ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, April 11, 2019

MHE. MKUCHIKA AWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA WA FEDHA 2019/20

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt (Mst) Mhe. George H. Mkuchika (Mb) akiwasilisha Bungeni Makadirio ya Matumizi ya Fedha kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora pamoja na Taasisi zilizo chini yake.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt (Mst) Mhe. George H. Mkuchika (Mb) amewasilisha Bungeni Makadirio ya Matumizi ya Fedha kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na kuwataka Waajiri katika Taasisi za Umma nchini kuwawezesha Watumishi wa Umma wanaoajiriwa kwa mara ya kwanza kupata mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji katika Chuo cha Utumishi wa Umma ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi.

Mhe. Mkuchika amesema kuwa, watumishi wengi hawajui taratibu za kiutumishi hivyo kukosa uwezo wa kutekeleza majukumu yao kikamilifu.

Mhe. Mkuchika amesisitiza kuwa, pamoja na majukumu mengine, Chuo cha Utumishi wa Umma kina jukumu la kuwajengea uwezo Watumishi wa Umma ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi na kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya Utumishi wa Umma iliyopo, hivyo ni vema watumishi hao wakapata mafunzo katika chuo hicho.

Ameongeza kuwa, kuanzia sasa atafanya ufuatiliaji wa karibu ili kuhakikisha waajiri wote wanawapeleka watumishi wa umma wote wanaoajiriwa kwa mara ya kwanza katika Chuo hicho kupata mafunzo stahiki.

Mhe. Mkuchika ameliomba Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuidhinisha jumla ya kiasi cha shilingi 683, 529,221,617 kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora pamoja na Taasisi zilizo chini yake.

IMETOLEWA NA:
KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI
OFISI YA RAIS (UTUMISHI)

TAREHE 10 APRILI, 2019

No comments: