ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, April 18, 2019

MARIAM WA SINGIDA ANAYETESEKA KWA KIDONDA AFIKISHWA MUHIMBILI

BINTI Mariam Rajab (25), mkazi wa Singida ambaye video yake imesambaa kwenye mitandao ya kijamii akiomba msaada wa matibabu, amewasili katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), saa 6:00 usiku wa kuamkia leo na kupokelewa katika Idara ya Magonjwa ya Dharura ambapo anaendelea kufanyiwa vipimo vya awali na kisha atalazwa ili aonane na jopo la madaktari bingwa wa upasuaji kwa ajili ya kupatiwa matatibu zaidi leo Alhamisi.

“Mimi naitwa Mariam Rajabu naishi katika Mkoa wa Singida, Mtaa wa Mnung’una, naishi katika familia ya kimasikini. Wazazi wangu hawana uwezo wa kunisaidia tatizo langu, ambalo ni kidonda kilichoko mgongoni. Nawaombeni Watanzania wenzangu mnisaidie niweze kwenda Hospitali ya Muhimbili niweze kupata matibabu. Sina cha kuwalipa bali Mungu atawalipa, asanteni,” hayo ni maelezo aliyotoa Mariam kupitia video iliyosambaa katika mitandao ya kijamii mwanzoni mwa wiki hii.

Kutokana na taarifa hiyo, Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, aliuagiza uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili kumtafuta Mariam ili apelekwe hospitalini hapo kwa ajili uchunguzi na matibabu.

Mariam alianza safari ya kupelekwa Muhimbili kwa gari la wagonjwa (ambulance) kutoka Singida iliyoanza safari saa 8:00 mchana jana.

Tutaendelea kuwapa taarifa zaidi juu ya mwenendo wa matibabu yake. Habari kwa Hisani ya Muhimbili National Hospital. GBL

No comments: