ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, August 3, 2019

Balozi Seif afungua Masikiti mpya wa Ijumaa Kibele

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Ikiwa na Spika Mstaafu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mh. Pandu Ameir Kificho akiufungua Rasmi Msikiti Mpya wa Ijumaa uliopewa jina la Al – Imam Shafii hapo Kibele Shehia ya Tunguu
Mmoja miongoni mwa Viongozi wa Msikiti Mpya wa Ijumaa Kibele Sheikh Amour Pandu Ameir akisoma Risala ya ufunguzi wa Msiki huo Mgeni rasmi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif.
Baadhi ya Viongozi wa Dini, Serikali na Vyama vya Siasa wakifuatilia hafla ya ufunguzi wa Masjid Al – Imam Shafii huko Kibele Mkoa wa Kusini Unguja
Naibu Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Mahmoud Mussa Wadi akitoa maelezo ya kumkaribisha mgenzi Rasmi kuufungua Msikiti wa Ijumaa wa Kibele.
Baadhi ya Waumini wa Dini ya Kiislamu wakifuatilia Hotuba ya Balozi Seif kwenye ufunguzi wa Masjid Al – Imam Shafii Kibele.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Waumini wa Dini ya Kiislamu wakati wa hafla ya ufunguzi wa Masjid Al – Imam Shafii huko Kibele.
Spika Mstaafu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mheshimiwa Pandu Ameir Kificho akitoa shukrani kwa niaya ya Waumini wa Mtaa wa Kibele mara baada ya ufunguzi wa Msikiti wao wa Ijumaa.
Muonekano wa mbali wa Masjid Al – Imam Shafii uliojengwa katika Mtaa wa Kibele Shehia ya Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja.
Spika Mstaafu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mh. Pandu Ameir Kificho Kushoto akimtakia safari njema Balozi Seif mara baada ya ufunguzi wa wa Masjid Al – Imam Shafii iliyopo Kibele.
Picha na – OMPR – ZNZ.


Waumini wa Dini ya Kiislamu Nchini wameombwa kushirikiana kwa kina katika kukomesha vitendo vya udhalilishaji wa Watoto, unyanyasaji wa Kijinsia pamoja na wizi wa mazazo na mifugo ambavyo vimekemewa na Kiongozi wa Dini ya Kiislamu Duniani Mtume Muhammad {SAW}.
Alisema Jamii imekuwa ikishuhudia wimbi kubwa la matukio ya Mmong’onyoko wa maadili katika Maeneo mbali mbali Nchini unaosababishwa na baadhi ya Wakorofi hasa Vijana kujiingiza katika matumizi ya Dawa za Kulevya zenye ushawishi unaopelekea kujiingiza katika matendo maovu.
Akiufungua Rasmi Msikiti Mpya wa Ijumaa uliojengwa katika Kijiji cha Kibele Mkoa wa Kusini Unguja { Masjid Al Imam Shafii } Balozi Seif Ali Iddi alisema juhudi zinapaswa kuelekezwa katika kutoa elimu ya kuachana na matendo hayo maovu sambamba na kujiletea Maendeleo yakilenga zaidi katika Sekta ya Kilimo cha Mazao ya Vyakula na Biashara.
Balozi Seif alisema Serikali imekuwa ikijenga mazingira bora ya kuwaelekeza Wananchi wake katika harakati za kujiletea Maendeleo kwa kuanzisha Mifuko ya Uwezeshaji Kiuchumi inayoambatana na Vikundi vya ujasiri Amali ambayo itawaondoa katika mawazo ya kufikiria mambo yasiyo na msingi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuomba Uongozi uliopewa jukumu la kuuendesha pamoja na kuusimamia Msikiti huo kuwa makini katika kuhakikisha itikadi dhaifu zinazopenyezwa na baadhi ya Watu wakorofi hazipati fursa za kutaka kuvuruga Waumini wa Dini hiyo.
Balozi Seif alitahadharisha kwamba hivi sasa kumejitokeza madhehebu tofauti yanayowachanganya vichwa Waumini mbali mbali kutokana na itikadi zao zinazopingana kabisa na mifumo sahihi ya Dini iliyozoeleka na kutia wasi wasi mkubwa kwa Waumini hao.
“ Siku hizi nasikia kuna madhehebu mbali mbali ambayo yanashamiri kwa ukweli tunatakiwa tujihadhari sana na itikadi zao zinazopingana kabisa na mifumo sahihi ya Dini tuliyoizoea”. Alisisitiza Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimshukuru na kumpongeza Muumini wa Dini ya Kiislamu aliyejitolea Kuujenga Msikiti huo na kuwaomba Waumini watakautumia kwa kufanya Ibada wamuombee Dua kwa Mwenyezi Mungu amjaalie baraka katika shughuli zake za Kimaisha.
“Ye yote nayekufanyieni mambo mema, basi mlipeni na mtakapokosa cha kumlipa basi muombeeni dua kwa Mwenyezi Mungu”. Balozi Seif alikariri maneno hayo ya Kiongozi wa Dini ya Kiislamu Ulimwenguni Mtume Muhammad {SAW}.
Balozi Seif alisema wapo Watu wengi waliobarikiwa kuwa na uwezo mkubwa wa Kifedha lakini kwa bahati mbaya Utajiri wao wanaendelea kuwekeza katika mambo ambayo hayatawasaidia katika Maisha yao ya Milele waendako.
Alifahamisha kwamba zipo Hadithi sahihi zinazoelimisha kwamba Mwanaadamu anapofariki amali zake zote hukatika isipokuwa sadaka inayoendelea kama kujenga Msikit, Madrasa, Kuchimba Kisima, kutoa Elimu yenye kuleta manufaa katika Jamii pamoja na Mtoto mwema anayemuombea Dua Mzazi wake.
Balozi Seif aliedelea kuwakumbusha Waumini wa Dini tofauti pamoja na Wananchi wote wazidishe mapenzi baina yao kwa kushirikiana katika kuiendeleza Amani na Utulivu iliyopo na kuwakataa kwa kutowapa nafasi wale wenye nia ya kutaka kuharibu Umoja na Mshikamano wa Umma.
Akisoma Risala Mmoja Miongoni mwa Viongozi wa Msikiti huo Sheikh Amour Pandu Ameir alisema Ujenzi wa Masjid Al – Imam Shafii ulianza Mnamo Mwezi Juni Mwaka 2018 uliokwenda sambamba na uchimaji wa Kisima ili kuondosha Usumbufu wa upatikanaji wa huduma ya Maji.
Sheikh Amour alisema ujenzi huo umekuja kufuatia kupanuka Kwa Mtaa wa Shehia ya Tunguu pamoja na kuongezeka kwa Idadi ya Waumini waliolazimika kufuata Nyumba ya Ibada katika masafa marefu.
Alisema mategemeo ya uwepo wa Jengo hilo la Ibada kutasaidia kupeleka mbele Dini ya Kiislamu itakayokwenda sambamba na ongezeko la nuru miongoni mwa wakaazi wa eneo hilo lililobarikiwa kuwa na Jengo tukufu la Ibada.
Alifahamisha kwamba Uongozi wa Msikiti huo ulikusudia pia kujenga Madrasa itakayotoa mafunzo ya Dini kwa Watoto na Waumini wanaouzunguuka Msiki huo lakini imechelewa kutokana na nguvu kubwa kulenga katika umaliziaji wa Msikiti huo.
Hata hivyo Sheikh Amour Pandu Ameir amewahakikishia Waumini wa Dini ya Kiislam kwamba nia ya ujenzi wa Madrasa hiyo bado upo pale pale na itaendelea katika siku za hapo baadae.
Akimkaribisha Mgeni Rasmi kuzungumza na Waumini hao wa Dini ya Kiislamu Naibu Mafti Mkuu wa Zanzibar Al Hajj Mahmoud Mussa Wadi amewashauri Waumini wasiopata nafasi ya kwenda kuhiji Makka Nchini Saudi Arabia waongeze Ibada katika Siku Kumi Tukufu zilizo ndani ya kipindi cha Ibada ya Hijja.
Al Hajj Mahmoud aliyataja baadhi ya mambo ya kufanywa katika kipindi hichi ni kuongeza swala za Sunna, kutoa zaka kwa wingi, kuleta tasbihi, kuomba maghfira pamoja na kuwatembelea Wazee wasiojiweza na Wagonjwa.

Masjid Al Imam Shafii una uwezo wa kusaliwa na Waumini wa Dini ya Kiislamu wapatao 300 Kike na Kiume.

No comments: