ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, April 10, 2019

KITENGO CHA MARADHI YASIYOPEWA KIPAUMBELE KUMALIZA MARADHI YA KICHOCHO NA MATENDE IFIKAPO MWAKA 2030 ZANZIBAR

 Kaimu Meneja Kitengo cha Maradhi yasiyopewa kipaumbele Salum Mohd Aboubakar akitoa taarifa ya maradhi Kichocho, Matende na Minyoo katika mkutano wa tathmini uliofanyika Kitengo Shirikishi cha Mama na Mtoto Kidongochekundu Zanzibar.
 Baadhi ya washiriki wa mkutano wa tathmini utendaji kazi wa Kitengo cha Maradhi yasiyopewa kipaumbele wakifuatilia mkutano huo uliofanyika Kitengo Shirikishi cha Mama na Mtoto Kidongochekundu Zanzibar.
Afisa wa Takwimu za Afya Wilaya ya Mjini Said Yussuf Mohd akitoa takwimu ya maradhi yasiyopewa kipaumbele katika wilaya yake kwenye mkutano wa tathmini uliofanyika Ukumbi wa Kitengo Shirikishi cha Mama na Mtoto Kidongochekundu Zanzibar.

Na Ramadhani Ali Maelezo Zanzibar
Wizara ya Afya Zanzibar kupitia Kitengo cha Maradhi yasiyopewa Kipaumbele (NTD) imepanga kumaliza tatizo la Maradhi ya Kichocho na Matende ifikapo mwaka 2030 iwapo jamii itatoa ushirikiano mzuri kwa kitengo hicho.

Akitoa taarifa katika mkutano wa kutathmini utendaji kazi, Kaimu Meneja wa Kitengo cha NTD cha Wizara ya Afya Salum Mohd Aboubakar alisema maradhi ya Kichocho kwa sasa yamepungua hadi kufikia asilimia moja na matende yamekuwa yakionekana katika sehemu chache Zanzibar

Alisema hatua hiyo imefikiwa baada ya Kitengo kufanya juhudi kubwa ya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu maradhi yasiyopewa kipaumbele na kuweka utaratibu wa kupita skuli za msingi kuwatibu wanafunzi.

Hata hivyo alisema bado baadhi ya wananchi wamekuwa wazito katika kutumia dawa za kupambana na maradhi hayo zinazotolewa kupitia viongozi wa shehia kwa visingizio visivyo na msingi.

Aliishauri jamii kuunga mkono juhudi za Serikali katika kupambana na kumaliza maradhi yasiyopewa kipaumbele yakiwemo Kichocho, Matende, Minyoo na Vikope.

Mkuu wa Kitengo cha Maradhi yasiyopewa Kipaumbele Pemba Saleh Juma Mohd alisema Kisiwa hicho ambacho kwa miaka mingi kimekuwa kikisumbuliwa na maradhi ya Kichocho hivi sasa yamepungua baada ya kupata Mradi maalum wa kutokomeza maradhi hayo unaofadhiliwa na Serikali ya watu wa China.

Alisema kupitia Mradi huo, wameteua vijiji vinne vilivyokuwa vikisumbuliwa na maradhi hayo ambavyo ni Mtangani, Kiuyu minungwini, Wingwi na Uwandani kupita kwenye mito na kutia dawa kwa lengo la kuuwa makonokono yanaosababisha maradhi ya Kichocho.

Saleh alisema katika maeneo hayo maradhi ya kichocho sio tatizo tena na wanafanya juhudi ili Mradi huo uweze kufanya kazi kisiwa chote cha Pemba na hatimae ufike Kisiwa cha Unguja.

Baadhi ya washiriki wa mkutano huo walisema dhana ya Ugatuzi bado haijaeleweka vizuri kwa baadhi ya maafisa wa Serikali na inaonekana kuwa ni moja ya tatizo katika kukabiliana na Maradhi yasiyopewa kipaumbele.

Walishauri kutolewa elimu zaidi kwa watendaji wa taasisi zilizofanyiwa Ugatuzi na viongozi wa Halmashauri ili kila mmoja aelewe majukumu na mipaka ya kazi yake bila ya kuingilia eneo la kazi ya mtu mwengine.

No comments: