ANGALIA LIVE NEWS

Monday, July 29, 2019

WAZIRI LUGOLA AMVUA MADARAKA RTO ARUSHA, ATOA ONYO KALI KWA WAKUU WA UPELELEZI MIKOA YA MOROGORO NA MARA

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, akiikagua pikipiki katika Kituo cha Polisi Malinyi, Mkoani Morogoro, leo, ambayo imepata ajali na kusababisha dereva wa pikipiki hiyo kufariki dunia. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Malinyi, Majura Kasike, na Kushoto ni Mkuu wa Kituo cha Polisi, ASP Evaristi Makalla. Majura kasika
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, akimpa maelekezo Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Malinyi, Mkoani Morogoro, SSP Ramadhan Fusi (kulia), wakati alipofanya ziara Wilayani humo, leo Julai 28, 2019.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (kushoto), akikagua kitabu cha taarifa ya mahabusu katika Kituo cha Polisi Malinyi, Mkoani Morogoro, leo, alipofanya ziara kituoni hapo, kwa ajili ya kukagua utendaji kazi wa askari. (Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi).

NA FELIX MWAGARA, MOHA-MALINYI.

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Kangi Lugola amemuondoa madarakani Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Arusha (RTO), Charles Bukombe kwa kosa la kuyapuuza maagizo yake na kuyaita ya kisiasa.

Licha ya kumuondoa katika nafasi hiyo, Waziri Lugola amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara yake, kumchukulia hatua kali za kinidhamu RTO huyo ili iwe fundisho kwa matrafiki hao wa mikoa nchini.

Lugola amesema RTO huyo ameshuhudia katika video ambayo ilikua inasambaa mitandaoni akiwa katika mkutano jijini Arusha, akipinga maagizo yake na kuyaita ya kisiasa na pia kutokuyatekeleza.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara wa wananchi wa Mji wa Malinyi, Mkoani Morogoro, leo, Lugola amesema yeye hatoi maagizo ya kisiasa bali anatoa maagizo yatakayomsaidia rais kazi zake kwa wananchi wanyonge wanaopambana na umaskini na ajira.

“namuagiza katibu Mkuu achukue hatua za kinidhamu ikiwa ni pamoja na kumuondoa u-RTO afanye shughuli zingine za kipolisi, na maRTO ambao mkono wangu haujafika kwenu, na wengine nimeanza kuwaona hamsimamii vizuri maagizo yangu, wapo ambao wanaendelea na uonevu, wapo baadhi ya askari wanaendelea kuchukua rushwa barabarani,” alisema Lugola.

Pia Waziri Lugola ametoa onyo kali kwa MaRTO Mikoa ya Morogoro na Mara akiwataka wachukue fursa ya kujitathimini katika utendaji wao kabla hajawachukulia hatua.

“Wapo baadhi ya askari waonevu, wanaendelea kuchukua rushwa, wajitathimini, katika utendaji wao kabla sijawachukulia hatua kali za kinidhamu,” alisema Lugola.

Lugola katika hotuba zake katika mikutano yake mbalimbali alisema Serikali ya awamu ya tano ni sikivu na haitaki kumnyanyasa mwananchi yeyote kupitia makosa ya trafiki wasiokuwa waaminifu.

Lugola alitoa maagizo kwa Jeshi la Polisi nchini, kuwa bodaboda zinazotakiwa kuwepo kituo cha polisi ni zile zilizopo katika makundi matatu ambayo ni Bodaboda zilizohusika kwenye uhalifu, zilizotelekezwa au zilizookotwa na zilizohusika katika ajali.

“Bodaboida hizo ndizo zinapaswa kuwepo vituoni, lakini kuziweka bodaboda ambazo hazipo katika makundi hayo, napiga marufuku na hii nataka Polisi nchi nzima munielewe,” alisema Lugola.

Pia Lugola aliwataka waendesha bodaboda mjini Malinyi na Tanzania kwa ujumla wafuate sheria za usalama barabarani zikiwemo kuvaa kofia ngumu, kutokubeba abiria zaidi ya mmoja na pia wakiendesha wanapaswa kuwasha taa.

Pia Waziri Lugola amepiga marufuku tabia ya baadhi ya askari Polisi hapa nchini kukamata pikipiki wakiwa hawana sare za Jeshi, anasema kwa kufanya hilo kunaleta kero kwa madereva na pia anayekamatwa anaweza akadhaniwa kuwa ni jambazi.

Lugola anaendelea na ziara yake mkoani Morogoro, na anatarajia kumaliza ziara hiyo Wilaya ya Ulanga Mkoa humo Julai 29, 2019

No comments: