ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, July 31, 2019

Kesi ya DC Chemba kumtaliki mkewe yapigwa kalenda hadi Agosti 5



Mkuu wa Wilaya ya Nchemba, Simon Odunga.
By Tausi Ally, Mwananchi tally@ mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mahakama ya Mwanzo Ukonga, Dar es Salaam Jumatatu Agosti 5, 2019 itaanza kusikiliza kesi ya madai ya talaka namba 181 iliyofunguliwa mahakamani hapo na mkuu wa Wilaya ya Nchemba, Simon Odunga.

Kesi hiyo ilitakiwa kuanza kusikilizwa jana Jumanne Julai 30, 2019 mbele ya Hakimu Christina Luguru lakini imesogezwa hadi Agosti baada ya wahusika kufika mahakamani lakini hawakusikia kesi yao ilipotajwa, hivyo kushindwa kuhudhuria.

Odunga alifunga ndoa kanisa la Sabato na kupata cheti cha ndoa A namba 00140917.

Katika kesi nyingine ya madai ya talaka namba 180 ya 2019 iliyofunguliwa tena mahakamani hapo na Odunga dhidi ya ndoa aliyoifunga serikalini itasikilizwa Agosti 19, 2019.

Katika kesi hiyo ya pili, Odunga anaomba talaka ya ndoa ya Serikali aliyoifunga Februari 21, 2010 na Ruth Osoro na kupewa cheti B namba 0979341.
Analalamikiwa na mkewe kwa kutotoa matunzo ya mtoto wao wa kiume mwenye umri wa miaka minne kwa kipindi cha miaka mitatu.

Licha ya malalamiko hayo, Odunga anaomba mahakamani hapo apewe ridhaa ya kumlea mtoto huyo bila kubughudhiwa.

Katika kesi hiyo ya pili, Odunga anaomba kutoa talaka kwa mkewe huyo kwa sababu amechoshwa na ugomvi na kudhalilishwa sehemu ya kazi.

Hata hivyo, alieleza mahakamani hapo kuwa hana mashaka na malezi ya mama wa mtoto huyo na anataka kumlea mwanaye kuepuka kadhia ya kudhalilishwa kila mahali ikiwapo kazini.

Soma zaidi: Mkuu wa wilaya ya Chemba afungua kesi, ataka kuwataliki wake zake wawili

No comments: