Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (katikati) akiongoza kikao cha maandalizi cha Ujumbe wa Tanzania kwenye Mikutano ya Kipupwe ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF, kwenye Ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini Marekani, kushoto kwake ni Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Balozi Wilson Masilingi na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Prof. Florens Luoga, kulia kwake ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Bw. Khamis Mussa Omar na Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Dkt. Yamungu Kayandabila.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kushoto) akiteta jambo na Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Balozi Wilson Masilingi wakati wa kikao cha maandalizi cha Ujumbe wa Tanzania kwenye Mikutano ya Kipupwe ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF, kilichofanyika kwenye Ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini Marekani, Mjini Washington DC.
Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Balozi Wilson Masilingi, akizungumza jambo wakati wa kikao cha maandalizi cha Ujumbe wa Tanzania kwenye Mikutano ya Kipupwe ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF, kilichofanyika kwenye Ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini Marekani, Mjini Washington DC.
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Prof. Florens Luoga, akiwa katika kikao cha maandalizi cha Ujumbe wa Tanzania kwenye Mikutano ya Kipupwe ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF, kilichofanyika kwenye Ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini Marekani, Mjini Washington DC.
Na Benny Mwaipaja, Washington DC
WAZIRI wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango, ameongoza ujumbe wa Tanzania kwenye mikutano ya kipupwe(Spring Meetings) ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) inayofanyika mjini Washington DC, Marekani.
Akizungumza kwenye Ofisi za Ubalozi wa Tanzania Mjini Washigton DC, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, amesema kuwa ujumbe wa Tanzania unaojumuisha pia wajumbe kutoka Serikali ya Mapinduzi-Zanzibar, utasimamia maslahi ya pande zote mbili za Muungano.
Mikutano hiyo inatoa fursa kwa Mawaziri wa Fedha na Magavana wa Benki Kuu kutoka katika nchi wanachama ambao pia mi Magavana wa Benki ya Dunia na IMF, kujadili maendeleo na changamoto mbalimbali zilizojitokeza katika utekelezaji wa masuala mbalimbali ya maendeleo na ushirikiano.
Aidha Mikutano hiyo hutoa fursa kwa nchi kushiriki kama mwanahisa kwenye mikutano ya kiutawala (Board of Governors) ya Taasisi hizo mbili ambapo maamuzi ya kiuendeshaji na kisera hufanyika
Tanzania itapata fursa ya kushiriki kwenye Kamati Maalum za Benki ya Dunia na IMF na baadhi ya mikutano hiyo ni Mkutano wa Mawaziri wa Fedha inayoshughulikia sera na utulivu wa Sekta ya fedha (International Monetary Committee and Finance Committee-IMFC
Dkt. Mpango atashiriki katika majadiliano na viongozi wa juu wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF wanaoshughulikia masuala ya Afrika kuhusu utekelezaji wa program za sera za kiuchumi, mikopo nafuu na misaada ya kitaalam kwa Tanzania.
Mazungumzo hayo yatajikita kwenye maeneo ya mwenendo wa uchumi wa dunia; miradi ya maendeleo iliyopendekezwa na Benki ya Dunia kwa mwaka 2019/20, kujenga uwezo wa rasilimali watu, mahitaji ya kujenga uchumi wa kidijitali na maeneo mengine ambayo Benki ya Dunia inaweza kusaidia kupatikana mikopo nafuu ya kugharamia miradi ya kipaumbele hasa reli na umeme.
Waziri wa Fedha pia anatarajia kupata fursa ya kukutana na Taasisi na mashirika mbalimbali ya kimataifa, washirika wa maendeleo na wawekezaji wenye nia ya kuwekeza katika sekta mbalimbali nchini.
Dkt. Mpango pia ameihakikishia Jumuiya ya Kimataifa na watanzania kwa ujumla kwamba Tanzania inafanya vizuri kiuchumi na kijamii na kumpongeza Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Wilson Masilingi, kwa jitihada kubwa anazozifanya kuitangaza nchi na kusukuma mbele agenda za nchi
Kwa Upande wake, Balozi Wilson Masilingi, akiukaribisha ujumbe wa Tanzania nchini Marekani, amebainisha kuwa yeye na timu yake wamejipanga kuhakikisha ushiriki wa nchi katika mikutano hiyo unakuwa mzuri na wenye manufaa na mafanikio kwa Taifa.
No comments:
Post a Comment