Wajumbe wa Tume na Wasimamizi wa Uchaguzi Mdogo kwenye Jimbo la Arumeru Mashariki na Kata Sita (6) za Tanzania Bara utakaofanyika Tarehe 19 Mei mwaka huu wakifuatilia mada iliyokuwa ikiwasilishwa. Mafunzo kwa wasimamizi hao yamefanyika Jijini Dodoma leo (Ijumaa Tarehe 12.04.2019) chini ya uratibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). (Picha kwa Hisani ya NEC)
Wasimamizi wa Uchaguzi Mdogo kwenye Jimbo la Arumeru Mashariki
na Kata Sita (6) za Tanzania Bara utakaofanyika Tarehe 19 Mei mwaka
huu wakila kiapo wakati wa mafunzo yaliyoandaliwa kwa ajili yao na
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jijini Dodoma leo (Ijumaa Tarehe
12.04.2019). (Picha kwa Hisani ya NEC)
Wasimamizi wa Uchaguzi kwenye Uchaguzi Mdogo wa Arumeru Mashariki na Kata Sita (6) za Tanzania Bara unaotarajiwa kufanyika Tarehe 19 Mei mwaka huu wametakiwa kuwa na weledi ili kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na wa haki.
Akifungua mafuzo kwa wasimamizi hao Jijini Dodoma leo (Ijumaa Tarehe 12.04.2019), Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Mhe. Jaji (Rufaa), Mbarouk Salum Mbarouk amewaambia wasimamizi hao kwamba weledi utapatikana kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na maelekezo ya Tume.
Jajji Mbarouk amewakumbusha kuwa Tume ndiyo yenye jukumu la kusimamia, kuendesha na kuratibu Uchaguzi, lakini watakaosimamia jukumu hilo kwa karibu ni wao (wasimaizi) kwa sababu wanabeba dhamana katika Jimbo hilo na Kata hizo sita.
Aidha, kiongozi huyo aliwaambia kuwa wanapaswa kuhakikisha kuwa wanazingatia maelekezo watakayopewa na Tume, kuzingatia matakwa ya Katiba na Sheria zinazosimamia Uchaguzi badala ya kufanya kwa mazoea.
Pamoja na hayo, Jaji aliwaeleza Wasimamizi na Wasimamizi Wasaidizi hao kuwa wanapaswa kujiamini na kujitambua kwa sababu wameaminiwa na Tume na wahakikishe kwamba wanayajua maeneo yao ya uchaguzi vyema.
Amesema chaguzi hizo ndogo zitajumuisha wapiga kura 211,741 waliojiandikisha Katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika vituo 567 vya kupigia kura.
Kaimu Mkurugenzi wa Uchaguzi, Bi. Givenes Aswile aliwakumbusha washiriki hao wa mafunzo kuwa wanapaswa kuhakikisha kwamba chaguzi hizo zinafanyika bila kuwa na dosari ili kupunguza malalamiko na mashauri mahakamani.
Kaimu Mkurugenzi aliwakumbusha pia Wasimamizi na Wasimamizi Wasaidizi hao kuwa wanatakiwa kuwepo maeneo ya kazi muda wote katika kipindi cha kutoa fomu za uteuzi, siku ya uteuzi, wakati wa kampeni, siku ya kupiga kura, kuhesabu na kujumlisha kura hadi kutangaza matokeo ya Uchaguzi.
Bi. Aswile aliwaambia kuwa wajiepushe na migogoro ya Vyama vya siasa kwa kutotoa fomu za uteuzi kwa wagombea wawili wa Chama kimoja cha Siasa. Kila Chama kinatakiwa kumdhamini Mgombea mmoja tu.
Wakati wa Kampeni, Kaimu Mkurugenzi aliwakumbusha kwamba wanatakiwa kuunda Kamati za Maadili Ngazi ya Jimbo kwa Ubunge na Kamati ya Maadili Ngazi ya Kata kwa Udiwani ili kushughulikia kwa haraka malalamiko kama yatakuwepo.
Kata zenye uchaguzi ni pamoja na Uwanja wa Ndege iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda Mkoani Katavi, Kitobo iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi Mkoani Kagera, Kyela iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Kyela Mkoani Mbeya, Mikocheni iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni Mkoani Dar es Salaam, Mvuleni iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Lindi Mkoani Lindi na Manda iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma.
No comments:
Post a Comment