ANGALIA LIVE NEWS

Monday, April 15, 2019

WATUMISHI WA TUME WANAOSHIRIKI KATIKA UKAGUZI WA RASILIMALI WATU KWA TAASISI 56 WATAKIWA KUZINGATIA MAADILI

Kaimu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Richard Odongo (aliyesimama) akisisitiza jambo kwa watumishi na Maafisa wa Tume (jijini Dar es Salaam) watakaoshiriki katika Ukaguzi wa Rasilimali watu kwa Mikoa mitano yenye jumla ya Taasisi 56, kuangalia namna masuala ya rasilimali watu yanavyosimamiwa kwa kuzingatia Sheria. (Picha na Ofisi ya Rais – Tume ya Utumishi wa Umma)

Watumishi wa Tume ya Utumishi wa Umma wanaoshiriki katika Ukaguzi wa Rasilimali watu  katika Mikoa mitano yenye jumla ya Taasisi 56 zilizopo nje ya Mkoa wa Dar es Salaam kwa lengo la  kuangalia kiwango cha uzingatiaji wa Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo katika usimamizi na uendeshaji wa Rasilimali watu katika Utumishi wa Umma wametakiwa kuzingatia maadili.

Kaimu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma,   Richard Odongo amezungumza na watumishi wa Tume pamoja na maafisa wanaofanya ukaguzi huo jijini Dar es Salaam na amewaasa kuzingatia maadili na wahakikishe wanatekeleza jukumu hili kwa uadilifu na uaminifu  mkubwa.

Odongo amesema kuwa Watumishi wa Tume wanaokwenda kufanya ukaguzi huo wanapaswa watambue kuwa wamebeba dhamana kubwa ya Tume ya Utumishi wa Umma hivyo wakati wote wajiepushe na mienendo isiyofaa, wakatekeleze jukumu hili la kisheria la ukaguzi wa rasilimali watu kwa weledi, wazingatie maadili na wahakikishe wanatoa maamuzi ya haki na taarifa sahihi na kwa wakati.


Mikoa itakayokaguliwa ni Dodoma, Morogoro, Pwani, Mbeya na Mtwara; miongoni mwa Taasisi 56 zitakazokaguliwa ni pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu); Wizara ya Nishati; Wizara ya Madini; Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; Tume ya Utumishi wa Walimu; Ofisi ya Taifa ya Takwimu na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Ukaguzi huo ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu ya Tume yaliyopangwa kufanyika katika mwaka huu wa fedha wa 2018/2019 ambapo Tume  tayari imefanya ukaguzi kwa Taasisi 33 zilizopo katika Mkoa wa Dar es Salaam.

Tume pia inatarajia kufanya ukaguzi mwingine katika Mikoa mingine mitano ambapo jumla ya Taasisi 61 zitakaguliwa, lengo likiwa ni kuangalia ni kwa kiwango gani masuala ya Rasilimali Watu yanasimamiwa na kuendeshwa kwa mujibu wa Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo mbalimbali katika Utumishi wa Umma; kuimarisha utendaji na uwajibikaji unaozingatia malengo na matokeo yanayopimika.

No comments: