ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, July 25, 2019

KATIBU MKUU WIZARA YA AFYA ATAKA MABORESHO YA HAKI JINAI YAJENGE NA SIO KUKOMOA

 Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Zainabu Chaula akiongea na kikosi kazi kinachofanya Maboresho ya Mfumo wa Haki Jinai jijini Dodoma. Kushoto ni Mkurugenzi Idara ya Katiba na Ufuatiliaji Haki Wizara ya Katiba na Sheria Ndg. Patience Ntwina na kulia ni Mkurugenzi kitengo cha Ugavi na Manunuzi Ndg. David Mwangosi.
Washiriki wa kikao kazi cha Maboresho ya Mfumo wa Haki Jinai wakimsikiliza Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Zainabu Chaula (hayupo pichani), alipotembelea kikosi kazi hicho kinachoendelea na maboresho jijini Dodoma.


Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt Zainabu Chaula ataka Haki Jinai itengeneze katika kujenga na sio kukomoana ili kuwa na jamii bora yenye kufuata misingi ya haki.

Ameyasema hayo alipotembelea kikao kazi cha Maboresho ya Mfumo wa Haki Jinai kinachoendelea Jijini Dodoma kwa ajili ya kuupitia mfumo wa haki jinai nchini na kuangalia changamoto inazoukabili mfumo huo ili kuona kwa pamoja namna ya kufanya maboresho katika Mfumo wa haki jinai nchini.

“Haki Jinai itengeneze katika kujenga na sio kukomoana” amesema na kuongeza kuwa sehemu kubwa ya jamii haina uelewa wa kutosha kuhusu haki zao na hivyo kusababisha kukosa haki hizo na pale wanapofanikiwa kuzijua hawazipati kwa sababu anayetoa haki ni mbabe.

Hivyo akasisitiza elimu ya haki jinai isambae kwenye jamii kupitia njia mbalimbali ikiwemo vipindi vya redio na Runinga  na njia nyingine mbalimbali ambazo zitakuza uelewa kwa jamii ili kuwawezesha kudai haki zao pale zinapokiukwa.

Katibu Mkuu huyo aliongeza kuwa nchi yetu ina mambo mengi mazuri ambayo jamii haiyajui ikiwemo suala zima la Haki Jinai na hivyo kusababisha ukiukwaji wa haki za msingi kwa jamii.

Mfumo wa Haki Jinai unafanyiwa maboresho katika maeneo ya Kisera, kisheria na kiorganizasheni ili kuufanya mfumo huo kuweza kuakisi changamoto za maendeleo zilizopo na zijazo. Aidha, ameipongeza Wizara ya Katiba na Sheria kwa kukutanisha wadau mbalimbali ili kufanya maboresho ya mfumo wa haki jinai nchini.

No comments: