NA HILAL K SUED NA MITANDAO
Wakati ambapo vumbi la siku ya uchaguzi limetulia, inabidi sasa chama tawala cha ANC kilichoshinda siyo tu kiamue kichukue hatua gani dhidi ya Katibu Mkuu wake mtukutu, Ace Magashule, bali pia kwa ujumla chama chenyewe chenye umri wa miaka 107 kinapaswa kijitathmini.
Chama hicho kimeachiwa kusagika na kuoza ndani ya miongo miwili tu iliyopita, na kuendelea kwake kuishi kunategemea namna kinachoweza kutatua matatizo yake, tena kwa haraka.
Matokeo ya kura zilizopigwa zinaonyesha kwamba uungwaji mkono wa chama hicho unazidi kupungua miongoni mwa mamilioni ya wananchi wa Afrika ya Kusini – kutoka asilimia 62 mwaka 2014 hadi 58 mwaka huu.
Miaka kumi tu iliyopita wananchi wasingefikiria kukipigia kura chama kingine chochote isipokuwa hicho kilichowakomboa kutoka minyororo ya utawala wa Wazungu wachache. Lakini siku zinavyopita zinabadilisha mambo.
Kutokana na mwelekeo wa upigaji kura tangu mwaka 2009 ANC imejihakikishia ushindi mmoja mwingine, huenda miwili, kwa kujisukuma sana, kabla hakijapoteza kabisa madaraka.
Vijana ambao miyoyo yao haiko na chama hicho, au chama chochote kingine watajitambulisha sana katika katika kipindi cha chaguzi mbili zijazo.
Medani ya kisiasa inajibadili chini ya miguu ya chama tawala, wakati ambapo wapinzani, wakiongozwa na vijana machachari – siyo tu wale walio juu vyamani, bali pia wale wa ndani ya Bunge.
Umoja miongoni mwa vyama unatarajiwa kuongezeka katika uchaguzi wa serikali za mitaa wa 2021 wakati ambapo miji mingi na manispaa zitagombaniwa. Hivyo kwa ANC kipindi cha kufanya mabadiliko ni sasa.
Lakini kuna masuala mawili yanayojiri ndani ya chama hicho sasa hivi: ajenda ya mabadiliko inayoongozwa na Rais Cyril Ramaphosa; na harakati za wale wenye dhamira ya ‘kukikomboa” chama na kukirudisha mikononi mwa mafisadi – kikundi ambacho kilishamiri sana chini ya utawala wa Jacob Zuma.
Baada ya ANC kupoteza uungwaji mkono kwa kiasi kikubwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2016 – hadi kufikia asilimia 54 – chama hicho kilianza mchakato wa kujitathmini.
Kiliitisha mkutano mrefu wa halmashauri yake kuu (NEC), mkutano ambao ulikuja na taarifa ya kushangaza iliyosema kwamba halmashauri yake hiyo itachukua hatua ya uwajibikaji wa kipamoja kutokana na kufanya kwake vibaya katika uchaguzi ule.
Hata hivyo madai kwamba chama hicho kilikuwa laini sana katika masuala ya ufisadi na migongano ya ndani kwa ndani ndiyo yalitajwa kama sababu ya kupungua uungwaji mkono wa chama hicho.
Uchaguzi huo wa 2016 ulifanyika baada ya kuibuka kwa taarifa kwamba Naibu Waziri wa Fedha Mcebisi Jonas kwamba alipewa uwaziri wa fedha na familia ya Gupta (inayotuhumiwa kwa ufisadi na kulindwa na Zuma), na pia hukumu ya Mahakama ya Katiba (Constitutional Court) kuhusu makazi binafsi ya Zuma kijijini kwake Nkandla, hukumu ambayo ilimtaka Zuma arudishe fedha za umma alizodaiwa kutumia katika “ukarabati” wa makazi hayo yaliyagharimu mammilion iya Dola za Kimarekani.
Aidha taarifa ile ya Halmashauri Kuu ya ANC (NEC) ilisisitiza mapendekezo 15 kwa uongozi wa chama kutekeleza katika kuhakikisha chama kinaondokana na hali mbaya ya uungwaji mkono baada ya uchaguzi wa seikali za mitaa wa 2016.
Lakini hakuna hata pendekezo moja lililotekelezwa au hata kutajwa tena, kwani punde tu chama hicho kiliingia katika kipindi kingine cha kuwania madaraka, suala ambalo liligombaniwa katika mkutano wao kule Nassrec mwaka mmoja baadaye.
Katika mkutano ule hali halisi ya ANC ya leo ilijitokeza – wajumbe 4,000 walimpigia kura Ramaphosa, ambaye walimuona kama chombo cha kuhakikisha chama kinabakia madarakani, lakini pia kilimchagua Ace Magashule – mtu ambaye anawakilisha upande mbaya zaidi kuhusu ufisadi wakati wa kupigania uhuru – kuwa katibu wake mkuu.
Hivyo ujumbe kutoka kwa wajumbe wengi ni kwamba Ramaphosa angekisaidia chama kushinda uchaguzi, na Magashule kuhakikisha kwamba shughuli kuhusu kuneemeka kwa makomredi inabakia ile ile.
RAI
No comments:
Post a Comment