ANGALIA LIVE NEWS

Friday, May 3, 2019

SERIKALI KUSHIRIKIANA NA TLS- AG

 Ujumbe wa Baraza la Uongozi la TLS wakiwa katika mazungumzo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali baadhi ya mambo yaliyojadiliwa ni kuhusu namna bora ya kuhakikisha sheria ambazo zimefanyiwa urekebu na baada ya kupitishwa na Bunge zinawafikia wadau kwa wakati. Pia walijadiliana kuhusu haja na umuhimu wa kuzifanyia urekebu wa baadhi ya sheria zenye changamoto.
 Mwanasheria Mkuu wa Serikali Profesa Adelardus Kilangi akisisitiza kwa Baraza la Uongozi la TLS likiogozwa na Rais wake Dk. Rugemeleza Nshala kwamba Serikali itashirikiana na TLS,Wakati Baraza hilo lilipomtembelea na kufanya mazungumzo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Ofisini kwake Mitumba- Ihumwa Jijini Dodoma. Mazungumzo hayo yalifanyika jana alhamisi.
  Rais wa TLS Dk. Rugemeleza Nshala akimkabidhi Mwanasheria Mkuu wa Serikali shajala za TLS mara baada ya mazugumzo yao yaliyowajumuisha pia wajumbe wa Baraza la Uongozi la TLS.
Picha ya pamoja baada ya majadiliano baina ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Baraza la Uogozi wa TLS. Walioketi mbele kuanzia kushoto ni Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dk Evaristo Longopa, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Profesa Adelardus Kilangi, Rais wa TLS Dk. Rugemeleza Nshala na CEO wa TLS. Picha na habari kwa hisani ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Profesa Adelardus Kilangi, amesema, Serikali inatambua mchango wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika ( TLS) katika kuimarisha na kudumisha Utawala wa Sheria nchini. Akasema wakati wote Serikali ipo tayari kupokea maoni na ushauri kutoka TLS ilimradi kwamba, maoni au ushauri huo unajikita katika kujenga, kuimarisha, hauegemei upande wowote, wenye staha na usio na mashinikizo.

“ Kwanza niwashukuru sana kwa kuja kukutana na kufanya mazungumzo nami, niwapongeze wewe Rais kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa TLS pamoja na wote mliochaguliwa katika baraza la uongozi. Ni matumaini yangu kwamba, hamtawaangusha wanachama wenu waliowachagua, msiwaagushe tafadhali” Akasema Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kuongeza

“Wakati wote Serikali imekuwa ikithamini sana mchango wenu na maoni yenu. Na kwa kweli mmekuwa mkitoa mchango na maoni mazuri sana, niwahakikishe kwamba Serikali wakati wote ipo tayari kushirikiana nanyi. Jambo la muhimu ni kuwa na majadiliano ( dialogue) pale ambapo mnaona kunajambo la kujadiliana kabla ya kulitolea matamko.

“Niwahakikishe kwamba, Serikali kwa ujumla na hasa Mhe. Rais John Pombe Magufuli katika uongozi wake anapenda sana Sheria na anataka mambo yafanyike kisheria na kwa kuzingatia sheria ” akasisitiza Profesa Kilangi Profesa Kilangi ameyasema hayo wakati alipokutana na kufanya mazungumza na ujumbe wa Balaza la Uongozi la TLS likiongozwa na Rais wake Dk. Rugemeleza Nshala.

Mazungumzo kati ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Ujumbe wa Balaza la Uongozi yaliyochukua zaidi ya masaa matatu, yalifanyika siku ya Alhamisi katika ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mitumba- Ihumwa Jijini Dodoma. “Niwaombe sana katika uongozi wenu msimamie sana weledi wa tasnia ya Sheria, hili nawaomba sana, sisi sote ni maofisa wa Mahakama, ni katika mkutadha huu tunatakiwa kutekeleza majukumu yetu ya uofisa Mahakama kwa welidi wa hali ya juu sana na kwa kuzingiatia misingi na maadili ya kazi zetu. Lisimamieni sana hili, simamie professionalism” akasisitiza Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Rais wa TLS Dk, Rugemeleza Nshala pamoja na kumshukuru Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuwakubalia ombi lao na kukutana nao. Alisema kuna mambo kadhaa ambayo walitamani au waliona ni vema wakabilishana naye mawazo. Dk Nshala aliyataja baadhi ya mambo hayo kuwa ni pamoja na kuangalia namna bora itakayowawezesha TLS na wadau wengine wa Sheria nchini, akiwamo Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya kushirikiana katika kuhakikisha kwamba Mawakili wa kujitegemea na Mawakili wa Serikali wanatekeleza majukumu yao kwa weledi na kwa kuzingatia maadili na miiko ya kazi zao.

Jambo jingine ambalo Dk. Nshala kwa niaba ya jumbe wake aliliwasilisha kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni la namna ya kuangalia jinsi ya kuifanyia marekebisho baadhi ya vifungu vya Sheria ya TLS hasa katika kifungu cha uchaguzi wa Viongozi unaotakiwa kufanyika kila mwaka. “Katika mkutano wetu wa Arusha wanachama tulilijadili hili la uchaguzi wa kila mwaka, ni hitajio la kisheria lakini gharama za kukutana kila mwaka ni kubwa sana na zinabebwa na wanachama, hivyo tulijadiliana kuona namna gani tunaweza kuliboresha hili kwa kujadiliana na wadau wengine na kwa kuangalia mifano ya nchi nyingne akasema “ Rais wa TLS.

Dk. Nshala pia alizungumzia kuhusu mitaala ya mafunzo Sheria katika Vyuo Vikuu na kushauri kwamba wadau wa Sheria wanapashwa kukaa na kujadiliana namna bora ya kuuboresha ili iendane na wakati. Kwa mujibu wa Rais huyo wa TLS amesema kwa uzoefu wake na katika utekelezaji wa majukumu yake kuna mifano hai ya mapungufu ya kiutendaji kwa kwa baadhi ya mawakili ambayo mengi kati ya hayo ni ukosefu wa mafunzo Stahiki

Katika hilo la uboreshaji wa mfumo wa ufundishaji, Mwanasheria Mkuu wa Serikali alisema anakubaliana nalo kwa asilimia kubwa, na kwamba , tatizo ambalo yeye analiona ndiyo changamoto kubwa katika tasnia ya Sheria ni mafunzo kwa vitendo. Mwanasheria Mkuu wa Serikali Profesa Kilangi na Uongozi wa TLS walijadili pia kuhusu namna bora ya kuhakikisha kwamba Sheria zinazofanyiwa urekebu na mara zikisha pitishwa na Bunge Ofisi ya Mwanasheria Mkuu isisambaze ili zinawafikia wadau kwa wakati.

Vile vile walibadilishana mawazo kuhusu haja na umuhimu wa kuzifanyia urekebu baadhi ya Sheria ambazo zinamatatizo au changamoto katika utekelezaji wake. Baadhi ya Sheria hizo ni pamoja na baadhi ya vifungu vya Sheria ya Jinai na Sheria ya Usuluhishi wa migogoro nje ya Mahakama.

Walibadilishana mawazo pia kuhusu mazingira ya utendaji kazi wa Mawakili hasa mawakili wa kujitegemea ambao Dk. Nshala alisema wanakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazopashwa kutafutiwa ufumbuzi. Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dk. Evaristo Longopa na Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu na Utoaji wa Huduma Dk. Gift Kweka.

No comments: