ANGALIA LIVE NEWS

Monday, April 8, 2019

WAZIRI MKUU ATEMBELEA KAMBI YA SERENGETI BOYS

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikabidhiwa kombe kutoka Nahodha wa timu ya Serengeti Boys, Morice Michael katika ofisi ya ubalozi wa Tanzania nchini Rwanda, April 7,2019, kufuatia timu hiyo kuibika bingwa katika mashindano maalum kimataifa yaliyofanyika nchini humo. Mashindano hayo yalishirikisha timu za umri wa chini ya miaka 17 kutoka nchi tatu ambazo ni Tanzania, Cameroon na wenyeji Rwanda. Wanaoshangilia kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Rwanda, Ernest Mangu na Mkurugenzi wa Ufundi wa timu ya Serengeti Boys, Khalid Abdallh.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Cherie Blair ambaye ni Mke wa Waziri Mkuu wa Zamani wa Uingereza, Tony Blair walipokutana katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kigali nchini Rwanda April 8, 2019. Majaliwa na Cherie walikuwa wakitoka kuhudhuria hafla ya kumbukumbu ya miaka 25 ya mauaji ya kimbari nchini humo iliyofanyika April 7, 2019. Katikati ni Balozi wa Tanzania nchini Rwanda, Ernest Mangu.
 Waziri Mkuu akiwa katika picha ya pamoja na Timu ya Serengeti Boys .katika Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania. Kigali Rwanda April 7, 2019. PICHA NA OFISI YA WAZIRI MKUU

*Asema Watanzania wanamatumaini makubwa kwao, waongeze bidii,

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ametembelea kambi ya timu ya Taifa ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 na kuwaeleza kuwa Watanzania wanamatumaini makubwa dhidi yao, hivyo waongeze bidii.

Alitembelea kambi hiyo Serengeti Boys iliyoko katika jiji la Kigali nchini Rwanda. Waziri Mkuu alikwenda Rwanda Aprili 7, 2019 kumuwakilisha Rais Dkt. John Magufuli kwenye kumbukumbu za miaka 25 ya mauaji ya Kimbari.

Akizungumza na wachezaji hao jana (Jumapili, Aprili 8, 2019) Waziri Mkuu aliwataka vijana wanaounda timu hiyo ya Serengeti Boys wahakikishe wanafanya mazoezi ya kutosha ili waweze kushinda mechi zinazofuata.

“Watanzania wanamatumaini makubwa dhidi yenu nasi tunazidi kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu muweze kuibuka na ushindi katika michezo yenu iliyobakia itakayowawezesha kushiriki mashindano ya kombe la dunia.”

Kadhalika, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuipongeza timu hiyo ya Serengeti Boys kwa namna wanavyoitangaza nchi kimataifa kupitia kwenye mashindano mbalimbali wanayoshiriki na kuibuka na ushindi.

Waziri Mkuu alisema endapo timu hiyo ya Taifa ya vijana ya Serengeti Boys itaibuka na ushindi katika michezo yake miwili itakuwa imekata tiketi ya kushiriki mashindano ya dunia huko nchini Brazil kwa vijana wa umri wa miaka 17.

Kwa upande wao, wachezaji na uongozi wa timu ya Serengeti Boys walimkabidhi Waziri Mkuu kombe walilolipata baada ya kuichapa timu ya Rwanda katika mashindano maalumu kwa ajili ya kujiandaa na AFCON-U17.

Mashindano hayo maalumu ya Kimataifa yalishirikisha timu za umri wa chini ya miaka 17 kutoka nchi tatu ambazo ni Tanzania, Cameroon na wenyeji Rwanda, ambapo Serengeti Boys ilishinda mabao mawili kwa moja dhidi ya Cameroon na kutoka sare ya mabao matatu kwa matatu na Rwanda.

Pia, wachezaji hao wamemuahidi Waziri Mkuu kwamba watajitahidi kadiri ya uwezo wao kuhakikisha wanaibuka na ushidi katika mechi zilizobakia ili waweze kushiriki kombe la dunia. “Hatutawaangusha Watanzania.”

Awali, Waziri Mkuu alimshukuru Balozi wa Tanzania nchini Rwanda, Mheshimiwa Balozi Ernest Mangu pamoja na maofisa wa ubalozi na Watanzania waishio Rwanda kwa kuendelea kuipa moyo Serengeti Boys.

No comments: