ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, May 4, 2019

WAAJIRI NCHINI WATAKIWA KUWAWEZESHA MAKATIBU MUHTASI KUSHIRIKI MIKUTANO YA MWAKA KWA LENGO LA KUINUA TAALUMA ZAO KWA MAENDELEO YA TAIFA.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George Mkuchika (Mb), akizungumza na Makatibu Muhtasi (hawapo pichani) alipokuwa akifungua Mkutano wa mwaka wa Chama cha Makatibu Muhtasi Tanzania (TAPSEA) jijini Arusha.
Baadhi ya Makatibu Muhtasi wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George Mkuchika (Mb) (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati akifungua Mkutano wa mwaka wa Chama cha Makatibu Muhtasi Tanzania (TAPSEA) jijini Arusha.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George Mkuchika (Mb), akipokea zawadi kutoka kwa Mwenyekiti wa Chama cha Makatibu Muhtasi Tanzania (TAPSEA), Bi. Zuhura Maganga baada ya kufungua Mkutano wa mwaka wa Chama cha Makatibu Muhtasi Tanzania (TAPSEA) jijini Arusha.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George Mkuchika (Mb), akimkabidhi zawadi Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Zanzibar, Bw. Seif Shaban Mwinyi ikiwa ni ishara ya kudumisha muungano katika masuala ya utumishi wa umma na utawala bora.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George Mkuchika (Mb), akifurahia jambo na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Zanzibar, Bw. Seif Shaban Mwinyi na Mwenyekiti wa Chama cha Makatibu Muhtasi Tanzania (TAPSEA), Bi. Zuhura Maganga.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George Mkuchika (Mb) amewataka waajiri nchini kuhakikisha wanawawezesha Makatibu Muhtasi katika taasisi zao kushiriki kikamilifu mikutano ya watumishi hao inayofanyika kila mwaka kwa lengo la kuinua taaluma zao kwa faida yao na taifa kwa ujumla.

Mhe. Mkuchika amesema hayo alipokuwa akifungua mkutano wa saba (7) wa mwaka wa Chama cha Makatibu Muhtasi Tanzania (TAPSEA) uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa (AICC) jijini Arusha.

Mhe. Mkuchika amesema kama ilivyo kwa viongozi na watumishi wa sekta nyingine kushiriki mikutano yao ya kitaaluma bila vikwazo, vile vile na Makatibu Muhtasi wawezeshwe kushiriki bila kikwazo chochote kwa kuwa ni haki yao ya msingi ya kukutana na kujadiliana masuala yao ya kitaaluma.

Mhe. Mkuchika ameongeza kuwa, suala la kuwawezesha Makatibu Mahsusi kushiriki mkutano huo lisiwe la sekta ya umma pekee bali na sekta binafsi pia kwani maendeleo huletwa kukiwa na ushirikiano.

“Tunavyozungumzia uchumi wa viwanda ni lazima twende pamoja yaani sekta ya umma na sekta binafsi, hivyo ni jukumu letu kushirikiana ili tuweze kuliletea taifa letu maendeleo,” Mhe. Mkuchika amesisitiza.

Mhe. Mkuchika amewapongeza waajiri waliowawezesha Makatibu Muhtasi wao kushiriki mkutano huo na kusisitiza kuwa ni matumaini yake mkutano ujao watawawezesha watumishi wengi zaidi kushiriki.

Aidha, Mhe. Mkuchika amewataka Makatibu Muhtasi hao kuitumia kwa ufasaha kauli mbiu ya mkutano wao wa mwaka huu isemayo “Tutumie muda wetu vizuri kufanya kazi kwa ufanisi na kuleta tija kazini.”


“Tumieni muda wa kazi vizuri, kuweni wakarimu na wenye weledi mnapowahudumia wageni kwani nyinyi ndio mnaobeba taswira ya ofisi, msipokuwa waangalifu na vinywa vyenu mnaweza kuhatarisha usalama wa ofisi na taifa kwa ujumla,” Mhe. Mkuchika amesisitiza.

Mkutano huo umewashirikisha zaidi ya Makatibu Muhtasi 2000 kutoka Tanzania Bara na Visiwani ukiwa na lengo la kuwambusha watumishi hao na kubadilishana uzoefu katika utendaji kazi ili kuongeza tija zaidi kwa maendeleo ya taifa.


IMETOLEWA NA:
KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI
OFISI YA RAIS (UTUMISHI)

TAREHE 04 MEI, 2019

No comments: