo la mgodi wa wachimbaji wadogo Ipanko.
Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof. Idris Kikula akionyesha jambo kwenye ramani ya mwekezaji wa Madini ya Graphite; TanzGraphite (T) Ltd. Wa tatu kushoto ni Meneja Uhusiano wa Jamii Bernad Mihayo, wa pili kushoto ni Kamishna wa Tume hiyo Dkt. Athanas Macheyeki.
Kamishna wa Tume ya Madini Dkt. Athanas Macheyeki kushoto akizungumza jambo na Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof. Idris Kikula mara baada ya kuzunguka na kukagua eneo la wachimbaji lililopo Iponka eneo ambalo awali lilifungiwa kufanya shuguli za uchimbaji.
Wachimbaji wadogo wakiwa chini ya mgodi katika shimo lenye urefu wa zaidi ya mita hamsini wakiwa wanaendelea na shuguli za uchimbaji katika eneo la Ipanko.
Na Issa Mtuwa- Ulanga Morogoro
Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof. Idris Kikula amewataka Watumishi wa tume hiyo ofisi ya Morogoro na Ulanga kutambua kwamba agizo la Waziri linalowataka kufuta leseni zisizofuata utaratibu wa kisheria sio la kujadili bali ni kutekeleza. Prof. Kikula ameyasema hayo Aprili 10, 2019 wilayani Ulanga wakati akizungumza na watumishi wa tume hiyo wakati wa ziara yake.
Taarifa iliyosomwa kwake na Afisa Migodi Mkazi ofisi ya Mahenge Ulanga, Tandu Jilabi inaonyesha kuwa wilaya ya Ulanga ina leseni za wachimbaji wadogo 221 kati ya hizo ni leseni 9 tu ndio zinazofanya kazi huku leseni za uchimbaji wa kati zikiwa 5 na leseni za utafiti wa madini 13.
Kufuatia hali hiyo, Afisa Migodi Mkazi ofisi ya Mahenge ameiomba tume ya madini kufuta leseni zisizofanya kazi ili wapewe wenye uhitaji ili waweze kuziendeleza. Kufuatia ombi hilo, Mwenyekiti wa tume amesema jukumu la kuzifuta leseni hizo ni la kwake pamoja na Afisa Madini Mkazi Morogoro na halina mjadala kwakuwa muongozo wa utekeleza wa suala hilo ulishatolewa na waziri wa Madini.
“Suala la leseni zisizofanya kazi sio la kujadili, hili ni agizo la Waziri na kazi yetu ni kutekeleza na wenye kuzifuta ni ninyi, fuateni taratibu uliowekwa kwa mujibu wa sheria katika kuzifuta na sio kuzifuta lazima wote waliozishikilia leseni hizo kwa muda wote walipe fidia na wasipo fanya hivyo taratibu za kisheria zifuatwe kwani katika kipindi hicho chote serikali imekosa mapato yake. Kuanzia leo pitieni leseni zote na ifikapo Juni 30 mwaka huu leseni zote zisizo hai ziwe zimefutwa”, amesema Prof. Kikula.
Wakati huo huo, mwenyekiti wa tume amekutana na kuzungumza mwakilishi wa mwekezaji wa kampuni ya TanzGraphite (T) Ltd ambae ni Meneja Uhusiano wa Jamii na kuzungumzia kuhusu mgogoro uliopo baina ya mwekezaji huyo na baadhi ya wananchi wanaotakiwa kufanyiwa tathimini ili kupisha shuguli za uchimbaji wa madini katika eneo hilo. Prof. Kikula ameonyesha kusikitishwa na mgogoro huo ambao amesema ni wa muda mrefu sasa na unachelewesha maendeleo ya watu na kuikosesha serikali mapato.
Ameongeza kimsingi wananchi wanapaswa kuelewa kuwa “right surface” (haki ya kumiliki vitu vilivyo juu ya ardhi) inampa mwananchi haki ya kulipwa fidia ya mali zilizo juu ya ardhi anayo miliki lakini watambue kuwa kuna “resource right” (haki ya kumiliki raslimali zilizo chini ya ardhi) ikiwemo madini ambayo mmiliki wake ni serikali, ndio maana inapohitaji raslimali hizo humuondoa na kumfidia mliliki wa mali za juu ya ardhi, hivyo wananchi wanapo ng’ang’ania wanatakiwa walitambue hilo.
Pia, amesema kuwa, kwa mpango ulioanishwa na mwekezaji huyo unaonyesha manufaa kwa wananchi kupitia miradi ya maendeleo (CSR) ambapo amebainisha kuwa mwekezaji ameahidi kuwalipa fidia, kuwajengea nyumba za kisasa wale wote walio ndani ya eneo. Mambo mengine ni pamoja na kuwapatia chakula kwa muda wa miaka miwili wakiwa kwenye makazi mapya watakayo jengewa na kila kaya kusomesha mtoto mmoja kwenye vyuo vya veta na wakihitimu wataajiriwa na mgodi ili waweze kupata kipato cha kusaidia na kuendeleza kaya zao.
Pamoja na hayo, mwekezaji huyo amemweleza mwenyekiti wa tume kuwa tayari wameshakubaliana kujengaa kituo cha afya, matundu ya vyoo kwa baadhi ya shule, kujenga shule na ukarabati wa vyumba vya madarasa katika shule mbalimbali. Hata hivyo hakusita kuonyesha kusikitishwa kwake na watu wachache wanaogoma kuondoka kupisha shuguli za uchimbaji huku kila kitu ikiwemo mtaji wa shuguli hizo ukiwa tayari.
Katika mgogoro huo, kaya 347 zinatakiwa kuondoka kupisha mwekezaji huyo na kati ya hizo kaya 62 ndio zinazo goma kuondoka ili mwekezaji aanze kazi ya uchimbaji. Mwenyekiti amesikitishwa na hali hiyo na na kuuomba uongozi wa mkoa na wilaya kuzungumza na kaya hizo sambamba na Baba Askofu aliyeko ndani ya eneo hilo ili mradi huo uanze kwani ni wa muda mrefu na serikali inakosa mapato.
Amesema kwa sasa anaziachia juhudi za serikali ya mkoa na wilaya katika kuupatia ufumbuzi mgogoro huo. Mapema mwenyekiti alikutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Wilaya ya Ulanga Ngolo Malenya ambapo amemshukuru kwa ushirikiano anao utoa kwa viongozi na wafanyakazi wa tume ya madini wilaya ya Ulanga.
Amesisitiza suala la uadilifu kwa wafanyakazi wa tume na amesema hilo litakuwa jambo la kwanza kulisema kila aendapo sambamba na ukusanyaji wa maduhuli ya serikali. Aidha, amesema kipimo kikubwa cha kila mkuu wa kituo cha tume ya madini kitakuwa ni ukusanyaji wa maduhuli ambapo katika Mwaka wa Fedha 2018/2019 tume ilipangiwa kukusanya Bilioni 310 na mwaka wa fedha ujao tume imepangiwa kukusanya Bilioni 467.
Upande wake, Kamishna wa tume hiyo Dkt. Athanas Macheyeki amewakumbusha na kuwasisitiza watumishi wa tume na wachimbaji wa madini kuhakikisha wanasimamia ukusanyaji na ulipaji wa tozo na stahiki zote za serikali kwa wakati. Amesema kwa kufanya hivyo raslimali za madini zitakuwa na tija kwa taifa kama anavyo sisitiza Rais John Pombe Magufuli kuwa anataka raslimali za madini ziwanufaishe watanzania wote na namna za kuwanufaisha ni kulipa stahiki za serikali zinazo tokana na madini ili zikatumike kujenga uchumi wa taifa.
Prof. Kikula na Dkt. Macheyeki wanaendelea na ziara yao mkoani Morogoro kukagua shuguli za Tume katika Wilaya mbalimbali ambapo leo walitembelea eneo la wachimbaaji wadogo ipanko wilayani ulanga.
No comments:
Post a Comment