Advertisements

Wednesday, April 17, 2019

Anzia kwa Mjumbe wa Nyumba Kumi Ndiye mwenye Wananchi


Faida ya kuwa na wajumbe wa nyumba kumi ni nyingi ikiwamo ukusanyaji wa taarifa na data ulikuwa rahisi, usalama wa raia na mali zake ulikuwa wa kuaminika, jamii pia ilikuwa imeshikamana na kuaminiana.

Suala la ulinzi na usalama lilianzia nyumba kumi kwa vile lilikuwa ni rahisi na salama kwa wananchi na vyombo vya ulinzi na usalama kubaini matendo yote ya kihalifu na lilikuwa jukumu la kila raia kumlinda mwenzake na kutoa taarifa kwa mjumbe kama kulikuwa na tatizo.

Bahati mbaya, ulipoanzishwa mfumo wa vyama vingi wajumbe hao waliokuwa wanafanya kazi za serikali na chama kwa wakati mmoja, wakabaki upande wa chama kwa ajili ya manufaa ya kisiasa.

Kutokana na hali hiyo, kumekuwa na matukio ya ajabu na ya kuogopesha ya kihalifu yanayotia hofu taifa letu.

Matukio hayo ni ya watoto kupotea katika mazingira tatanishi, watu kutekwa, ubakaji, udhalilishaji watoto yanazidi kutia wasiwasi.

Kwa mwelekeo wa matukio haya hata Baba wa Taifa aliyeanzisha mfumo wa ulinzi hadi ngazi za chini kabisa angekuwepo sijui angechukuliaje?

Kinachoogopesha zaidi hata watu maarufu wameanza kutekwa kama ilivyotokewa kwa Mohamed Dewji ambaye alitekwa na kupatikana baada ya siku tisa jijini Dar es Salaam.

Unaweza kujiuliza, kama hali ipo hivyo kwa watu maarufu ambao wanapotea au kutekwa, vipi hali ya wananchi huku chini ambao ni wa kawaida?

Wananchi wanajiuliza haya mambo yanatokea wapi? Mbona awali hayakuwapo na hata kama yalikuwapo mbona hayakushika kasi namna hii? Ina maana watekaji kwa sasa wana uwezo kuliko vyombo ulinzi na usalama?

Licha ya jitihada mbalimbali zinazooneshwa na jeshi letu la polisi kuhakikisha wanatokomeza masuala ya utekaji na kupotea kwa watu kusikojulikana, ni wakati sasa Serikali kuwashirikisha wananchi kwa kufufua mifumo iliyokuwapo awali ukiwamo wa wajumbe wa nyumba kumi.

Japo mifumo hiyo bado ipo kwenye baadhi ya maeneo kwa jina tu, ni vizuri wajumbe wa nyumba kumi wawepo nma watambuliwe kupitia serikali za mitaa badala ya kuwa chini ya chama cha siasa.






















Turudi enzi hizo ambazo babu na wazazi wetu walilindana na matukio ya kihalifu kuyasikia ilikuwa kazi. Enzi hizo mtoto wa mwenzio alikuwa wa kwako, si kizazi hiki ambacho kila mtu anakwenda kivyake.

No comments: