Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza, Godwin Barongo, akifungua warsha ya Mafunzo ya Wawezeshaji wa mpango wa elimu kwa wasichana walio nje ya shule. Warsha hii ya siku nne imefunguliwa rasmi leo tarehe 23 Julai, 2019 na itaendelea hadi tarehe 26 Julai, 2019 ikilenga kuwajengea uwezo wawezeshaji wa mpango huu kuanzisha vituo vya mafunzo na kuendesha mafunzo kwa wasichana walio nje ya elimu rasmi katika wilaya ya Sengerema. Mradi huu unatekelezwa na Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa UNESCO kwa ufadhili wa Shirika la Korea KOICA katika wilaya tatu za Sengerema, Ngorongoro na Kasulu.
Mwezeshaji wa mafunzo yakuwajengea uwezo wakufunzi wa mpango wa kuwajengea uwezo wasichana walio nje ya mfumo rasmi wa elimu katika wilaya ya Sengerema Bi. Leonia Kassamia akiwasilisha mada kwa wawezeshaji wa vituo vya mpango wa elimu mbadala ya wasichana walio nje ya shule, Warsha hii inalenga kuwajengea uwezo wawezeshaji wa mpango huu kuanzisha vituo vya mafunzo na kuendesha mafunzo.
Washiriki wa warsha ya kujenga uwezo kwa wawezeshaji wa vituo vya mpango wa elimu mbadala ya wasichana walio nje ya shule wakiendelea kufuatilia maelekezo ya kuwajengea uwezo wakati wa mafunzo hayo yaliyofanyika Wilayani Sengerema mkoani Mwanza.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza, Ndugu Godwin Barongo akiwa kwenye picha ya pamoja na washiriki wa warsha ya kujenga uwezo kwa wawezeshaji wa vituo vya mpango wa elimu mbadala ya wasichana walio nje ya shule. (wa pili kutoka kushoto).
Na Mwandishi wetu- Sengerema, Mwanza
Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) inaendesha mafunzo ya kuwajengea uwezo wawezeshaji wa mpango wa elimu mbadala kwa wasichana na wanawake walio nje ya shule katika wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza ili kuwajengea stadi za kuwawezesha kujitambua, kutambua mazingira yao na kuchukua hatua sahihi za kujikwamua kiuchumi.
Mafunzo hayo ya siku nne yamefunguliwa rasmi leo na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema Ndugu Godwin Barongo.
Ndugu Barongo amefafanua kuwa, mpango huo umejikita katika maeneo matatu ya kujifunza ambayo ni stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK), stadi za maisha na ujasiriamali zinazoendana na mahitaji ya jamii kwa sasa.
Aidha, ameeleza kuwa wasichana na wanawake hao watapata ujuzi wa kusindika karanga, matunda, mihogo, kutengeneza sabuni na batiki ili waweze kushiriki katika shughuli za kuwaingizia kipato hivyo kuboresha maisha yao na kuchangia katika ujenzi wa Taifa.
Ameongeza kuwa, baada ya mafunzo, wasichana na wanawake hao wataunda na kusajili vikundi vyao ili kupata mikopo ya kujiendeleza inayotolewa na Halmashauri pamoja na asasi mbalimbali zilizojikita katika kukwamua kundi hilo.
Kaimu Mkurugenzi Barongo ameeleza kuwa elimu mbadala inaweza kubadili mtizamo na fikra za jamii juu ya mtoto wa kike kwa kumwezesha kuwa mtu mwenye mchango wa thamani katika maendeleo ya jamii.
Ndugu Barongo amewataka washiriki wa warsha hii kufatilia mafunzo hayo kwa umakini kwani yataweza pia kuwaongezea ujuzi na thamani katika utendaji wao kikazi.
Mpango wa Elimu mbadala unatekelezwa na Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa UNESCO kwa ufadhili wa Shirika la Korea KOICA katika wilaya tatu za Sengerema, Ngorongoro na Kasulu. Mpango huu unalenga kuwafikia wasichana na wanawake 900 walio nje ya shule wenye umri kati ya miaka 14-24.
No comments:
Post a Comment